Ulichovaa hakipaswi kuwa kichocheo cha ukatili wa kingono- Manusura wa ukatili wa kingono

Manusura watano wa ukatili wa kingono wamejiweka hadharani wakati wa maonesho yaliyofanyika kwenye makao makuu ya UN, New York, yakiwapatiwa jina, "Ulikuwa umevaa nini?"
Spotlight Initiave
Manusura watano wa ukatili wa kingono wamejiweka hadharani wakati wa maonesho yaliyofanyika kwenye makao makuu ya UN, New York, yakiwapatiwa jina, "Ulikuwa umevaa nini?"

Ulichovaa hakipaswi kuwa kichocheo cha ukatili wa kingono- Manusura wa ukatili wa kingono

Haki za binadamu

Hebu fikiria machungu yasiyokwisha ya shambulio la kutisha la ukatili wa kingono. Na wakati umefika polisi ukiwa na mikwaruzo mwilini na huku unatetemeka unawaeleza kilichokufika cha kustaajabisha, wao wanakugeuka na kukuuliza: ulikuwa umevaa nini?

 “Gauni la rangi ya buluu, soksi ndefu na mabuti,” ndivyo asimuliavyo Jessica Longo, manusura wa ukatili wa kingono ambaye kwa miaka sita sasa amekuwa akiendesha kampeni kuhusu haki ya manusura wa ukatili wa kingono. “Hicho ndio nilikuwa nimevalia usiku ule ambao niliburuzwa. Nilibakwa na kisha nikaachwa peke yangu nife.” 

Nguo 103 zawakilisha manusura bilioni 1.3 wa ukatili wa kingono

Jessica ni miongoni mwa manusura 103 wa ukatili wa kingono ambaye alikuwa anatoa kauli hiyo mbele ya hadhira iliyoshiriki uzinduzi wa kazi ya sanaa inayoonesha mavazi yaliyokuwa yamevaliwa na manusura wa ukatili wa kingono, kazi hiyo ya sanaa ikibeba jina, Ulikuwa umevaa nini? 
 
Swali hilo na mengine mengi ya kushambulia huwa mara kwa mara yanawapatia kiwewe manusura au waathirika wa ukatili wa kingono duniani kote – wakilaumiwa wao kwa uhalifu waliotendewa.

Mimi ni miongoni mwa waliobakwa- Amanda

Amanda Nguyeni kutoka RISE ambalo ni shirika la kiraia la hapa Marekani la kutetea haki za raia anasema ,”mwaka jana tulianzisha kazi ya sanaa iitwayo Ulikuwa umevaa nini? Midoli hiyo mitano imevalishwa nguo ambazo manusura walikuwa wamevalia wakati wanabakwa. Mimi ni miongoni mwao.” 

Manusura wa ukatili wa kingono Kadijatu Grace akisimulia kwa uchungu yaliyomfika wakati wa hafla ya uzinduzi wa maonesho ya "Ulikuwa umevaa nini?" kwenye makao makuu ya UN, New York, Marekani
Spotlight Iniative
Manusura wa ukatili wa kingono Kadijatu Grace akisimulia kwa uchungu yaliyomfika wakati wa hafla ya uzinduzi wa maonesho ya "Ulikuwa umevaa nini?" kwenye makao makuu ya UN, New York, Marekani

Maonesho haya yana jumla ya nguo 103 zikiwakilisha jumla ya manusura bilioni 1.3 duniani kote ambao walibakwa.  

Ukatili wa kingono ni suala la dunia nzima na linahitaji kutambuliwa kimataifa. Shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani, WHO linasema asilimia 35 ya wanawake duniani au zaidi ya theluthi moja ya wakazi wa dunia ni manusura wa ukatili wa kingono. 

Uko hoi na polisi wanakuuliza ulikuwa umevaa nini?

Jessica anarejea akisema,  “Ulikuwa umevaa nini? Je ulikuwa unakunywa pombe au ulikuwa unacheza dansi? Je ulikuwa unatabasamu kupindukia ? haya ni maswali ambayo polisi waliniuliza kabla ya kuniambia, ‘ pole sana kwa yaliyokusibu, lakini hakuna ambacho tunaweza kufanya. » 
 
Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Abdullah Shahidi alituma ujumbe wake kwa njia ya video akisema, «maonesho haya yanapaswa kuwa kichocheo cha mjadala muhimu kuhusu wajibu wetu wa pamoja wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa kike. » 
 
Manusura mwingine Samantha McCoy anasem kile alichokuwa amevaa hakipaswi kuwa hoja. Kule anakoishi nako hakupaswi pia kubadilisha iwapo alipata huduma bora.” 

Kilichonipata siwezi kubadili lakini natetea wengine

Kwa manusura mwingine Britney Lane yaliyomkumba yeye hawezi kubadilisha lakini kuna hatua anaweza kuchukua.

Britnery anasema, “siwezi kubadili kile kilichonikumba usiku ule, lakini naweza kufanya kazi kubadili mfumo kuhakikisha kuwa hakuna tena mtu mwingine anatumbukia kwenye janga hilo.” 
 
Spotlight Initiative ni ubia kati ya Umoja wa Mataifa na Muungano wa Ulaya wenye lengo la kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake ifikapo mwaka 2030. 

Baadhi ya nguo ambazo ziko kwenye maonesho "ulikuwa umevaa nini?"Waliokuwa wamevalia mavazi haya ni manusura wa ubakaji.
UN News/Elizabeth Scaffidi
Baadhi ya nguo ambazo ziko kwenye maonesho "ulikuwa umevaa nini?"Waliokuwa wamevalia mavazi haya ni manusura wa ubakaji.

Kadijatu Grace manusura mwingine akiwa kwenye mimbari ya maonesho ya kazi hii ya Sanaa akafunguka akisema, “mlidhani mmenisambaratisha! La hasha! Mmenipatia jukwaa. Katu sitoacha kuimba. Na katu sitoacha kuelezea watu simulizi yangu.” 
 
Na ndipo Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed akaeleza washiriki wa tukio hili lililoandaliwa kwa pamoja na Spotlight Initiative na RISE. 

Naibu Katibu Mkuu anasema, “mmetuhamasisha sote kuzungumza dhidi ya ukatili wa kijinsia na uongozi wenu utaisaidia wengine kupata ujasiri wa kuhoji mifumo inayonyamazisha manusura.” 

Paris Hilton naye asimulia masahibu yake 

Ama hakika sasa sauti zinapazwa na miongoni mwa sauti hizo ni ya Paris Hilton, mmoja wa vijana wa kike wenye ushawishi duniani.

Paris anasema alipokuwa ana umri wa miaka 16 aliamshwa na wanaume wawili wakiwa na pingu ambao walimsafirisha hadi jimbo jingine kwenye jengo la tiba kwa waraibu wa madawa ya kulevya.

Amesema kwa miaka miwili wafanyakazi wa kituo hicho “walinipatia kipigo cha mwili, ukatili wa kingono na kisaikolojia. Nilijiona sina uwezo kabisa. Niko hap aleo kwa sababu ukatili huu bado unaendelea.” 
 
Amanda, kutoka Rise anatamatisha video yao akisema, “hii ndio simulizi yetu.  Ni simulizi ya pamoja ya maendeleo. Na ina maana kwamba hakuna asiye na nguvu au uthabiti pindi tunaposhirikiana. Na hakuna ambaye hatoonekana pindi tutakapodai tuonekane.”