Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lindeni wanaharakati wanaohoji utendaji wa kampuni kubwa za biashara Colombia

Mchoro kwenye moja ya kuta nchini Colombia ukiwa na maneno "maridhiano na manusura" ukionesha maendeleo ya kitamaduni katika kujumuisha wapiganaji wa zamani wa kikundi cha FARC nchini Colombia
UN Mission in Colombia/Bibiana Moreno
Mchoro kwenye moja ya kuta nchini Colombia ukiwa na maneno "maridhiano na manusura" ukionesha maendeleo ya kitamaduni katika kujumuisha wapiganaji wa zamani wa kikundi cha FARC nchini Colombia

Lindeni wanaharakati wanaohoji utendaji wa kampuni kubwa za biashara Colombia

Haki za binadamu

Wanaharakati ambao wanaibua shaka na shuku dhidi ya miradi ya kibiashara nchini Colombia wanakumbwa na vitisho kwa sababu ya kuzungumza ukweli, wamesema wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa huku wakitaka serikali ichukue hatua zaidi kuwalinda.
 

Vitisho vikali, ikiwemo kutishiwa kuuawa, ni kawaida nchini Colombia kwa watetezi wanaoibua hofu kuhusu shughuli za kampuni kubwa hasa viwanda vinavyohitaji maeneo makubwa ya ardhi,” amesema Mary Lawlor, Mtaalamu Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali za watetezi wa haki za binadamu, katika taarifa iliyotolewa Alhamisi.

Wataalamu hao wamegusia hali ya Pedro Jose Velasco Tumiña, mtetezi wa haki kutoka kabila la watu wa asili la Misak ambaye amekuwa akipokea vitisho kwa uchechemuzi wake kuhusu masuala ya ardhi.

Harakati dhidi ya madhara ya miradi

Tangu mwezi Julai mwaka jana, watu wa makabila ya asili ya Misak na Nasa pamoja na Campesino wamekuwa wakiandamana huko mkoa wa Cauca, kusini-magharibi mwa Colombia, dhidi ya ardhi inayomilikiwa na Smurfit-Kappa, kampuni inayoongoza duniani kwa utengenezaji wa karatasi.

Hadi mwaka 2021, kampuni hiyo kutoka Ireland imekuwa inamiliki zaidi ya ekari 67,000 za ardhi nchini Colombia na eneo kubwa lina miti ya misonobari na mikaratusi.

Waandamanaji wanapinga madhara yatokanayo na matumizi  ya ardhi hiyo kutokana na shughuli za Smurfit-Kappa, athari za mazingira na haki za binadamu.

Hadi mwaka 2021, kampuni hiyo kutoka Ireland imekuwa inamiliki zaidi ya ekari 67,000 za ardhi nchini Colombia na eneo kubwa lina miti ya misonobari na mikaratusi.

Wanataka utekelezaji wa haki wa vipengele vilivyorekebishwa kuhusu matumizi ya ardhi kwa mujibu wa Mkataba wa kihistoria wa amani wa mwaka 2016 uliomaliza vita vya miongo mitano na waasi wa FARC nchini Colombia.

Watu hao wa jamii ya asili wanasisitiza kuhusu haki yao ya kuchukua ardhi inayomilikiwa na Smurfit-Kappa kwa mujibu wa Mkataba wa Kimataifa wa haki za watu wa jamii ya asili.
Bwana Velasco Tumiña ameanza kupokea vitisho vya vifo tangu mwezi Agosti mwaka 2021, amesema mtaalamu huyo.

Mapema mwaka huu alisafiri hadi mji mkuu wa Ireland, Dublin kuwasilisha malalamiko yao kwa kampuni.Aliporejea nyumbani alipokea kitisho kingine cha kuuawa.

Wataalamu wamesema mtu mmoja ameuawa tangu kuanza kwa vuguvugu la kutetea ardhi ya watu wa asili, na mtu huyo yadaiwa alipigwa risasi na majeshi ya usalama wakati wa maandamano mwezi Agosti mwaka jana.

Wajibu wa kulinda

“Serikali lazima itemize wajibu wake wa kulinda haki za binadamu na ichunguze madai yoyote ya ukiukwaji wa haki,” wamesema wataalamu wa haki za binadamu wakiongeza kuwa “vitisho dhidi ya Pedro vinatisha na lazima vichukuliwe kwa umakini, vivyo hivyo masuala ambayo yeye na wengine wanaibua.”

Wataalamu wametoa pia ushauri kwa serikali mpya ya Colombia ambayo inaanza kazi ramsi Jumapili wakisema, “ili kuhakikisha kampuni za kibiashara zinaheshimu haki za binadamu.

Wamesema  serikali ijayo inapaswa kuhamasisha sekta ya biashara kuzungumza na watetezi wa haki za binadamu. Kampuni kwa upande wake, zinapaswa kueleza hadharani nia yao ya kufanya hivyo hata kama uchechemuzi wa watetezi wa haki unagua operesheni za kampuni.”