Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ndui ya nyani au Monkeypox ni nini na inaeneaje? Kila unachopaswa kufahamu kiko hapa. 

Wataalamu wa wanyama wanachunguza nyani ambaye alikuwa mojawapo ya vyanzo vinavyoshukiwa vya maambukizi ya magonjwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa wanadamu  katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuanzia 1996 hadi 1997.
© CDC
Wataalamu wa wanyama wanachunguza nyani ambaye alikuwa mojawapo ya vyanzo vinavyoshukiwa vya maambukizi ya magonjwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa wanadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuanzia 1996 hadi 1997.

Ndui ya nyani au Monkeypox ni nini na inaeneaje? Kila unachopaswa kufahamu kiko hapa. 

Afya

Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na maneno mengi kuhusu ugonjwa ambao si mgeni, lakini ambao ulikuwa haujasikika sana, hasa kwa vile ulikuwa umeenea katika nchi chache za bara la Afrika na sasa mlipuko umeonekana katika maeneo mbalimbali duniani. Hii ni monkeypox, ndui ya nyani kwa lugha ya Kiswahili. 

Ingawa hatari kwa umma ni ndogo, ni muhimu kuujua vizuri ugonjwa huu ili kukabiliana nao. Shukrani kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO, hapa tunajibu maswali yote uliyo nayo kuhusu ugonjwa huu na ni hatua gani unaweza kuchukua ili kujilinda. 

Ndui ya nyani ni nini? 

Ni ugonjwa unaosababishwa na virusi, vinavyojulika kama monkeypox. Ni ugonjwa wa virusi vinavyotoka kwa wanyama hadi kwa wanadamu, kitaalamu Zoonotic au Zoonosis. Ugonjwa huu pia unaweza kuenea kutoka kwa mtu hadi mtu. Ugonjwa huu umepewa jina hilo kwa sababu uligunduliwa katika nyani kadhaa wa maabara mwaka wa 1958. Hata hivyo, wengi wa wanyama wanaoweza kuambukizwa na kisha kuambukiza watu ni panya, kama vile panya wakubwa wa Gambia, panya wadogo na wanyama wengine wa nyikani wafahamikao kama prairie dogs. 

Ugonjwa huu wa ndui ya nyani unapatikana wapi zaidi 

Ndui ya nyani/Monkeypox hupatikana kwa wingi katika misitu ya mvua ya Afrika ya kati na magharibi, ambapo wanyama wanaoweza kubeba virusi hivyo huishi, na ni ugonjwa wa kawaida unaokuwa katika eneo fulani. Wakati fulani, Ndui ya nyani inaweza pia kupatikana kwa watu walio nje ya maeneo hayo ya Kiafrika ambao wanaweza kuwa wameambukizwa baada ya kuyatembelea maeneo hayo.   

Dalili za Ndui ya nyani ni zipi? 

Dalili za ugonjwa wa Ndui ya nyani ni kwa kawaida hujumuisha homa, maumivu makali ya kichwa, maumivu ya misuli, maumivu ya mgongo, nguvu kidogo, kuvimba mitokin, na vipele au vidonda kwenye ngozi. 

Kwa mtu aliyeambukizwa Ndui ya nyani, kawaida upele huanza siku ya kwanza au ya tatu ya kuanza kwa homa. Vidonda vinaweza kuwa tambarare au vilivyoinuka kidogo, vikijazwa na umajimaji usio na rangi wakati mwingine wenye umanjano, kisha kuganda juu, kukauka na kuanguka. Idadi ya majeraha au makovu kwa mtu inatofautiana kutoka kwa machache hadi elfu kadhaa. Upele huwa unaonekana kwenye uso, viganja vya mikono, na nyayo za miguu. Upele unaweza pia kupatikana katika kinywa, sehemu za siri, na macho. 

Kawaida dalili huchukua wiki mbili hadi nne na huondoka zenyewe bila matibabu. Ikiwa unafikiri dalili zako zinaweza kuwa zinazohusiana na Ndui ya nyani, wasiliana na daktari wako au kituo cha afya mara moja. Ikiwa umewasiliana kwa karibu na mtu ambaye ana dalili hizi au unashuku kuwa kuna uwezekano wa kuambukizwa, mjulishe daktari wako. 

Vidonda vya Monkeypox mara nyingi huonekana kwenye mikono ya mikono.
© CDC
Vidonda vya Monkeypox mara nyingi huonekana kwenye mikono ya mikono.

Je, watu wanaweza kufa kutokana na Ndui ya nyani? 

