Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 10 uwepo wa kambi ya Za’atari juhudi zinahitajika kumaliza mzozo wa Syria

Katika kambi ya wakimbizi ya Za’atari huko Jordan, Rawan Majali anaadhimisha sherehe za ufunguzi wa Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake kwa ahadi yake ya chapa ya mkono.
UN Women/Lauren Rooney
Katika kambi ya wakimbizi ya Za’atari huko Jordan, Rawan Majali anaadhimisha sherehe za ufunguzi wa Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake kwa ahadi yake ya chapa ya mkono.

Miaka 10 uwepo wa kambi ya Za’atari juhudi zinahitajika kumaliza mzozo wa Syria

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi duniani UNHCR wiki hii linaadhimisha miaka 10 tangu kufunguliwa kwa kambi ya wakimbizi ya Za’atari iliyoko nchini Jordan kwa ajili ya kuhudumiwa wakimbizi wa Syria. 

Mwakilishi wa UNHCR aliyeko Amman Jordan Dominik Bartsch amezungumza na waandishi wa Habari jijini Geneva Uswisi na kuwaeleza kuwa kambi hiyo imekuwa makazi ya muda ya zaidi ya wasyria 80,000 wake kwa waume na watoto.

Bartsch amesema wiki hii ya miaka 10 inaadhimishwa kwa kutazama fursa mbalimbali za kiuchumi kwa raia wa Jordan na wasyria lakini pia amesihi jumuiya ya kimataifa kusaidia “Kutafuta suluhu za kudumu za kumaliza mgogoro wa syria na wakati huo huo kusaidia changamoto zinazoendelea kuikabili kambi hiyo.” 

Msichana mwenye umri wa miaka sita anafanya mazoezi ya kutembea na magongo mapya katika kambi ya wakimbizi ya Za’atari huko Jordan, karibu na mpaka wa Syria.
© UNICEF/ Shehzad Noorani
Msichana mwenye umri wa miaka sita anafanya mazoezi ya kutembea na magongo mapya katika kambi ya wakimbizi ya Za’atari huko Jordan, karibu na mpaka wa Syria.

Maisha kambini 

Takiwmu za mpaka sasa zinaonesha Jordan ina takriban wakimbizi 675,000 walioandikishwa kutoka Syria tangu mwaka 20211 wakati machafuko yalipobukoa Syria na kusababisha mateso makubwa kwa wananchi wake. Wananchi wa Syria walioko nchini Jordan hawaishi kambini pekee, kuna wanaoishi mijini na vijijini wakichanganyika na wanajamii. Ni asilimia 17 pekee ndio wanaoishi katika kambi za wakimbizi za Za’atari na Azraq.

Zaidi ya watoto 20,000 wamezaliwa kambini tangu ifunguliwe, kizazi hiki hakijui chochote duniani zaidi ya eneo la kambi hiyo walipozaliwa. 

Wahusika wakuu wa kuisaidia kambi hizo ni UNHCR kwakushirikiana na serikali ya Jordan, “Zaidi ya wafanyakazi wa kimataifa 1,200 kutoka mataifa 32 wanahudumia kambini hapa.  Msaada huu wa kibinadamu usingewezekana kuwepo bila ya usaidizi kutoka kwenye jamii ya kimataifa” amesema mwakilishi huyo wa UNHCR nchini Jordan. 
Kambini hapo mpaka sasa kuna jumla ya shule 32, vituo vya kijamii 58, vituo vya afya 8 pamoja na ulinzi wa jamii na vituo vya polisi. “UNHCR tunashirikiana na washirika wetu kutoa ulinzi, huduma ya afya na msaada wa fedha taslimu kwa wanawake, wanaume na watoto katika kambi hii. 

Ndani ya muongo mmoja wa kuwepo kwa kambi hiyo UNHCR na washirika wengine wameweza kujenga magari yanayotumika kama nyumba 25,000 na kila mwezi wanatoa huduma ya matibabu kwa takriban watu 25,000. 

“Kila baada ya miezi minne UNHCR tunatoa fedha taslimu kwa familia zinazoishi kambini. Uwekezaji huu unawasaidia wakimbizi walio kambini kustawi.”

