Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tumechota maarifa YALI, tunapeleka nyumbani Afrika kutekeleza SDGs – Catherine, Hussein na Suzan

Hussein Melele, Mkurugenzi Mtendaji wa Mulika Tanzania.
Picha ya UN
Hussein Melele, Mkurugenzi Mtendaji wa Mulika Tanzania.

Tumechota maarifa YALI, tunapeleka nyumbani Afrika kutekeleza SDGs – Catherine, Hussein na Suzan

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Takribani vijana mia saba, kwa takribani wiki 6, wamekuwa katika vuo vikuu mbalimbali nchini Marekani wamesafiri kupata maarifa ya uongozi kupitia Mpango wa serikali ya Marekani unaolenga kuwaelimisha viongozi vijana wa Afrika ili waweze kuwa viongozi bora katika jamii zao.

Hii ni kwa kutambua kuwa theluthi mbili ya malengo madogo madogo ya malengo yote 17 ya maendeleo endelevu, SDGs kwa njia moja au nyingine yanahusisha vijana kwa lengo la kuwawezesha,kuwashirikisha na kuimarisha ustawi wao na stadi zao za uongozi. Mpango huo uitwao Young Afrikan Leaders Initiative, YALI, ulianzishwa mwaka 2014 na kufikia sasa zaidi ya vijana 5,000 wa kati ya umri wa miaka 25 hadi 35 wamenufaika na mafunzo haya.  

Miongoni mwa vijana hao ambao wameshiriki mafunzo ya hivi karibuni ya YALI kupitia Mandela Washington Fellowship, ni Hussein Melele wa shirika la Mulika Tanzania ambao wanahamasisha ushiriki wa vijana kushiriki katika shughuli za maendeleo, Catherine Shembilu wa kampuni ya Vikapu Bomba na Suzan Yumbe wa shirika la AfyaPlus, wote hawa kutoka Tanzania. 

Wote kwa nyakati tofauti wakihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa walipozuru Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani, wanasema wamejifunza mengi kupitia YALI na wanayapeleka maarifa haya moja kwa moja kwa vijana wenzao na jamii kwa ujumla katika nchi yao.  

Hussein Melele ambaye ni Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lililo la kiserikali la Mulika Tanzania anasema, “mojawapo ya tuliyojifunza ni jinsi wenzetu wanavyopanga mikakati yao. Wanapanga mikakati yao na jinsi ya kuitekeleza na jinsi ya kuifuatilia kuangalia utekelezaji wake umefikia wapi. Sisi wakati mwingine tunapanga mipango lakini hatuiwekei njia sahihi au njia bora ya kuangalia utekelezaji wake.” 

Kwa upande wake Catherine Shembilu ambaye ni Mwanzilishi wa Vikapu Bomba, Kampuni ambayo inafanya kazi na wanawake wasusi wa vikapu katika nyanda za juu kusini mkoa wa Iringa na Njombe nchini Tanzania, ujumbe wake ni kama huo wa kwamba mengi aliyojifunza anayapeleka kwa wanawake wa vijiji ambao amekuwa akifanya nao kazi ili kujikwamua kiuchumi na pia kwamba kupitia mafunzo haya amejifunza zaidi, “kuhusu uongozi wa kibiashara, lakini pia namna ninavyoweza kujenga uhusiano na watu walioko hapa Marekani.”  

Mshiriki mwingine ni kijana, Suzan Yumbe, huyu yeye ni Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Shrika lisilo la kiserikali la AfyaPlus ambao wanajihusisha na kuzuia na kupambana na magonjwa kupitia uwekaji wa mazingira bora ya usafi na kujisafi hususani kwa wasichana balehe na wanawake wa umri mdogo. Je, yeye baada ya kuhitimu mafunzo haya ya uongozi, anaenda kuyatumiaje? 

“baada ya kumaliza mafunzo haya (YALI) ninarudi nyumbani kwenda kutoa mafunzi ya uongozi kwa vijana wenzangu ambao hawajaweza kupata nafasi ya kufika hapa ili waweze kuelewa kwamba uongozi katika mashirika tunatakiwa tufanye kazi na serikali kwa kushirikiana na wadau wengine, lakini pia kuweza kujitambua na kuanzisha miradi ambayo inaenda kunufaisha watu wengi zaidi.” Anasema Suzan.