Shule ya Kakenya Dream yazidisha mapambano dhidi ya mila potofu kwa jamii za kimasai

5 Agosti 2022

Kenya ni moja ya nchi za kwanza barani Afrika kuridhia mkataba wa kulinda haki za watoto wa Umoja wa mataifa. Ijapokuwa hatua zimepigwa kuimarisha hali ya watoto bado kazi ipo zaidi inayohitaji kufanywa na jamii kwa ujula ili kulinda maslahi ya watoto.

Miongoni mwa changamoto zinazowakabili waoto, hususan wa kiafrika ni mapambano ya mila na tamaduni ambazo zinaweza kuwarejesha nyuma na kuwaathiri maishani. Baadhi zinakiuka haki za watoto.

Mimba na ndoa za utotoni ni maovu yanayosababisha madhila kwa mtoto wa kike kote ulimwenguni.Usawa wa kijinsia ni haki ya msingi ya binadamu kadhalika kiungo muhimu katika harakati za kufanikisha maisha.

Ukeketaji na ndoa za utotoni 

Takwimu zinaashiria kuwa kiasi ya 78% ya wasichana wa jamii ya Wamasai wamekeketwa. Hii ni sawa na wasichana 8 kati ya 10. Nusu ya idadi ya wasichana wa kimasai huolewa kabla ya kutimiza umri wa miaka 19 kimsingi bado ni watoto.

Jason Ole Mooke ni mwanaharakati wa shirika la kijamii la Dupoto-E-Maa linalojikita kwenye miradi ya Elimu na matumizi endelevu ya rasilimali kwa Wamasai na,”kwa Wamasai,mwanamume ndiye mwenye sauti. Kwahiyo sisi wanaume tukiielimisha jamii kuwa ukeketaji unamnyima mwanamke sauti, tutakuwa mbele. Msichana anapovunja ungo anasukumwa kukeketwa ndio akaanze maisha ya unyumba na hilo halileti tija.” 

Baadhi ya mila na desturi zinazomrejesha nyuma mtoto wa kiafrika ni matambiko ya kumtakasa mhusika, mimba na ndoa za utotoni zinazosababishwa kwa kiasi kikubwa na ukeketaji na utamaduni wa kuwa moran kwa vijana wa kimasai. 

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, mwanamke mmoja kati ya watano walio na umri wa miaka 14 hadi 49 wamekeketwa nchini Kenya.Ukeketaji ni haramu na ulipigwa marufuku nchini Kenya mwaka 2011. 

Adhabu yake ni kifungo kisichopungua miaka 3 jela au na kutozwa faini ya shilingi laki mbili.Kwa anayesababisha kifo kwa ukeketaji anaweza kufungwa maisha. 

Ijapokuwa Rais Uhuru Kenyatta aliahidi kuutokomeza ukeketaji ifikapo mwaka 2022, changamoto bado zipo ukizingatia hali ya maisha na athari za COVID 19. 

Kenya imeutenga mwisho wa mwaka 2022 kuwa muda wa mwisho kuutokomeza ukeketaji.

Shule na kituo cha Kakenya Dreams kilichoko nchini Kenya
Thelma Mwadzaya
Shule na kituo cha Kakenya Dreams kilichoko nchini Kenya

Kikosi kazi cha UN kiliunda GESCI 

Umoja wa mataifa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali wako mbioni kuhakikisha kuwa vitendo au tamaduni zozote zinazomrejesha nyuma mtoto wa kike zinaangamizwa. Moja ya njia za kuhakikisha watoto wa kike wanapata msingi mzuri maishani ni kupitia elimu na hifadhi kwenye vituo vinavyowalinda na tamaduni zinazowarejesha nyuma.

Shirika la Gesci lililoundwa 2003 kwa msukumo wa jopokazi la Umoja wa mataifa la teknolojia lina azma ya kuimarisha elimu kwa kutumia teknolojia. 

Samuel Otieno ni mtafiti na mratibu wa mipango katka shirika la GESCI na anaelezea kuwa,”Idadi ya watoto wanaoenda shule imeongezeka japo bado juhudi zinahitaji kuongezwa kasi.Wanafunzi sasa wanahitaji elimu ya kisasa kuweza kupambana na maisha na kuchangia kwenye uchumi na maendeleo.” 

Kituo na shule ya Kakenya iliyoko Kilgoris huko Narok, inawahifadhi wasichana ambao wamekikwepa kisu cha ngariba.Hili linaenda sambamba na lengo la tano la milenia la Umoja wa Mataifa ambalo dhamira yake ni kuangamiza vitendo vinavyomdhuru mtoto kama vile ukeketaji, mimba na ndoa za utotoni.

Christine Kortun ni mzazi na mkaazi wa Lontare kaunti ya Narok na ameona kuwa,”wanafunzi wamebadilika tabia kwasababu ya kufuata maagizo ya wazazi. Mila potofu zinapaswa kuachwa kwani vijana wetu watatatizika baadaye maishani.Iwapo msichana hakeketwi na anaendelea na masomo pindi anapokutana na mvulana ambaye pia amesoma basi jamii yetu inaimarika na wanakuwa mbele zaidi.” 

Elimu ya maisha

Idadi ya wasichana wanaoenda shule imeongezeka kwasababu ya juhudi zilizowekezwa na wadau mbalimbali. Muasisi wa shule ya Kakenya, alifanikiwa kurejea shule hata baada ya kukutana na kisu cha ngariba.Wasichana kwenye kituo hiki hupata hifadhi na kusoma pasina malipo. 

Wakiwa shuleni wanapokea pia elimu ya maisha kuwawezesha kupambana na ulimwengu kupitia mpango wa vijana wa Jijue. 

Gladys Nanyore ni mmoja ya waratibu wa mpango wa Jijue wa mradi wa shule ya Kakenya ya wasichana iliyoko Kilgoris kaunti ya Narok na anakiri kuwa,” Tangu vijana waanze kupata mafunzo na elimu ya maisha kupitia mpango wa Jijue, tumeona tofauti kubwa.Endapo kijana anajikuta katika hali ambapo wazazi wanamlazimisha kukeketwa, elimu wanayopata imewapa ujasiri kukataa.” 

Kwa kawaida watoto wa kiume wa Kimasai hupelekwa jandoni na wanavuka rika kwa njia maalum na kuwa moran.Utamaduni huu unalaumiwa kwa kuendekeza ndoa na mimba za utotoni kwani pindi mvulana anapobaleghe na kwenda jandoni anakuwa haambiliki. 
Hata hivyo wazazi wa kiume wanalipiga vita hilo na wanawashajiisha vijana kutoikumbatia mila hiyo.

Tempaty William ni mkaazi wa Kilgoris na mzazi na kwa mtazamo wake,” Ni muhimu kwa wazazi kuelewa kuwa ipo haja ya kushirikiana ili kupambana na mila na tamaduni ambazo zimepitwa na wakati. Ni sawa kwa wavulana kupashwa tohara lakini kwa wasichana kitendo hicho kina madhara badala ya manufaa.” 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter