Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchunguzi kuhusu askari wa MONUSCO kuhusika katika tukio baya la mauaji DRC unaendelea 

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakisindikiza wapiganaji wa M23 waliojisalimisha Kivu Kaskazini. (MAKTABA)
MONUSCO
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakisindikiza wapiganaji wa M23 waliojisalimisha Kivu Kaskazini. (MAKTABA)

Uchunguzi kuhusu askari wa MONUSCO kuhusika katika tukio baya la mauaji DRC unaendelea 

Amani na Usalama

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akizungumza na waandishi wa habari hii leo Jumanne, Agosti 2, mjini New York Marekani kuhusu mambo mbalimbali yanayoendelea katika Umoja wa Mataifa, ameeleza kile kinachoendelea hivi sasa kuhusiana na tukio baya la mauaji ya raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC lililohusisha askari wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO katika eneo la Kasindi, mpaka wa Uganda na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC.

Msemaji huyo ameeleza kuwa kwa mujibu wa taarifa za awali zilizopatikana, tukio hilo lilitokea katika kituo cha mpakani ambapo Kikosi cha Kujibu Mashambulizi cha MONUSCO, kiliporejea kutoka mapumzikoni, hakikuruhusiwa mara moja kuingia DRC. 

“Wanajeshi hao walisubiri usiku kucha katika eneo kati ya kituo rasmi cha kutoka Uganda na kituo rasmi cha kuingia DRC (katika mpaka wa Uganda na DRC).” Ameeleza. 

Tukio la vurugu lililotokea asubuhi iliyofuata sasa ni jambo la uchunguzi ulioanzishwa na MONUSCO. Walinda amani waliohusika wamezuiliwa kwa amri ya Kamanda wa Kikosi. 

Ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa pia umewasiliana na Nchi inayochangia Wanajeshi ambayo wanajeshi hao wanatoka kwa nia ya kuendeleza uchunguzi wa kimahakama wa kitaifa kuhusu matukio hayo. 

Mnamo Jumapili ya wiki iliyopita yaani tarehe 31 Julai, huko Kasindi, jimbo la Kivu Kaskazini, wanajeshi wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kuleta Amani katika DRC, MONUSCO walifyatua risasi walipokuwa wakirejea kutoka mapumzikoni nchini mwao (haijatajwa bado ili kukamilisha uchunguzi wa awali).  

Taarifa zilisema kuwa wanajeshi hao wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa waliua watu wawili na kujeruhi wengine kadhaa. 

Siku iliyofuata, Agosti 1, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais Félix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kuhusu tukio hilo na pamoja na kutuma salamu za rambirambi, Bwana Guterres aliutumia wasaa huo kuomba radhi. 

Siku hiyo, Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric aliwaeleza waandishi wa habari jijini New York, Marekani kuwa katika mazungumzo hayo pia, Katibu Mkuu alimjulisha Rais Tshisekedi kuwa Umoja wa Mataifa umejizatiti kwenye suala la amani na kuratibiana na kushirikiana na jeshi la DRC, FARDC kutatua hali ya sasa na kuleta utulivu mashariki mwa taifa hilo la maziwa makuu.