Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kesi za unyanyasaji kingono zaongezeka kwa asilimia 218 nchini Sudan Kusini

Robo ya visa vya ukatili wa kingono nchini Sudan Kusini ni dhidi ya watoto.
© UNICEF/Mackenzie Knowles-Coursin
Robo ya visa vya ukatili wa kingono nchini Sudan Kusini ni dhidi ya watoto.

Kesi za unyanyasaji kingono zaongezeka kwa asilimia 218 nchini Sudan Kusini

Haki za binadamu

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini UNMISS umeeleza kuwa na wasiwasi mkubwa kutokan na kuongezeka kwa kesi za unyanyasaji wa kingono unaohusiana na migogoro zinazoibuka licha ya kupungua kwa jumla kwa idadi ya raia walioathiriwa na ghasia nchini humo.

Taarifa iliyotolewa leo kutoka Juba nchini Sudan Kusini na UNMISS imeeleeza kuwa ripoti ya hivi karibuni ya Haki za Kibinadamu waliyoitoa ikiangazia robo ya pili ya mwaka huu ilirekodi vifo vya raia 922 ikiwa ni sawa na kupungua kwa asilimia 15 kwa waathiriwa ikilinganishwa na kipindi kama hicho kwa mwaka 2021.

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo Nicholasa Haysom ameeleza jambo la kutia wasiwasi zaidi ni ongezeko la asilimia 218 la unyanyasaji wa kingono unaohusiana na migogoro akimaanisha ubakaji pamoja na ubakaji wa makundi, miongoni mwa aina nyingine za unyanyasaji wa kijinsia unaohusishwa na migogoro katika robo hii.

“Ongezeko kubwa la unyanyasaji wa kingono na kijinsia halikubaliki kabisa, na linawaathiri vibaya zaidi wanawake na wasichana. Ghasia hizi zinazogawanya jamii na kutatiza maridhiano zinafaa kukomeshwa,” akasema Haysom.

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini Nicholus Haysom akizungumza na waandishi wa habari (Hawapo kwenye picha) mjini Juba
UNMISS
Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini Nicholus Haysom akizungumza na waandishi wa habari (Hawapo kwenye picha) mjini Juba

Haki ipatikane kupitia mahakama

UNMISS imesema inaunga mkono mamlaka kuhakikisha kuna uwajibikaji na upatikanaji wa haki kwa walionusurika na waathiriwa kupitia mahakama mbalimbali maalum za kuhamahama kama vile uamuzi wa kesi za ubakaji kupitia mchakato wa Mahakama Kuu ya Kivita huko Yei, Jimbo la Equatoria ya Kati.

Kama ilivyokuwa katika robo ya kwanza ya mwaka huu 2022, migogoro baina ya jamii iliendelea kuwa chanzo kikuu cha madhara ya raia na kusababisha asilimia 60 ya vifo vya raia, wakati asilimia 38 ya vifo vilisababishwa na vikosi vya serikali na Vuguvugu la Ukombozi wa Watu wa Sudan. /Jeshi, wa upinzani ni SPLM/A-IO ambao wanazidi kutegemea wanamgambo washirika kushiriki katika migogoro.

Taarifa hiyo imetoa mfano wa kisa katika Jimbo la Umoja Kusini, ambako ghasia zilisababisha takriban theluthi moja ya vifo vya raia katika kipindi cha kuripoti.

UNMISS imeitaka Serikali ya Sudan Kusini kuchunguza kwa haraka ukiukaji wa haki za binadamu na kuwawajibisha wahusika. 

Huku ikiwa imesalia miezi michache katika kipindi cha mpito, UNMISS umetoa wito wa kuhakikisha kuna utekelezaji kikamilifu wa mkataba wa amani ili kuwezesha sekta ya usalama kutekeleza jukumu la msingi la Serikali la kulinda raia.