Katika hali nyingi, dalili za ugonjwa wa ndui huondoka zenyewe ndani ya wiki chache, lakini kwa watu wengine, inaweza kusababisha matatizo ya kiafya na hata kifo. Watoto wachanga, watoto na watu walio na upungufu wa kinga wanaweza kuwa katika hatari ya kupata dalili kali zaidi na kifo kutokana na ugonjwa huo. 

Matatizo ya maambukizi makali ni pamoja na maambukizi ya ngozi, nimonia, kuchanganyikiwa, na maambukizi ya macho ambayo yanaweza kusababisha kupoteza uoni. Kati ya asilimia 3 na asilimia 6 ya maambukizi yaliyotambuliwa katika maeneo ambako Ndui ya nyani ni kawaida,  yamesababisha vifo. Wengi wa kesi hizi ni watoto au watu ambao wanaweza kuwa na hali nyingine za afya. Kumbuka kuwa takwimu hizi zinaweza kuwa za kukadiria kupita kiasi kwa sababu uhesabuji wa maambukizi katika nchi zilizo na ugonjwa ni ndogo. 

Ndui ya nyani/Monkeypox huambukizwaje kutoka kwa wanyama hadi kwa wanadamu? 

Hali hii inaweza kuenea kwa watu wanapogusana kimwili na mnyama aliyeambukizwa. Wanyama walio na virusi hivi wanaweza kujumuisha panya au nyani. Hatari ya kuambukizwa ugonjwa huo kutoka kwa wanyama inaweza kupunguzwa kwa kuepuka kugusana bila kinga na wanyama pori, hasa wale ambao ni wagonjwa au waliokufa (ikiwa ni pamoja na kugusa nyama na damu zao). Ni muhimu kusisitiza kwamba chakula chochote kilicho na nyama au sehemu za wanyama kinapaswa kupikwa, hasa katika nchi ambazo ugonjwa wa Ndui ya nyani ni kawaida.

Je, Ndui ya nyani huenezwaje kutoka kwa mtu hadi mtu? 

Watu walio na ugonjwa huu huambukiza huku wakiwa na dalili (kwa kawaida ndani ya wiki mbili hadi nne za kwanza). Unaweza kupata hali hii kwa kugusana kimwili na mtu ambaye ana dalili kama vipele, maji maji ya mwili (kama vile maji maji, usaha, au damu kutoka kwenye vidonda vya ngozi), na upele. Kugusa vitu ambavyo vimegusana na mtu aliyeambukizwa kama vile nguo, matandiko, taulo au vitu kama vile vyombo vya kulia vinaweza pia kuwa chanzo cha maambukizi. 

Vidonda vya namna mbalimbali mathalani vya mdomoni pia vinaweza kuambukiza kwa vile virusi vinaweza kuenea kwa njia ya mate. Kwa hiyo, tutakuwa na hatari kubwa ya kuambukizwa ikiwa tunaishi na watu walioambukizwa katika makazi yetu au ikiwa tutafanya hivyo na washirika wetu wa ngono. Pia watu wanaofanya kazi katika sekta ya afya wanawekwa wazi zaidi katika mazingira ya kuambukizwa. 

Virusi pia vinaweza kuambukiza kutoka kwa mwanamke mjamzito hadi kwa mtoto mchanga tumboni kupitia kupitia plasenta au mfuko wa uzazi, au kwa kugusana kwa mzazi aliyeambukizwa na mtoto wakati au baada ya kujifungua kwa njia ya ngozi hadi ngozi. 

Hata hivyo bado haijulikani wazi ikiwa watu ambao hawana dalili za Ndui ya nyani wanaweza kusambaza ugonjwa huo. 

Nani yuko hatarini kuambukizwa Ndui ya nyani au Monkeypox? 

Mtu yeyote anayegusana kimwili na mtu aliye na dalili au mnyama aliyeambukizwa, yuko kwenye hatari kubwa ya kuambukizwa ugonjwa wa Ndui ya nyani. Watu ambao wamechanjwa dhidi ya ndui wana uwezekano wa kuwa na kinga fulani dhidi ya maambukizi. Mnamo mwaka 1980, ugonjwa wa ndui ulikuwa ugonjwa wa kwanza kwa wanadamu kutokomezwa, kwa hivyo chanjo dhidi ya ugonjwa huu ilisimamishwa. Kwa hiyo, vijana wana uwezekano mkubwa wa kuupata ugonjwa wa Ndui ya nyani. Hata hivyo, watu ambao wamechanjwa dhidi ya ndui wanapaswa pia kuchukua tahadhari ili kujikinga na kuwalinda wengine. 

