Skip to main content

Waafrika zaidi ya milioni 91 wanaishi na ugonjwa wa Homa ya Ini wakiwemo watoto chini ya miaka 5

Upimaji wa homa ya ini Togo
UN
Upimaji wa homa ya ini Togo

Waafrika zaidi ya milioni 91 wanaishi na ugonjwa wa Homa ya Ini wakiwemo watoto chini ya miaka 5

Afya

Zaidi ya Waafrika milioni 91 wanaishi na Ugonjwa wa Homa ya Ini aina B au C, ambayo ni aina mbaya zaidi ya virusi, kulingana na chapisho lililotolewa Julai 27,2022 kwenye wavuti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni WHO.

Taarifa ya WHO kanda ya Afrika kutoka Brazaville nchini Congo imeeleza kuwa chapisho hilo la alama za Homa ya Ini kwa mwaka 2021 limeangazia takwimu kutoka kanda ya Afrika lakini limejikita katika Homa ya Ini aina B na C, ambazo husababisha ugonjwa wa cirrhosis na saratani au kansa.

Kwenye ukusanyaji wa taarifa kwa mwaka jana 2021 ilibainika kuwa katika nchi 19, zaidi ya asilimia 8 ya watu wameambukizwa homa ya ini, huku katika nchi 18, zaidi ya asilimia moja ya watu wanaishi na homa ya ini. Mwaka 2020, ukanda wa Afrika ulikuwa na asilimia 26 ya watu wanaougua Homa ya Ini B na C na vifo 125,000 vinavyohusiana na ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika Dkt. Motshidiso Moeti , takriban asilimia 70 ya maambukizi ya Homa ya Ini aina B duniani kote hutokea barani Afrika na inaweza kuchukua miongo kadhaa baada ya kuambukizwa na virusi kabla ya mtu kuanza kudhihirisha dalili.

“Homa ya ini imeitwa janga la kimya, lakini kadi hii ya alama imepiga kengele ya hatari kwa kanda na ulimwenguni kote,” alisema Dkt. Moeti

Mtoto akichomwa chanjo ya Homa ya ini nchini Venezuela
© UNICEF/Cesar Poveda
Mtoto akichomwa chanjo ya Homa ya ini nchini Venezuela

Homa ya ini kwa watoto

Taarifa hiyo pia imeeeleza watoto milioni 4.5 wa Afrika wameambukizwa ugonjwa huo na takwimu za mpaka sasa nchi 33 zina maambukizi ya Homa ya ini aina B kwa zaidi ya asilimia 1 kati ya watoto walio na umri wa chini ya miaka 5, takwimu ambazo zinaonesha kuna maendeleo chanja japo kidogo ikilinganishwa kutoka nchi 40 mwaka 2019.

“Ni lazima tufanye vyema zaidi na kukomesha ugonjwa huu unaoiba maisha ya baadaye ya watoto wetu. Kuna chanjo salama na madhubuti ambayo hutoa kinga ya karibu asilimia 100 dhidi ya Homa ya Ini aina B, mojawapo ya aina hatari zaidi za virusi. Ni lazima tuhakikishe kwamba watoto wote wa Kiafrika wanapata chanjo ndani ya saa 24 baada ya kuzaliwa na kufuatiwa na dozi mbili au zaidi za chanjo hiyo.” Amesema Mkuu huyo wa WHO kanda ya Afrika. 

Uchunguzi uliofanywa na WHO kuangalia maendeleo ya kati ya mwaka 2019 na 2021 umegundua kuwa chanjo ya kawaida ya watoto dhidi ya Homa ya Ini aina B ni asilimia 72 kwa Afrika hii ni chini ya lengo la kimataifa la asilimia 90 linalohitajika ili kuhakikisha kuwa virusi sio tishio la afya ya umma.

Idadi ya nchi zenye chanjo ya zaidi ya asilimia 90 imeongezeka, kutoka nchi 23 mwaka 2019 hadi 27 mwaka 2021. Zaidi ya hayo, wakati chanjo ya dozi ya kuzaliwa inasimamiwa katika nchi 14 pekee za Afrika, kwa chanjo ya jumla ya asilimia 10 ni ongezeko kutoka nchi 11 mwaka 2019.

Kusoma kwa undani kuhusu ugonjwa huu wa Homa ya Ini , namna unavyoambukiza na mengine mengi bofya hapa