Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO yasema uhamasishaji wa kimataifa ni muhimu ili kulinda mikoko duniani

Mikoko katika Ziwa Sentarum huko Kalimantan Magharibi, Indonesia.
CIFOR/Yayan Indriatmoko
Mikoko katika Ziwa Sentarum huko Kalimantan Magharibi, Indonesia.

UNESCO yasema uhamasishaji wa kimataifa ni muhimu ili kulinda mikoko duniani

Tabianchi na mazingira

Muda unayoyoma wa kulinda mikoko duniani ambayo sio tu makazi ya viumbe wengi lakini pia ni muhimu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi, amesema Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Audrey Azoulay, hii leo.

Audrey Azoulay, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, alitoa wito wa uhamasishaji wa kimataifa kuhusu maeneo haya muhimu ya pwani katika ujumbe wake wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Uhifadhi wa ikolojia ya Mikoko duniani.
“Inakadiriwa kuwa zaidi ya robo tatu ya mikoko duniani sasa inatishiwa kupotea pamoja na mambo yote mizuri yanayoitegemea” alisema.

Tweet URL

Mradi wa Mikoko katika nchi Saba

Azoulay alitangaza kuwa mwezi ujao wa Agost, UNESCO itazindua mradi mpya wa kurejesha mikoko katika nchi saba za Amerika ya Kusini ambazo ni  Colombia, Cuba, Ecuador, El Salvador, Mexico, Panama, na Peru.
Mradi huo utaleta fursa za kiuchumi kwa jamii za wenyeji. Pia itawezesha ubadilishanaji na kushirikishana maarifa kati ya wanajamii, watu wa asili na jumuiya ya wanasayansi.

“Zaidi ya ulinzi na urejeshaji wa mikoko, tunahitaji ufahamu wa kimataifa. Hili linahitaji kuelimisha na kutahadharisha umma, sio tu shuleni, lakini popote inapowezekana,” alisema.

Dhamira hii inaonyeshwa katika maonyesho ya UNESCO yaliyoundwa kwa ajili ya Makumbusho ya Kitaifa ya Sayansi ya Thailand, ambayo sasa yanatembezwa duniani kote, “kwa sababu pia ni maonesho na maelezo ya siri za mikoko ambazo tutaweza kuzihifadhi kwa uendelevu,” aliongeza.

Uzuri na mazingira magumu

Azoulay aliangazia lengo la Siku ya Kimataifa, wakati kila mtu anahimizwa kufahamu thamani, uzuri na hatari ya mazingira ya mikoko, na kujitolea kuilinda.

“Kutoka kwenye mizizi iliyoshikamana hadi ncha za matawi, katika makazi tata, aina nyingi huja kulisha na kuzaliana, na kuunda kwapamoja mfumo wa ikolojia unaostawi zaidi kuwako. Na sisi binadamu tunategemea mazingira haya ambayo yanapunguza kasi ya mmomonyoko wa pwani na ni chanzo cha chakula kwa wengi,” alisema.

Mkuu huyo wa utamaduni wa Umoja wa Mataifa pia alimtaja mshairi wa Colombia, Tomás González, ambaye ametengeneza mikoko kuwa alama ya moja ya vitabu vyake.

Azoulay alinukuu kutoka katika mkusanyiko wake wa mashairi yake ya Manglares, neno la Kihispania likimaanisha "mikoko", ambalo linatoa wito wa kurejea kwa umoja kwenye umuhimu wa asili:

“Ili miti itokee kwanza na kisha kuweka ukungu na kuunganishwa na hewa, mandhari ya nyuma, tambarare za matope; ili maporomoko yaingie baharini papo hapo iliyonyunyizwa na chumvi, jua, mwangaza na ili bahari iangaze kwanza na kisha kuungana tena na nchi kavu”.

UNESCO inafanya kazi kulinda mikoko duniani, na “mifumo mingine ya kaboni ya bluu”, kupitia mipango kama vile Geoparks, maeneo ya Urithi wa Dunia, na hifadhi za Biosphere. Lakini Azoulay alionya kuwa saa inayoyoma.
“Katika hali ya dharura ya mabadiliko ya tabianchi, hata hivyo, muda unasonga na lazima twende mbali zaidi, kwa sababu mikoko pia ni mifereji ya kaboni ambayo hatuwezi kumudu kupoteza,” alisema.