Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wajumbe ya tume ya Haki za binadamu wahitimisha ziara yao nchini Ethiopia

Mkimbizi wa ndani akiwa amebeba mwanae huko Mekelle, mji mkuu wa jimbo la Tigray nchini Ethiopia.
©UNICEF/ Esiey Leul
Mkimbizi wa ndani akiwa amebeba mwanae huko Mekelle, mji mkuu wa jimbo la Tigray nchini Ethiopia.

Wajumbe ya tume ya Haki za binadamu wahitimisha ziara yao nchini Ethiopia

Haki za binadamu

Wajumbe watatu kutoka Tume ya Kimataifa ya Wataalamu wa Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Ethiopia wahitimisha ziara yao ya kwanza nchini Ethiopia, iliyofanyika kuanzia tarehe 25 hadi 30 mwezi Julai walipokwenda kujadili masuala kadhaa kuhusiana na mamlaka yao.

Taarifa kutoka Geneva Uswisi na Addis Ababa Ethiopia imewataja wajumbe hao watatu ni Kaari Betty Murungi  rais wa Kenya ambaye n mwenyekiti, Steven Ratner raia wa Marekani na Radhika Coomaraswamy rais wa Sri Lanka.

Wajumbe hao walikutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa serikali, akiwemo Naibu Waziri Mkuu, Waziri wa Sheria pamoja na viongozi wengine wakuu nchini Ethiopia.

Pia walikutana na wajumbe wa Tume ya Kitaifa ya Mazungumzo na Kikosi Kazi cha Mawaziri, wajumbe wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu ya Ethiopia, wanachama wa mashirika ya kiraia, wanadiplomasia, na mashirika ya Umoja wa Mataifa na wafanyikazi nchini Ethiopia kujadili hali ya sasa ya haki za binadamu nchini humo.

Wakati wa mikutano yao na viongozi wa serikali, Tume ilijadili mbinu za ushirikiano, ikiwa ni pamoja na tafsiri yake ya mamlaka yake na kusisitiza maombi waliyotoa ya kupata ruhusa ili kufika maeneo muhimu kwa uchunguzi wake. 

“Tume hiyo imeeleza inamatumaini serikali itawapatia ufikiaji bila kuwa na vizuizi na bila kuchelewa, ili iweze kutembelea maeneo hayo na kuzungumza kwa uhuru na faragha na waathirika, mashahidi, na watu wengine wenye maslahi na masuala watakayo zungumzia.” Imeeleza taarifa hiyo.

Kuhusu Tume hiyo

Tume hiyo yenye wajumbe watatu, iliyoundwa na Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa  tarehe 17 Desemba 2021, imepewa jukumu la kufanya uchunguzi wa kina na usiopendelea upande wowote wa tuhuma za ukiukaji na matumiz mabaya ya sheria za kimataifa za haki za binadamu na ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu na sheria ya kimataifa ya wakimbizi nchini Ethiopia tangu tarehe 3 Novemba 2020 na pande zote kwenye mzozo. 

Tume pia ina jukumu la kutoa mwongozo na mapendekezo kuhusu usaidizi wa kiufundi kwa Serikali ya Ethiopia kuhusu haki ya mpito, ikijumuisha uwajibikaji, upatanisho na uponyaji wa jamii.

Tume iliwasilisha taarifa yake ya kwanza kwa Baraza la Haki za Binadamu tarehe 30 Juni 2022, na imepangiwa kuwasilisha ripoti kamili iliyoandikwa kwa shirika la haki za binadamu katika kikao chake kijacho mnamo mwezi ujao wa Septemba 2022.