Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wiki ya unyonyeshaji wa watoto maziwa ya mama, imetupa uzoefu - Wanajamii Tanzania

Mtoa huduma za Afya kitengo cha Mama na Mtoto katika Zahanati ya Kata ya Mkambalani Rebeca Wami akimfanyia vipimo vya ukuaji mtoto huku mama yake akishuhudia  wakati wa wiki ya unyonyeshaji.
Hamad Rashid

Afya

Wiki ya unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa watoto ambayo ilianza tarehe mosi ya mwezi huu wa Agosti na kuadhimishwa duniani kote kwa jamii kuelimishwa kuhusu umuhimu wa mama kumnyonyesha mtoto imehitimishwa jana tarehe 7. Huko mkoani Morogoro nchini Tanzania, kwa wiki nzima mashirika mbalimbali kwa kushirikiana na serikali yamekuwa yakizungumza na wanajamii ili kufahamu uelewa wao kuhusu suala hili la unyonyeshaji na pia kuwapa elimu panapohitajika.

Fadhila Yusufu ni mmoja wa wanawake waliohudhuria maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji mtoto maziwa ya mama na ana mtoto mwenye umri wa miezi sita. Mama huyu ni mkazi wa kijiji cha Mkambalani, hapo hapo mkoani Morogoro, anasema unyonyeshaji kwake ndio kipaumbele kikubwa kwa mtoto wake na anaahidi kwa kusema, “sasa hivi tulivyotoka hapa inamaana tutaongeza juhudi za unyonyeshaji. Dakika 45 mpaka dakika 60.”

Mtoa huduma za afya kitengo cha Mama na Mtoto katika Zahanati ya Kata ya Mkambalani Rebeka Wami anathibitisha wanawake kuwa na mwamko wa kunyonyesha watoto wao kwa mujibu wa malekezo ya wataalamu wa afya.

“Katika siku yetu hii ya unyonyeshaji, tumeweza kupata uzoefu wa kipekee ambao tumeona akina mama wengi wanahamasika na unyonyeshaji wa maziwa pekee kwa mtoto chini ya miezi sita. Na ukanda huu akina mama wengi wanaonekana wamepata elimu na elimu hii imeweza kuwasaidia kunyonyesha watoto wao na kuondoa hali ya utapiamlo.” Anaeleza kwa furaha ya mafanikio mtoa huduma ya afya, Rebeka Wami.
 
Mtoa huduma za Afya kitengo cha Mama na Mtoto katika Zahanati ya Kata ya Mkambalani Rebeca Wami akizungumza na mama ambaye amehudhuria mafunzo wakati wa wiki ya unyonyeshaji.
Hamad Rashid
Mtoa huduma za Afya kitengo cha Mama na Mtoto katika Zahanati ya Kata ya Mkambalani Rebeca Wami akizungumza na mama ambaye amehudhuria mafunzo wakati wa wiki ya unyonyeshaji.

Rajabu Shabani, baba wa familia katika Kijiji cha Mkambalani anasema katika kipindi cha mke wake kunyonyesha huwa anawajibika ipasavyo kumhamasisha. Bwana Shabani anasema, “namchukua mtoto namsaidia kumbembeleza, yeye ananyonyesha mimi ninatumia fursa hiyo kufungua nguo za mtoto hata za kwake mwenyewe. Nimejifunza mengi sana kutokana na malezi ya mtoto. Ushauri kwa akina baba ambao hawashiriki kumsaidia mama, ninawasihi nao wawe na upendo kumsaidia mama wakati wa kunyonyesha.”