Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS yalaani shambulio katika kaunti ya Mayom nchini Sudan Kusini

Wafanyakazi wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) wawasili Kaunti ya Mayom, Jimbo la Umoja, ili kuwahamisha raia waliojeruhiwa.
Picha ya Umoja wa Mataifa/Isaac Billy
Wafanyakazi wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) wawasili Kaunti ya Mayom, Jimbo la Umoja, ili kuwahamisha raia waliojeruhiwa.

UNMISS yalaani shambulio katika kaunti ya Mayom nchini Sudan Kusini

Amani na Usalama

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini, UNMISS, umelaani shambulizi lililotokea Julai 22 mwaka huu 2022 katika Kaunti ya Mayom, iliyoko katika jimbo la Umoja nchini humo na kusababisha vifo vya watu kadhaa akiwemo Kamishna wa Kaunti hiyo ya Mayom.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu nchini humo Nicholas Haysom akiwa Juba imesema kikundi cha waasi cha Sudan Kusini People’s Movement wakiongozwa na Jenerali Stephen Buay Rolnyang wamedai kuhusika na shambulio hilo, kufuatia mapigano ya awali kati ya kundi hilo na vikosi vya serikali katika eneo hilo tarehe 19 Julai mwaka huu 2022. 

"Vurugu ambazo zinatokea katika maeneo haya ya nchi tayari zimekuwa na athari mbaya kwa jamii. Tunatoa wito kwa makundi yote yenye silaha kuweka chini silaha zao na kushiriki katika juhudi za kusaka  amani. Hii ndiyo njia pekee ya kuvunja mzunguko wa ghasia na mauaji ya kulipiza kisasi, na kufungua njia ya amani ya kudumu na endelevu,” amesema Haysom.

UNMISS imeeleza kuendelea kufuatilia kwa karibu hali katika Kaunti ya Mayom na inaunga mkono mchakato wa kusaka amani.