Watoto wakimbizi katika kambi za Zaatari nchini Jordan wakionyesha ishara ya amani
UN Photo/Sahem Rababah
Watoto wakimbizi katika kambi za Zaatari nchini Jordan wakionyesha ishara ya amani

Uchumi wa wakimbizi 

UNHCR imeshuhudia tangu siku ya kwanza wakimbizi wakijishughulisha na ujasiriamali wakiwa na dhamira ya dhati ya kujiinua kiuchumu wakimbizi hao mpaka sasa wana zaidi ya maduka 1,800 na biashara nyingine kambini humo. 

“Wanajishughulisha na shughuli mbalimbali kuanzia kuuza simu mpaka migahawa, maduka ya nguo za maharusi, na vifaa kieletronik. Hizi biashara zimeajiri zaidi ya wakimbizi 3,600” asema Bartsch na kueleza kuwa wakimbizi hao hawafanyi kazi pekeyao kwa kujitenga bali mara kwa mara wanashirikiana na makampuni na wateja walio katika mji wa karibu wa Mafraq na kwa kufanya hivyo wanasaidia kuinua uchumi wa Jordan pamoja na jamii zilizowakaribisha. 

Mahema na vifaa katika kambi ya Za’atari vilifurika kutokana na mvua kubwa iliyonyesha kaskazini mwa Jordan mapema Januari 2013
Photo: UNICEF/Jordan/2013
Mahema na vifaa katika kambi ya Za’atari vilifurika kutokana na mvua kubwa iliyonyesha kaskazini mwa Jordan mapema Januari 2013

Changamoto 

UNHCR ina wasiwasi na uimara wa muda mredu wa nyumba zilizojengwa kama magari kwa ajili ya makazi ya wakimbizi ambayo yalianza kama makazi ya muda na sasa kambi imefikisha miaka 10. 

“Makazi haya yalijengwa ikiw ani mbadala wa maturubai mwaka 2013 , lakini yana kipindi maalum cha kudumu cha miaka 6 mpaka 8 hii inamaanisha kuwa makazi haya yapo kwenye uhitaji wa haraka wa kubadilishwa au kurekebishwa”

Ameeleza mwaka 2021 zaidi ya wakimbizi 7000 waliomba msaada wa marekebisho ya makazi yao kwenye paa na madirisha wakieleza yamepasuka na kuta zimekuwa na nyufa hali inayowaaacha wakazi wake wakikabiliwa na hali mbaya ya hali ya hewa. 

“Utafiti wetu tuliofanya hivi majuzi mwaka huu 2022 tunagundua asilimia 70 ya hali ya kuta katika kambi ya Za’atari ni duni”

Suala lingine aliloeleza ni umeme na kwamba kwa sasa wanalazimika kupunguza mpaka saa 9 kwa siku kutoka saa 11.5 walizokuwa walisambaza na hii ni kutokana na kuongezeka kwa mahitaji hususan katika kipindi cha kiangazi. 

Janga la COVID-19 nalo lilirudisha nyuma maendeleo ya familia nyingi hususan kiuchumi na wananchi wengine kujikuta katika madeni makubwa huku wengine wakipunguza hali kuwa na mlo mmoja ua miwili kwa siku ili kukabiliana na athari za kupanda kwa gharama kwa kiasi cha kutisha. 

Watoto wakimbizi wa Syria wakiwa darasani ndani ya kambi ya wakimbizi ya Za'atari nchini Jordan
Photo: UNICEF Video
Watoto wakimbizi wa Syria wakiwa darasani ndani ya kambi ya wakimbizi ya Za'atari nchini Jordan

Muhimu ni kupata suluhu ya mzozo wa Syria

Mwakilishi wa UNHCR aliyeko Amman Jordan Dominik Bartsch katika kuadhimisha miaka 10 ya kambi ya Za’atari kwa kushrikiana na serikali ya Jordan wametoia wikto kwa washirika kujitolea upya kusaidia maendelo ya wakimbizi na jamii zilizowakaribisha. 

Bartsch amehitimisha kwa kusema iwapo hakutakuwa na suluhu za haraka za kumaliza mzozo wa Syria hali za kibinadamu itazidi kuwa mbaya na kuzorota kwa kuwa mpaka sasa inazorota kwa kiasi cha kutia wasiwasi.

“Wahusika wote wanahitajika kufanya kazi pamoja kutafuta suluhu za muda mrefu kwaajili ya wakimbizi wote wa Syria walioko Jordan na kwingineko na kuunga mkono ustahimilivu wao hadi suluhu hizo zipatikane.”