Skip to main content

Katibu Mkuu wa UN apewa uraia wa heshima wa Hiroshima

Akiwa Japan, Katibu Mkuu Antonio Guterres(Katikati) alikutana na hibakusha
UN Photos/Ichiro Mae
Akiwa Japan, Katibu Mkuu Antonio Guterres(Katikati) alikutana na hibakusha

Katibu Mkuu wa UN apewa uraia wa heshima wa Hiroshima

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anaendelea na ziara yake nchini Japan baada ya mapema hii leo Jumamosi kuhudhuria sherehe za kuadhimisha miaka 77 ya shambulio la mbomu la nyuklia la Hiroshima lilosababisha maafa ambayo athari zake zinaendelea kuonekana mpaka hii leo. 

Mara baada ya kutoka katika maadhimisho hayo Katibu Mkuu huyo alishiriki katika mambo mbalimbali ikiwemo kushiriki mazungumzo na vijana, mkutano na waandishi wa habari na kikao na viongozi mbalimbali. 

Guterres alikutana na meya wa Hiroshima, na naibu meya wa Nagasaki, na akapewa uraia wa heshima wa Hiroshima.

“Ninakubali heshima hii kubwa kwa niaba ya wanawake na wanaume wote wa Umoja wa Mataifa ambao wanafanya kazi kwa ajili ya amani duniani kote. Ninakubali kwa niaba ya wanadiplomasia na wapatanishi ambao wiki hii hii wanakutana New York, Marekani kuzuia kuenea kwa silaha za nyuklia”. alielezea.

Ashiriki mazugumzo ya vijana

Katika siku hii pia ameshiriki mazungumzo yasiyo rasmi na wanaharakati vijana wa Kijapani wanaoongoza mipango ya uondoaji wa silaha za nyuklia, kutozieneza na masuala mengine ya kimataifa.

“Ningependa kuomba msamaha kwa niaba ya kizazi changu kwa hali ya ulimwengu tunayowaachia kizazi chenu”, alisema, akirudia kuomba msamaha ambao alitoa hapo awali kwa vijana ulimwenguni kote.

 Alizungumza kuhusu hali ya sasa ya dunia, ikiwa ni pamoja na mzozo wa sayari tatu, ukosefu wa usawa unaoendelea, na kuenea kwa vita vya silaha.

“Vizazi vyetu vinahitaji kufanya kazi pamoja ... na kisha nyinyi mtachukua majukumu haya na mnnahitajika kuwa tayari na kuwa katika hali nzuri sana”, aliwaambia washiriki vijana.