Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu Mkuu wa UN ziarani nchini Uturuki kushughulikia mzozo wa Ukriane na Urusi

Mavuno ya ngano karibu na kijiji cha Krasne nchini Ukraine.
© FAO/Anatolii Stepanov
Mavuno ya ngano karibu na kijiji cha Krasne nchini Ukraine.

Katibu Mkuu wa UN ziarani nchini Uturuki kushughulikia mzozo wa Ukriane na Urusi

Masuala ya UM

Katika kushughulikia mzozo wa vita ya Ukraine na Urusi ambayo imepandisha gharama mbalimbali za mazao na mbolea hii leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewasili jijini Instanbul nchini Uturuki kwa ajili ya kutafuta suluhu ya changamoto hizo. 

Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu Farhan Haq akizungumza na waandishi wa habari hii leo jijini New York Marekani amewaeleza ziara hii ya Katibu Mkuu ni sehemu ya jitihada zake za kuhakikisha kuna upatikanaji kamili wa bidhaa za chakula za Ukraine, pamoja na chakula na mbolea kutoka Urusi.

Tweet URL

Haq amesema akiwa mjini Instanbul, Uturuki lengo kubwa wanalotarajiwa ni kuwa na makubaliano ambayo yataruhusu chakula na mbolea ya Ukraine na Urusi kufikia soko la kimataifa. 

“Kama ambavyo tumewadokeza kwa miezi mingi namna shida ya chakula duniani kote ilivyo mbaya, na hali hii kisababishi kikubwa ni mzozo wa nchi hizo kwahiyo tunachotaka ni kutatua hilo. Tunaweza kuokoa Maisha ya mamia ya maelfu, pengine watu milioni kadhaa ambao kwasasa wanaathirika bei kubwa ya chakula ambayo ipo nje ya uwezo wao. Kwahiyo hii ni sehemu ya hayo ikiwa kutafikiwa makubaliano.”

Duru kutoka vyombo mbalimbali vya habari duniani zinaeleza kuwa miongoni mwa mambo yatakayo jadiliwa ni pamoja na meli za Ukriane za nafaka kuruhusiwa kuingia na kutoka kupitia bandari ya Mined, Urusi imekubaliana na suluhu hii ya usafirishaji ambapo Uturuki ikisaidiana na Umoja wa Mataifa itahusika kwenye uchunguzi wa meli hizo ili kuondoa hofu ya usafirishaji wa silaha za magendo.

Alipoulizwa iwapo ana uhakika kama makubaliano hayo yatafikiwa naibu msemaji huyo wa katibu Mkuu alisema hali mpaka sasa ni tete. 

“Hali bado inasalia kuwa tete kwahiyo siwezi kusema ni lini makubaliano yoyote yatasainiwa. Kama ambavyo Katibu Mkuu alizungumza nanyi wiki iliyopita na amekuwa akisema wakati wote kwamba tunachukua hatua muhimu ili kuhakikisha usafirishaji salama na usalama wa bidhaa za chakula kutoka Ukraine kupitia bahari nyeusi. Alisema wakati ule kwamba kuna kazi iliyobaki kufanyika na ukweli kwamba amesafiri kwenda Instanbul inamaana tunaendelea na hili.” 

Ukraine na Urusi ni wauzaji wakuu wa ngano duniani kote, na urusi pia ni muuzaji mkubwa wa mbolea wakati Ukraine ni mzalishaji mkubwa wa mahindi na mafuta ya alizeti. 

Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine pamoja na kuziba bahari ya Ukraine umesababisha kusimamisha mauzo ya nje na kuacha makumi ya meli zikiwa zimekwama na zaidi ya tani milioni 20 za nafaka zimekwama kwenye ghala huko Odesa. 

Kulingana na ripoti mbalimbali za vyombo vya habari mavuno yanayokuja yapo hatarini kwakuwa Ukraine kwa sasa ina uhaba wa nafasi ya kuhifadhi mazao kutokana na kusimamishwa kwa mauzo ya nje. 

Umoja wa Mataifa pia unashughulikia kuwezesha usafirishaji wa nafaka na mbolea ya Urusi ambayo Moscow imesema imezuiwa na vikwavyo vya magharibi.