Ndui ya Nyani au Monkeypox ni tishio la afya ya umma duniani- WHO

Vidonda vya Monkeypox mara nyingi huonekana kwenye mikono ya mikono.
© CDC
Vidonda vya Monkeypox mara nyingi huonekana kwenye mikono ya mikono.

Ndui ya Nyani au Monkeypox ni tishio la afya ya umma duniani- WHO

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO limetangaza kuwa mlipuko wa ndui ya nyani au monkeypox duniani ni tishio kwa afya ya umma.

Tangazo hilo limetolewa leo na Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Geneva, Uswisi baada ya kikao cha pili cha Kamati ya Kimataifa ya dharura za kiafya ya WHO kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa ndui ya nyani au Monkeypox.

Dkt. Tedros amesema ingawa wajumbe wa kamati hawakufikia muafaka kuhusu ndui ya nyani kama ni tishio au la kwa mujibu wa vigezo vya kutoa tamko hilo, ametangaza kuwa mlipuko ni tishio na umeenea zaidi Ulaya.

Hadi sasa, kwa mujibu wa Dkt. Tedros mlipuko umeendelea kukua na hadi sasa kuna waonjwa zaidi ya 16,000 kutoka nchi 45 na vifo  vya watu watano.

Amesema kilichobainika ni kwamba ugonjwa huo unasambaa zaidi miongoni mwa wanaume mashoga na wenye wapenzi zaidi ya mmoja na hivyo ni vyema kuchukua hatua kujikinga na iwapo hatua zitachukuliwa, ugonjwa huo unaweza kudhibitiwa na mlipuko kudhibitiwa.

Vigezo vitano

Vigezo vitano vya kuamua mlipuko ni tishio au la ni pamoja na mosi; taarifa zinazotolewa na nchi na kwa hili, virusi vimesambaa kwa kasi katika nchi ambako awali havikuweko. Pili; vipengele vitatu vya kutangaza dharura ya afya ya umma kwa muijbu wa kanuni za kimataifa na hiki kimefikiwa; Tatu; ushauri kutoka kamati ambayo haikufikia muafaka, nne; misingi ya kisayansi, Ushahidi na taarifa nyingine muhimu ambavyo sasa havitoshelezi na tano athari kwa afya binadamu, kusambaa kimataifa na uwezekano wa kuvuruga safari za kimataifa.”

Amesema tathmini ya WHO ni kwamba hatari ya ndui ya nyani ni ya kati duniani na katika kanda zote isipokuwa kanda ya Ulaya ambako hatari ni kubwa. 

Halikadhalika kuna hatari dhahiri ya kusambaa zaidi kimataifa, ijapokuwa hatari ya kuvuruga safari za kimataifa bado kwa sasa ni kidogo.

Dkt. Tedros amesema “tuna mlipuko ambao umesambaa duniani kote kwa kasi kupitia njia mpya, na sababu tunafahamu kwa kiwango kidogo sana na hivyo kukidhi vigezo vya kanuni za kimataifa.”

“Kwa misingi hiyo nimeamua kuwa mlipuko wa ndui ya nyani ni tishio la afya ya umma duniani. Nimeweka mapendekezo kwa makundi manne ya nchi. Ambazo hazijaripoti mgonjwa kabisa au ndani ya siku 21. Zile ambazo zimeripoti na zina maambukizi  baina ya binadamu. Hawa wachukue hatua kudhibiti mlipuko.

Kundi la tatu ni wale wenye maambukizi baina ya wanyama kwenda kwa binadamu na nne ni nchi zinazotengeneza vipimo vya uchunguzi, chanjo na matibabu.

Mkutano wa kwanza ulifanyika tarehe 25 mwezi uliopita wa Juni na kamati hiyo kwa kauli moja kubaini kuwa ingawa homa ya ndui ya nyani ni tatizo lakini lakini si dharura ya afya ya umma inayoleta hofu ya kimataifa.