Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takribani wahamiaji 50,000 walisaidiwa kurejea nyumbani kwa hiari mwaka 2021

Wahamiaji kutoka Ethiopia waliokuwa wamekwama nchini Yeman wakirejea Addis Ababa kwa msaada wa IOM (Julai 2019)
IOM Bole Addis Ababa International Airport
Wahamiaji kutoka Ethiopia waliokuwa wamekwama nchini Yeman wakirejea Addis Ababa kwa msaada wa IOM (Julai 2019)

Takribani wahamiaji 50,000 walisaidiwa kurejea nyumbani kwa hiari mwaka 2021

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji, IOM linasema mwaka 2021 lilisaidia takribani wahamiaj 50,000 kurejea nyumbani kwa hiari huku shirika hilo likisaidia zaidi shughuli 113,000 za wahamiaji kujumuika tena kwenye jamii zao.
 

Taarifa ya IOM iliyotolewa leo Geneva, Uswisi inanukuu ripoti ya shirika hilo iliyopatiwa jina Vidokezo vya shughuli za ujumuishaji mwaka 2021 ikisema  mwaka jana ulishuhudia ongezeko la mienendo ya watu kuhama.

Hata hivyo kutokana na janga la COVID-19, idadi ya watu wanaorejea nyumbani ni ndogo ikilinganishwa na kipindi cha kabla ya Corona kwani ongezeko la kutoka idadi ya mwaka 2020 hadi 2021 ni asilimia 18 pekee.

“Kama ilivyokuwa mwka 2020, Eneo la Kiuchumi la Ulaya ndio lilikuwa eneo lenye wahamiaji wengi mwaka 2021 ambako wahamiaji 16,993 walisaidiwa kurejea makwao kwa hiari,” imesema taarifa hiyo.

Wahamiaji wakisajiliwa katika Kituo cha Usafiri cha Agadez nchini Niger.
IOM
Wahamiaji wakisajiliwa katika Kituo cha Usafiri cha Agadez nchini Niger.


Imeongeza kuwa, Niger vile vile barani Afrika ilisalia kuwa nchi mwenyeji kwa wahamiaji wengi ikiwa na jumla ya wahamiaji 10,573 ambao walisaidia kurejea makwao, na hivyo kudokeza kuwa mwendelezo wa mwenendo wa kurejea kutoka kituo cha mpito kwenda maeneo mengine nje ya eneo la kiuchumi la Ulaya.

“Ripoti hii ya IOM inaonesha uwezo wetu wa kukidhi ongezeko la mahitaji ya wahamiaji na kurejea nyumbani kwa utu pamoja na kusaidia shughuli au miradi ya kujumuika tena kwenye jamii zao kufuatia kuondolewa kwa vikwazo vingi vya safari vilivyowekwa wakati wa janga la COVID-19,” amesema Yitna Getachew, Mkuu wa Kitengo cha ulinzi cha IOM.

IOM inasema miradi ya kujumuisha tena wahamiaji kwenye jamii zao ni muhimu sana katika mipango ya kusaidia mhamiaji kurejea nyumbani kwa hiari kwa kuwa inawapatia fursa wahamiaji na pia maendelelo endelevu kwenye jamii zao.

Miradi hiyo ni ya ngazi ya mtu binafsi, jamii ya kujenga mifumo.

Kwa ujumla, nchi tatu ambazo zinahifadhi wahamiaji na pia wahamiaji wanatoka ambako kulifanyika miradi ya usaidizi ni Ujerumani asilimia 15, Niger asilimia 12 na Guinea asilimia 8.
Misaada hiyo ni pamoja na ya kijamii, kiuchumi na ushauri nasihi wakati mhamiaji anajumuishwa tena kwenye jamii.