Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kusini mwa jangwa la Sahara kunufaika na mradi wa FAO wa ramani ya virutubisho vya udongo

Wakulima wakiwa kazini nchini Guatemala
© FAO
Wakulima wakiwa kazini nchini Guatemala

Kusini mwa jangwa la Sahara kunufaika na mradi wa FAO wa ramani ya virutubisho vya udongo

Ukuaji wa Kiuchumi

Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO limetangaza kuanza haraka utekelezaji wa mradi wa kuchora ramani za kidigitali za mahitaji ya virutubisho vya udongo katika nchi za Kusini mwa jangwa la Sahara na Amerika ya Kati baada ya kupokea mchango wa dola milioni 20 kutoka Serikali ya Marekani. 

Taarifa hii imetangazwa leo na shirika hilo kutoka Roma nchini Italia ambapo wameeleza kuwa ucharaji wa ramani hizo itasaidia kuboresha ufanisi katika matumizi ya mbolea na kusaidia kuimarisha usalama wa chakula na lishe. 

Mkurugenzi Mkuu wa FAO Qu Dongyu ameishukuru serikali ya Marekani na kusema mradi huu ni muhimu kwakuwa utawasaidia kufahamu ni virutubisho gani udongo na mazao yanahitaji  na hii itapunguza uharibifu wakati wa kuweka mbolea na kuongeza ufanisi wake.

“Mchango huu umekuwa wakati muafaka na unatuwezesha kuongeza matumizi ya ramani ya udongo katiak kanda ambazo zina uhitaji zaidi na ambako tumeshuhudia kupungua kwa matumizi ya mbolea kutokana na kupanda kwa bei” ameeleza Dongyu.

Mchango huo wa Marekani ulitangazwa wakati wa ziara ya wiki moja katika nchi za Guatemala na Honduras iliyofanywa na Balozi Cindy McCain ambaye ni Mwakilishi wa kudumu wa Marekani katika FAO na Mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyoko Roma Italia.

Balozi McCain alisema fedha hizo walizozitoa zitasaidia kukabiliana na mzozo wa chakula duniani usio na kifani na kushughulikia mahitaji ya haraka na yale ya muda mrefu ambayo mataifa mengi yanakabiliwa nayo kutokana na kupanda kwa bei za vyakula na mbolea, athari za mabadiliko ya tabianchi, ukame wa mara kwa mara, mafuriko, joto la juu pia na kukosekana kwa uhakika wa lishe.

“Tumeamua kufadhili mradi huu kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara na Amerika ya kati kwakuwa tunaamini utakuwa na matokeo chanya ya haraka na yatakayoleta mabadiliko ya mazao endelevu. Kusimamia udongo kwa njia endelevu ni kuongeza ustahimilivu na kukabiliana na mabadiliyo haya na nimuhimu na lazima tuelekee kwenye maamuzi sahihi na ufuatiliaji endelevu wa afya ya udongo.”

Taarifa hii imetolewa katika wiki ambayo FAO na washirika wa masuala ya udongo duniani wanakutana kwenye kongamano la siku nne kwa njia ya mtandao ambapo wanajadili kuhusu rutuba ya udongo kimataifa na njia za kuimarisha upatikanaji wa virutubisho vya udongo kwa mazao bila kuharibu mazingira.

Wanawake huko Rio Negrp wakiandaa ardhi kwa ajili ya kilimo
UNHCR/Diego Moreno
Wanawake huko Rio Negrp wakiandaa ardhi kwa ajili ya kilimo

Mradi wa Majaribio

Mradi huu umefashanikiwa katika majaribio yaliyofanyika nchini Ethiopia kwa wakulima wadogo ambao ni takriban asilimia 40 ya wachangiaji wa ukuaji wa uchumi na umekuwa na matokeo chanja. 

Kupitia mradi huo FAO walikuwa wakitumia teknolojia ya uchoraji wa kidigitali ya uchoraji wa udongo na kisha teknolojia hiyo inatoa taarifa kwa wakati kuhusu vitu mbalimbali mfano uboreshaji wa mbolea katika udongo.

Matokeo yaliyopatikana na ni ongezeko la mavuno na upatikanaji wa nafaka za ubora wa juu nchini humo.  

FAO inasaidia katika ukuzaji wa utengenezaji wa takwimu za kitaifa za udongo na mifumo ya taarifa za udongo kama bidhaa ya umma ambayo itatumiwa na watunga sera, sekta binafsi na zaidi wakulima ili waweze kuzitumia taarifa hizo na kuzalisha kwa manufaa kwa muda mrefu pamoja na kuboresha muitikio ndani ya kipindi kifupu ili kukabiliana na mwenendo wa soko la mbolea na mabadiliko ya hali ya tabianchi bila kuathiri watakacho zalisha.

Mwanachama wa kikundi cha kinamama akiandaa udongo kwa ajili ya kilimo
UNHCR/Diego Moreno
Mwanachama wa kikundi cha kinamama akiandaa udongo kwa ajili ya kilimo

Miaka zaidi ya 60 ya kupima udongo

FAO ina uzoefu wa kuchora ramani za udongo kwa zaidi ya miaka 60 ambapo kwa mara ya kwanza mradi ulianza mwaka 1961 kwa ushirikiano wa FAO na UNESCO na wamekuwa wakiendelea na tangu kipindi hicho huku wakiboresha juhudi na kutumia teknolojia mpya pamoja na kujifunza kwakutumia teknolojia zinazoendeshwa na mashine ambapo kumewawesha kuzidi kupata usahakiki wa taarifa ambazo zimekuwa zikitumiwa na watunga será, wawekezaji na wadau wengine wa kilimo ikiwemo wazalishaji wa mbolea. 

Mpaka sasa ushirikiano wa kimataifa wa masuala ya udongo umewafikia zaidi ya wataalamu 500 katika ngazi ya kitaifa kwenye mataifa 52 ya Amerika ya Kati na Kusini mwa Jangwa la Sahara pamoja na kuwaunga mkono kwenye uzalishaji wa kazidata zinazozingatia vitu vinavyotishia zaidi ubora wau gongo, uwezekano wa rasilimali za udongo ili kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi  na kukabiliana na uhaba wa chakula. 
Kufahamu zaidi kuhusu ramani za udongo duniani bofya hapa