Dalili kali zaidi na za kutishia maisha zinaweza kuonekana kwa watoto wachanga, watoto, na watu walio na upungufu wa kinga ya mwili. Wahudumu wa afya pia wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa kutokana na muda wao mwingi kuwa katika mazingira ya virusi.  

Ninawezaje kujilinda mwenyewe na wengine? 

Unaweza kupunguza hatari ya kuambukizwa kwa kupunguza kukutana na watu wanaoshuku kuwa wana ugonjwa huo au ni ikiwa wana maambukizi yaliyothibitishwa. 

Iwapo unahitaji kugusana kimwili na mtu aliye na hali hii kwa sababu ni mfanyakazi wa afya au mnaishi pamoja, mhamasishe mtu aliyeambukizwa ajitenge na kufunika michubuko yoyote ya ngozi kama anaweza (kwa mfano, kwa kuvaa nguo juu ya upele). Utahitaji kuvaa barakoa ya matibabu unapokuwa karibu nao kimwili, hasa ikiwa wanakohoa au wana vidonda mdomoni. Epuka kugusana ngozi kwa ngozi na ikiwa una mgusano wowote wa moja kwa moja vaa glavu zinazoweza kutupwa baada ya kutumika. Vaa barakoa ikiwa ni lazima uguse nguo au kitanda cha mtu aliyeambukizwa. 

Nawa mikono yako mara kwa mara kwa sabuni na maji au tumia kitakasa mikono chenye pombe, hasa baada ya kugusana na mtu aliyeambukizwa, au mavazi yake (pamoja na shuka na taulo) au vitu vingine au nyuso ambazo umegusa au kugusa ambayo inaweza kugusana na upele wako au vifaa vingine kama  vyombo au sahani. 

Fua nguo, taulo, shuka, na vyombo vya chakula vya mtu aliyeambukizwa kwa maji ya joto na sabuni. Safisha iapasavyo na kuua vijidudu kwenye nyuso zozote zilizochafuliwa na tupa taka zilizochafuliwa (kama vile mavazi). 

Watoto wanaweza kuambukizwa Ndui ya nyani? 

Watoto wanaweza kuupata na mara nyingi wana uwezekano mkubwa wa kuwa na dalili kali kuliko vijana na watu wazima. Virusi pia vinaweza kuambukiza kutoka kwa mwanamke hadi kwa kijusi chake (mtoto aliyeko tumboni) au mtoto mchanga wakati wa kuzaliwa au kupitia mgusano wa mwili. 

Nifanye nini ikiwa ninashuku nimeambukizwa? 

Wasiliana na daktari wako mara moja kwa ushauri, upimaji na huduma ya matibabu ikiwa unadhani una dalili au umekutana na mtu aliyeambukizwa. Ikiwezekana, jitenge na epuka mawasiliano ya karibu na watu wengine. Nawa mikono yako mara kwa mara na ufuate hatua zilizoorodheshwa hapo juu ili kuwalinda wengine dhidi ya maambukizi. Mhudumu wako wa afya atachukua sampuli kwa ajili ya kupima ili uweze kupata huduma sahihi. 

Kuna chanjo dhidi ya Ndui ya nyani? 

Kuna chanjo kadhaa zinazopatikana za kuzuia ugonjwa wa ndui ambazo pia hutoa kinga fulani. Chanjo ya ndui (MVA-BN, pia inajulikana kama Imvamune, Imvanex, au Jynneos) ilitengenezwa katika miaka ya hivi karibuni na kuidhinishwa mwaka 2019 kwa ajili ya matumizi ya kuzuia Ndui ya nyani na bado haijapatikana kwa wingi. WHO inashirikiana na mtengenezaji wa chanjo hiyo ili kuboresha upatikianaji wake. Watu ambao wamechanjwa dhidi ya ndui hapo awali pia watakuwa na kinga fulani. 

Kuna tiba yoyote ya Ndui ya nyani? 

Dalili mara nyingi huondoka zenyewe bila hitaji la matibabu. Ni muhimu kuufuatilia upele kwa kuuacha uwe mkavu iwezekanavyo au kuufunika kwa bandeji yenye unyevu ikiwa ni lazima ili kulinda eneo hilo. Epuka kugusa vidonda mdomoni au machoni mwako. Visafisha kinywa na dawa za macho zile za matone zinaweza kutumika mradi tu bidhaa zenye cortisone ziepukwe. Katika hali mbaya, vaccinia immunoglobulin (VIG), dawa ya kuzuia virusi ambayo ilitengenezwa kutibu ndui (tecovirimat, iliyouzwa kama TPOXX) ambayo pia iliidhinishwa kwa ajili ya matibabu ya Ndui ya nyani mnamo Januari mwaka 2022, inaweza kupendekezwa. 

