Sanamu ya risasi yazinduliwa UN kuenzi wataalamu waliouawa DRC

Katibu Mkuu wa Umoja wa MataifAntonio Guterres na Ann Linde ,Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden wakiwa katika  hafla ya uzinduzi wa Sanamu ya Risasi zilizotumiwa vibaya, iliyotengenezwa na Thommy Bremberg kama kumbukumbu ya Zaida Catalán na Michael Sharp.
Picha ya Umoja wa Mataifa/Mark Garten
Katibu Mkuu wa Umoja wa MataifAntonio Guterres na Ann Linde ,Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden wakiwa katika hafla ya uzinduzi wa Sanamu ya Risasi zilizotumiwa vibaya, iliyotengenezwa na Thommy Bremberg kama kumbukumbu ya Zaida Catalán na Michael Sharp.

Sanamu ya risasi yazinduliwa UN kuenzi wataalamu waliouawa DRC

Masuala ya UM

Sanamu mpya ya risasi kwa ajili ya kuwaenzi wataalamu wawili wa haki za binadamu  wa Umoja wa Mataifa waliouawa miaka mitano iliyopita nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Congo, DRC imezinduliwa hii leo katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres  amezindua sanamu hiyo ya kioo iliyopatiwa jina "Risasi iliyotumiwa vibaya"  ikiwa na umbo la risasi ya dhahabu na kusema itatumika kama kumbukumbu maalum ya wataalamu hao wawili wa haki za binadamu.

Familia za Zaida Catalan na Michael Sharp zimehudhuria hafla hiyo fupi sambamba na wageni wengine wakiwemo wawakilishi wa serikali ya Sweden, Marekani, ambao ni wafadhili wa sanamu hiyo. Mchongaji wa sanamu hiyo Thommy Bremberg alishiriki kwa njia ya video kutoka Sweden.

Shukrani kwa Sweden, Marekani na Mchongaji

Katibu Mkuu Guterres ameshukuru serikali za Sweden na Marekani na kusema “Zaida na Michael walijitolea maisha yao katika kuendeleza haki za binadamu na matendo ya kibinadamu na kusaidia watu walio katika mazingira magumu. Mauaji yao yalikuwa uhalifu wa kikatili."

Yalikuwa ni shambulio dhidi ya maadili ya  Umoja wa Mataifa, amesema Katibu Mkuu, na ushambuliaji wa malengo ambayo wanawake na wanaume wasio na idadi duniani kote wanaweka maisha yao hatarini kuyatetea.

Ameongeza kuwa sanamu hiyo ni heshima kwa malengo yao hayo “kwa kufikiria machungu ambayo vitu visivyo na uhai kama vile risasi, vinaweza kusababisha kwenye vifo na uharibifu.”

Guterres pia amemshukuru msanii Thommy Bremberg “kwa ujumbe wake wa huruma, na kwa kuheshimu mafanikio na kujitolea kwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa.”

“Kwa familia za Zaida na Michael, tunawakaribisha kwa moyo mkunjufu. Asanteni kwa kuungana nasi hapa. Ninataka kutoa tena rambirambi zetu za dhati kwa hasara yanu isiyohesabika,” Alieleza Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa akitoa pole kwa familia za wafiwa.

Zaida na Michael

Zaida na Michael walitekwa nyara tarehe 12 mwezi Machi mwaka 2017 wakichunguza ripoti za mauaji ya kikatili kwenye eneo la Kasai nchini DRC kufuatia mapigano kati ya jeshi la serikali na wanamgambo waliojihami.

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa waligundua miili yao wiki mbili baadaye nje ya mji wa Kananga.

Hatma ya mkalimani wao na waendesha bodaboda watatu haijulikani hadi leo.

Mwezi Januari mwaka huu, mahakama ya kijeshi ya DRC ilihukumu adhabu ya kifo watu 51 baada ya kupatikana na hatia ya kuua wataalamu hao.