Ndui ya nyani ilipuuzwa hadi ilipobisha hodi Ulaya, tubadilike - Dkt. Fall

2 Agosti 2022

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO, limesema nchi zinapaswa kushirikiana kukomesha haraka kuenea kwa ugonjwa wa ndui ya nyani, au Monkeypox bila kujali utaifa, rangi ya mtu au dini, amesema afisa mwandamizi wa shirika hilo hii leo.

Dkt. Ibrahima Soce Fall, Mkurugenzi Msaidizi wa WHO akihusika na dharura amesema hayo wakati akijbu swali la mwandishi wa Habari huko Geneva, Uswisi aliyetaka kufahamu kuchelewa kubadilishwa kwa taarifa kwenye jukwaa la ugonjwa wa ndui ya nyani kufuatia taarifa za vifo nje ya Afrika.

“Kuchelewa huko kunatokana na kuthibitisha takwimu na uratibu na mamlaka za taifa husika,” amesema Dkt. Fall akiongeza kuwa “kwa bahati mbaya, kama ilivyokuwa kwa ugonjwa wa Zika, kuibuka kwa ugonjwa huu nchi za Ulaya ndio kumesababisha dunia nzima sasa kuwa makini kuhusu homa ya ndui.”

Kuingia ndui ya nyani Ulaya kumeamsha watu wengi

Amekumbusha kuwa wamekuwa wakishughulikia ndui ya nyani barani Afrika kwa miaka kadhaa lakini hakuna mtu yeyote ambaye alitilia maanani.

“Ugonjwa huu kwa bahati mbaya uliwekwa kwenye kundi la magonjwa ya kitropiki yanayopuuzwa, NTDs tulihangaika na rasilimali chache na ilihitajika nchi za kaskazini nazo ziambukizwe ugonjwa huu ili dunia ichukue hatua. Ndiyvo ilivyokuwa kwa Zika na lazima tukomeshe ubaguzi huu,” amesisitiza Dkt. Fall.

Tayari WHO ilitangaza tarehe 23 mwezi uliopita wa Julai kuwa ndui ya nyani ni dharura ya afya ya umma duniani, hatua ambayo inalenga kuwezesha shirika hilo kuratibu na kushirikiana na nchi na wadau halikadhalika mshikamano wa kidunia.

Hadi sasa WHO inasema maambukizi barani Ulaya na Amerika kaskazini ni miongoni zaidi mwa wanaume mashoga wenye wapenzi Zaidi ya mmoja.

“Dunia lazima ichukue hatua kulinda jamii hii bila kujali utaifa, rangi yao au dini na kadhalika. Nadhani ni muhimu sana tena sasa ambapo Zaidi ya nchi 70 zina ugonjwa huo hivyo kila mtu anajishughulisha.”

Hadi mwaka huu, ndui ya nyani iliripotiwa barani Afrika na haijawahi kuripotiwa nje ya bara hilo.

Chanjo iliyopitishwa mwaka 2019 dhidi ya ndui ya nyani iko lakini upatikanaji wake bado ni changamoto.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter