Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wiki ya unyonyeshaji: Usaidizi zaidi unahitajika kwa familia zilizopo katika mazingira hatarishi

Mama akimnyonyesha mwanae hospitalini wadi ya kuzaliwa nchini India.
© UNICEF/Vinay Panjwani
Mama akimnyonyesha mwanae hospitalini wadi ya kuzaliwa nchini India.

Wiki ya unyonyeshaji: Usaidizi zaidi unahitajika kwa familia zilizopo katika mazingira hatarishi

Wanawake

Wiki ya Unyonyeshaji watoto maziwa ya mama duniani imeanza rasmi hii leo chini ya kauli mbiu yake isemayo Kuongeza Unyonyeshaji: Elimisha na Usaidizi, Umoja wa Mataifa unatoa wito kwa serikali kutenga rasilimali zaidi ili kulinda, kukuza, na kusaidia sera na programu za unyonyeshaji, haswa kwa familia zilizo hatarini zaidi ambazo zinaishi katika mazingira ya dharura.

Wito huu umetolewa na Mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la kuhudumia watoto UNICEF na la Afya ulimwenguni WHO ambayo kwa pamoja wameeleza maziwa ya mama ndio chanjo ya kwanza inayomlinda mtoto kutopata magonjwa ya kawaida ya utotoni na kumlinda kutopata utapiamlo na udumavu. 

Katika taarifa yao ya pamoja kutoka New York Marekani na Geneva Uswisi mashirika hayo yametolea mfano wakina mama walio katika Pembe ya Afrika, Ukanda wa Sahel, Afghanistan, Yemen na Ukraine kuwa wengi wao wanashindwa kuwahakikishia watoto wao unyonyeshaji kama chanzo salama cha lishe kwakuwa wazazi hao ni wachovu wa kimwili, wanakosa faragha, usafi ni duni na muda wote wakina mama hao wapo kwenye hali ya dharura. 

Ndio maana UNICEF na WHO wanatoa wito kwa serikali,wafadhili, mashirika ya kiraia na sekta binafsi kuongeza juhudi kwenye kuweka kipaumbele kwenye programu za usaidizi wa unyonyeshaji,kuhakikisha wanawapa wahudumu wa afya lishe na ushauri bora ili waweze kuwasaidia wakina mama wanaonyonyesha, kutekeleza sera zinazofaa na zenye kuhakikisha wakina mama wanapata nafasi na usaidizi unahitajika kunyonyesha, na kulinda walezi na wahudumu wa afya wasi washawishi wanyonyeshaji kutumia maziwa ya kutengenezwa viwandani. 

Mama akinyonyesha mwanae nchini Tanzania
UN Photo/B. Wolff
Mama akinyonyesha mwanae nchini Tanzania

Katika hatua nyingine mashirika hayo yametangaza takwimu zinazoonesha chini ya nusu, ya watoto wote wanaozaliwa, hunyonyeshwa katika saa ya kwanza ya maisha yao, na kuwaacha katika hatari zaidi ya magonjwa na kifo. 

Baraza la afya ulimwenguni nalo liliweka malengo ya kunyonyesha watoto bila kuwapa kitu kingine chochote kwa miezi sita wafikie asilimia 50 ifikapo mwaka 2025. Lakini takwimu zilizotolewa leo zinaonesha ni asilimia 44 pekee ya watoto wachanga wanaonyonyeshwa maziwa ya mama pekee katika miezi sita ya kwanza ya maisha. 

Wakati mizozo ya kimataifa ikiendelea kutishia afya na lishe ya mamilioni ya watoto ulimwenguni, umuhimu wa kunyonyesha kama mwanzo bora zaidi maishani umezidi mara dufu kuliko hapo awali.