Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umri wa mtu kuishi tena akiwa na afya Afrika waongezeka

Kiwango cha umri wa kuishi barani Afrika chaongezeka kwa takribani miaka 10.
WHO Africa
Kiwango cha umri wa kuishi barani Afrika chaongezeka kwa takribani miaka 10.

Umri wa mtu kuishi tena akiwa na afya Afrika waongezeka

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO limesema umri wa kuishi barani Afrika tena akiwa na afya bora, umeongezeka kwa wastani wa miaka 10 kwa mtu mmoja kati ya mwaka 2000 na 2019, ikiwa ni ongezeko la kubwa kuliko ukanda mwingine wa shirika hilo duniani katika kipindi hicho hicho na sababu ni pamoja kuimarika kwa huduma za mama na mtoto.

Taarifa ya WHO kanda ya Afrika iliyotolewa leo huko Brazaville, Jamhuri ya Congo, imenukuu ripoti ya mwaka huu ya kufuatilia huduma ya afya kwa wote kanda ya Afrika, ripoti ambayo imetambua kuwa COVID-19 inaweza kutibua mafanikio hayo.

“Ripoti imebaini kuwa idadi ya miaka ambayo mtu anaishi akiwa na afya njema imeongezeka hadi umri wa miaka 56 mwaka 2019 kutoka umri wa miaka 46 mwaka 2000,” imesema taarifa hiyo ikifafanua kuwa, “ingawa bado tuko nyuma ya wastani wa Dunia wa umri wa kuishi wa miaka 64, bado katika kipindi hicho hicho, wastani wa kuishi duniani uliongezeka kwa miaka mitano pekee.”

Sababu za msingi kwa Afrika kuibuka ‘kidedea’

Kuimarika kwa huduma za msingi za afya, mafanikio katika afya ya uzazi hasa kwa wajawazito, watoto wachanga na afya yam toto. Maendeleo mazuri katika kudhibiti magonjwa ya kuambukiza kama vile UKIMWI, Kifua Kikuu na  Malaria.

“Kwa wastani, utoaji wa  huduma ya afya kwa wote, imeongezeka kutoka asilimia 24 mwaka 2000 hadi asilimia 46 mwaka 2019,” imesema taarifa hiyo.

Muuguzi akimfanyia uchunguzi mjamzito wakati wa kliniki katika kituo cha afya nchini Uganda.
© UNICEF/Zahara Abdul
Muuguzi akimfanyia uchunguzi mjamzito wakati wa kliniki katika kituo cha afya nchini Uganda.

Mafanikio makubwa zaidi ni kuzuia na kutibu magonjwa ya kuambukiza lakini ingawa mafanikio hayo yalitiwa kiza na ongezeko la ghafla la magonjwa kama vile moyo, kisukari na magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza na ukosefu wa huduma za afya zinazolenga magonjwa hayo.

Afrika imejizatiti kuimarisha afya lakini tusibweteke

Akizungumzia ongezeko la umri wa kuishi Afrika, Mkurugenzi WHO kanda ya Afrika, Dkt. Matshidiso Moeti amesema ni ushahidi ya harakati za bara hilo kuboresha afya na ustawi wa wakazi wake.

“Ina maana watu wengi wanaishi maisha yenye afya, wanaishi muda mrefu na wachache wanatishiwa na magonjwa ya kuambukiza na wana huduma bora za kujikinga na magonjwa,” amesema Dkt. Moeti.

Hata hivyo ameonya kuwa maendeleo hayo yasikome kwa kuwa bila hatua za kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile saratani au kansa, mafanikio yaliyopatikana yatatokomea.