Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shukrani kwa UNICEF kutupatia mafunzo ya ndege zisizo na rubani ndani – Vijana Afrika

Debora Mtambalika ni mmoja wa wanafunzi katika chuo cha Afrika cha mafunzo ya kutengeneza ndege zisizo na rubani, ADDA nchini Malawi.
© UNICEF/UNI280220
Debora Mtambalika ni mmoja wa wanafunzi katika chuo cha Afrika cha mafunzo ya kutengeneza ndege zisizo na rubani, ADDA nchini Malawi.

Shukrani kwa UNICEF kutupatia mafunzo ya ndege zisizo na rubani ndani – Vijana Afrika

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Miaka miwili na nusu iliyopita, kupitia hapa hapa katika Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa tulikufahamisha kuhusu kuanzishwa kwa shule ya kwanza ya mafunzo kuhusu takwimu na ndege zinazoruka bila rubani (Drone), ADDA ilipofunguliwa nchini Malawi kwa ufadhili wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.  Sasa shule hiyo inaendelea vizuri na wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali wanaosoma hapo wanaushukuru Umoja wa Mataifa kwa kuwafanikishia elimu hii muhimu itakayosaidia katika maendeleo ya jamii za sasa na kwa siku zijazo.

Atanilson Tucker Cachinjumba, Mwanafunzi kutoka Angola aliyeko katika shule hii ya ndege zisizo na rubani nchini Malawi kwa ufadhili wa UNICEF. Aanasema, “ninashukuru sana kuwa hapa. Na kwa siku zijazo, ningependa kufanya kazi na watoto na vijana kuboresha maisha yao. Ningependa kuchukua maarifa na kufundisha watu wengine. Ili tuifanye teknolojia ya  ndege zisizo na rubani kuwa kitu cha kweli katika nchi yangu.” 

Sithembile Banda ni mwanafunzi mwingine anayesoma katika shule hii. Yeye ni wa humuhumu nchini Malawi. Anasema kujiunga katika shule hii umekuwa uzoefu na imebadilisha maisha yake. Anaeleza kwamba amejifunza mengi zaidi ya alivyodhani angejifunza katika muda mfupi. Amepata marafiki wapya. Amejifunza stadi mpya na hiyo ni vizuri. 

Kijana mwingine Joshua Muranga, yeye anatoka nchini Rwanda. Anasema, hapa tunategemea kwamba kutoka hapa tutakuwa na uelewa wa kutatua matatizo kwa kutumia teknolojia ya kisasa.  

Mnamo mwaka 2020 wakati wa uzinduzi wa shule hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF wa wakati huo, Henrietta Fore alisema “programu za misaada ya kibinadamu na maendeleo barani Afrika zinaweza kunufaika kwa kiasi kikubwa kutokana na matumizi ya teknolojia ya ndege zinazoruka bila rubani.” 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kitengo cha Shirika la masuala ya anga nchini Malawi, James Chakwera alisema, Malawi wanaamini kwamba kukumbatia teknolojia za kisasa kwa mfano ndege zinazoruka bila rubani na tathmini bora ya takwimu na usimamizi kutasaidia kuhudumia watoto weto. Na anaongeza akisema, “tunafuraha kuungana na UNICEF katika ushirkiano huu mzuri.” 

Mtaala wa mafunzo ktika shule hii ulitengenezwa kwa ushirikiano wa taasisi ya mafunzo ya anga Virginia na Chuo Kikuu cha Virgina nchini Marekani kufuatia warsha zao za mafunzo nchini Malawi tangu 2017. Mafunzo katika shule hii yanahusisha  mafunzo darasani na matendo ikiwemo ya kukarabati na kurusha ndege hizo zisizo na rubani.