Ni wapi ulimwenguni kuna hatari kubwa kwa sasa? 

Tangu mwaka 1970, maambukizi kwa binadamu ya ugonjwa wa Ndui ya nyani yameoatikana katika nchi 11 za Afrika: Benin, Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Gabon, Côte d'Ivoire, Liberia, Nigeria, Jamhuri ya Congo, Sierra Leone, na Sudan Kusini. 

Maambukizi yanayotokea mara kwa mara katika nchi zisizo na ugonjwa wa Ndui ya Nyani ni kutoka kwa watu walioambukizwa walipofasiri kwenda nchi zenye ugonjwa. Mlipuko mmoja ulisababishwa na kukutana na wanyama walioletwa kutoka nje ya nchi.   

Hivi sasa, milipuko ya ugonjwa wa Ndui ya nyani inatokea katika nchi kadhaa za Ulaya, Amerika, Afrika, Pasifiki ya Magharibi na nchi za Mashariki ya Mediterania ambapo virusi vya monkeypox au Ndui ya nyani  havijawahi kugunduliwa hapo awali. Mwaka huu 2022, idadi kubwa zaidi ya kawaida ya maambukizi inaripotiwa katika sehemu za Afrika ambazo ziliwahi kutangaza maambukizi hapo awali, zikiwemo Nigeria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Jamhuri ya Afrika ya Kati. WHO inafanya kazi na nchi zote zilizoathiriwa ili kuimarisha ufuatiliaji na kutoa mwongozo wa jinsi ya kukomesha maambukizi na jinsi ya kuhudumia wagonjwa. 

Nchi kadhaa za Kiafrika zilikuwa zimeripoti maambukizi ya ndui ya nyani katika miaka iliyotangulia kabla ya mlipuko wa sasa. Nchi hizo ni pamoja na Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Congo, Côte d'Ivoire, Gabon, Liberia, Nigeria na Sierra Leone. Baadhi ya nchi hizi zina maambukizi machache tu, wakati zingine zimeendelea au zimekuwa na milipuko ya mara kwa mara. Maambukizi ya mara kwa mara katika nchi zingine yamehusishwa na historia ya kusafiri kwenda Nigeria. Mlipuko wa sasa unaoathiri nchi nyingi kwa wakati mmoja sio mlipuko wa kawaida kama milipuko ya siku za nyuma. 

Nchi zilizothibitishwa na WHO kuwa na maambukizi ya Ndui ya nyani  kuanzia 1 Januari 2022 hadi 22 Juni 2022 

Asilimia 86 Ulaya, asilimia 2 Afrika 

Idadi kubwa ya maambuki yaliyothibitishwa katika maabara (2933/3413; 86%) yameripotiwa kutoka Kanda ya WHO Ulaya. Maeneo mengine nayo yaliyoripoti maambukizi ni pamoja na: Kanda ya Afrika (73/3413, 2%), 

Orodha nzima iko hapa

Je! tunajua nini kuhusu mlipuko uliotambuliwa katika nchi kadhaa mnamo Mei 2022? 

Nchi kadhaa ambapo aina hii ya ndui si ya kawaida ziliripoti maambuki mnamo Mei 2022. Kufikia Mei 19, 2022, visa viliripotiwa katika zaidi ya nchi 10 katika maeneo yasiyo ya kawaida kwa ugonjwa huo. Maambukizi ya ziada yanachunguzwa. Kwa taarifa za mara kwa mara za hivi punde kuhusu Ndui ya nyani, bonyeza hapa

Isipokuwa baadhi ya matukio yaliyogunduliwa kwa wasafiri waliotembelea nchi zilizo na ugonjwa huo, matukio katika maeneo yasiyo ya kawaida ambayo hayahusiani na kusafiri kutoka nchi za ugonjwa si ya kawaida. Hivi sasa (kuanzia Mei 2022), hakuna uhusiano wa wazi kati ya maambukizi na kusafiri kutoka nchi zenye ugonjwa na hakuna uhusiano na wanyama walioambukizwa. 

Tunaelewa kuwa mlipuko huu unawahusu wengi, hasa watu ambao wapendwa wao wameathiriwa. Jambo la msingi kwa wakati huu ni kwamba tunaongeza ufahamu wa Ndui ya nyani kati ya watu ambao wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa na kutoa ushauri wa jinsi ya kuzuia kuenea zaidi kati ya watu. Kadhalika, ni muhimu kwa wafanyakazi wa afya ya umma kuwa na uwezo wa kutambua na kuhudumia wagonjwa. Ni muhimu kuelewa kwamba hakuna mtu aliyeathiriwa na virusi anapaswa kunyanyapaliwa. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni, WHO linafanya kazi kusaidia nchi wanachama katik shughuli za ufuatiliaji wa mlipuko, maandalizi na majibu katika nchi zilizoathiriwa. 

