Baraza la Usalama la UN lakutana kujadili DRC

4 Agosti 2022

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo Alhamisi limekuwa na kikao cha faragha kuhusu hali ya usalama nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kufuatia matukio kadhaa ikiwemo lile la jumapili iliyopita ambapo walinda amani wa ujumbe wa Umoja huo huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC MONUSCO kuua raia na kujeruhi wengine kwenye eneo la Kasindi jimboni Kivu Kaskazini mpakani na Uganda.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani hii leo amesema Mkuu wa Operesheni za Umoja wa Mataifa za ulinzi wa amani, Jean-Pierre Lacroix alikuwa anatarajiwa kuhutubia wajumbe.

Mkutano huu unafanyika wakati kumekuweko pia na mfululizo wa matukio ya raia kuvamia vituo vya MONUSCO na kupora mali na vifaa wakitaka ujumbe huo uondoke, huku maafisa wa juu wa ujumbe huo wakisema taratibu za kuondoka zinaendelea na kila jambo lazima lifanyike kwa amani.

Bwana Dujarric pia amezungumzia uamuzi wa serikali ya DRC kumtaka msemaji wa MONUSCO kuondoka nchini humo.

“Tunasikitishwa na uamuzi wa serikali ya DRC ya kumtaka msemaji wa MONUSCO aondoke nchini humo. Kwa mujibu wa Chata ya Umoja wa Mataifa, shaka zozote ambazo serikali inakuwa nazo kuhusu vitendo vya mtumishi yeyote wa MONUSCO, zinapaswa kuibuliwa moja kwa moja na uongozi wa ujumbe husika,” amesema Dujarric.

Amesema kwa sasa makao makuu ya Umoja wa Mataifa na viongozi wa  MONUSCO wanazungumza na serikali ya DRC kuhusu suala hilo.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter