FAO yapeleka mbolea Tigray kuimarisha kilimo msimu huu wa upanzi

Hadi leo hii, FAO imeshapeleka tani 19,000 za mbolea sawa na asilimia 40 ya mahitaji kwa kaya 380,000 huko Tigray.
©Michael Tewelde/FAO
Hadi leo hii, FAO imeshapeleka tani 19,000 za mbolea sawa na asilimia 40 ya mahitaji kwa kaya 380,000 huko Tigray.

FAO yapeleka mbolea Tigray kuimarisha kilimo msimu huu wa upanzi

Ukuaji wa Kiuchumi

Huko Tigray, shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo duniani, FAO linaimarisha upatikanaji wa mbolea ili kusaidia wakulima kupanda mazao katikati ya msimu huu wa upanzi na hili linawezekana kutokana na mkopo wa dola milioni 10 ulioidhinishwa na mfuko wa Umoja wa Mataifa wa kushughulikia majanga, CERF.

Taarifa ya FAO iliyotolewa leo huko Roma, Italia inasema fedha hizo ni sehemu ya ahadi za wadau za kusaidia FAO kuchagiza upatikanaji na usambazaji wa pembejeo za kilimo hususuan mbolea huko Tigray, Ethiopia.

Mbolea itasaidia kurejesha kilimo bora na chenye tija miongoni mwa wakulima jimboni humo ambako tangu kuanza kwa mapigano mwezi Novemba mwaka 2022, shughuli za kilimo zimevurugwa, kiwango cha ukosefu wa uhakika wa chakula kimeongezeka, na wakazi hawana mbinu za kujipatia kipato.

Mratibu wa FAO kanda ya Afrika Mashariki na Kaimu Mkuu wa FAO Ethiopia, David Phiri anasema iwapo wakulima watapatiwa pembejeo wanazohitaji, wataweza kuvuna na kuanza kuanza kula mavuno yao mwezi Oktoba mwaka huu.

Amesema mavuno hayo yatakidhi mahitaji ya chakula kwa miezi sita na katika hali bora zaidi yanaweza kufika hadi msimu mwingine wa mavuno na wakawa na ziada ya kuuza.

Kilimo ndio uti wa mgongo wa takribani asilimia 80 ya wananchi wa Ethiopia hasa wale wanaoishi vijijini na mazao wanayolima yanalisha taifa.

Msimu wa sasa wa upanzi ujulikanao Meher ni msimu muhimu kwa uzalishaji chakula na yaelezwa kuwa hali ya mvua ni nzuri na utabiri unaonesha mwelekeo mzuri wa kuongeza uzalishaji na upatikanaji bora wa chakula kwenye eneo hilo.

Hadi sasa FAO na wadau wameshapeleka tani 19,000 za mbolea, sawa na asilimia 40 ya mahitaji kutosheleza kaya 380,000. Shehena ya kwanza ya zaidi ya tani 7,000 ilishasambazwa kwa wakulima Tigray.