Uchunguzi pia unaendelea katika nchi zilizoathiriwa ili kubaini chanzo cha maambukizi kwa kila tukio liliyotambuliwa na kutoa huduma ya matibabu na kuzuia kuenea zaidi. 

Je, kuna hatari kwamba mlipuko wa sasa wa Ndui ya nyani utageuka kuwa mlipuko mkubwa zaidi? 

Ndui ya nyani kwa ujumla haichukuliwi kuwa ya kuambukiza sana kwa sababu inahitaji mguso wa karibu wa kimwili na mtu anayeambukiza (kwa mfano, ngozi-kwa-ngozi). Hatari kwa umma ni ndogo. WHO inashughulikia mlipuko huu kama kipaumbele cha juu ili kuzuia kuenea zaidi; kwa miaka mingi Ndui ya nyani imekuwa ikizingatiwa kuwa maambukizi yanayopewa kipaumbele. Matukio tunayoona kwa sasa si ya kawaida kwa sababu hakuna taarifa kuhusu usafiri kutoka nchi za asili au wanyama wanaosafirishwa kutoka nchi zilizo na ugonjwa huo. Kutambua jinsi virusi hivyo vinavyoenea na kulinda watu wengi zaidi dhidi ya kuambukizwa ni kipaumbele kwa shirika la Umoja wa Mataifa. Kuongeza ufahamu wa hali hii mpya kutasaidia kukomesha maambukizi zaidi. 

Je, Ndui ya nyani/Monkeypox ni ugonjwa wa zinaa? 

Ugonjwa huo unaweza kuenezwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kupitia migusano ya karibu ya mwili, pamoja na ngono. Hata hivyo, kwa sasa haijulikani ikiwa inaweza kuenea kwa njia ya ngono (kwa mfano, kupitia shahawa au maji maji ya uke). Hata hivyo, kugusa ngozi moja kwa moja na vidonda wakati wa shughuli za ngono kunaweza kueneza virusi. 

Vipele wakati mwingine huweza kuonekana kwenye sehemu za siri na mdomoni, ambayo pengine huchangia maambukizi wakati wa kujamiiana. Kwa hiyo, mgusano wa mdomo hadi wa ngozi unaweza kusababisha maambukizi wakati kuna vidonda katika mojawapo ya sehemu hizi. 

Upele unaweza pia kufanana na magonjwa mengine ya zinaa, kama vile herpes na kaswende. Hii inaweza kueleza kwa nini maambukizi mengi katika mlipuko wa sasa yametambuliwa miongoni mwa wanaume wanaotafuta huduma katika kliniki za afya ya ngono. 

Hatari ya kuambukizwa haiko tu kwa watu wanaofanya ngono au wanaume wanaofanya ngono na wanaume. Mtu yeyote ambaye ana mawasiliano ya karibu ya kimwili na mtu ambaye anaambukiza yuko hatarini. Yeyote ambaye ana dalili zinazoweza kuwa Ndui ya nyani anapaswa kutafuta ushauri wa mhudumu wa afya mara moja. 

Je, ni hatua gani zinachukuliwa na WHO kwa ujumbe wa unyanyapaa unaosambazwa mtandaoni kuhusiana Ndui ya nyani? 

Tumeona ujumbe unaonyanyapaa makundi fulani ya watu katika mlipuko huu. Tunataka kuweka wazi kabisa kwamba hii haikubaliki. 

 Kwanza kabisa, mtu yeyote ambaye ana mawasiliano ya karibu ya kimwili ya aina yoyote na mtu aliye na Ndui ya nyani yuko hatarini, bila kujali yeye ni nani, anafanya nini, anachagua nani kufanya naye ngono, au sababu nyingine yoyote. Pili, hairuhusiwi kuwanyanyapaa watu kwa sababu ya ugonjwa. Unyanyapaa unaweza tu kufanya mambo kuwa mabaya zaidi na kutuzuia kukomesha mlipuko huu haraka iwezekanavyo. Tunapaswa kusimama pamoja ili kusaidia mtu yeyote ambaye ameambukizwa au ambaye anasaidia kutunza watu ambao wanaumwa. Tunajua jinsi ya kukomesha kuenea na jinsi tunaweza kujilinda sisi wenyewe na wengine. Unyanyapaa na ubaguzi haukubaliki kamwe. Sote tuko pamoja katika hili.