Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 na Ukraine vimetulazimu tupunguze ukubwa wa chapati- Prince

Prince Emmanuel mkimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC sasa yuko kambini Dzaleka nchini Malawi. yeye ni mpishi mzuri wa chapati lakini vita ya Ukraine na COVID-19 vimesababisha apunguze ukubwa wa chapati.
WFP Video
Prince Emmanuel mkimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC sasa yuko kambini Dzaleka nchini Malawi. yeye ni mpishi mzuri wa chapati lakini vita ya Ukraine na COVID-19 vimesababisha apunguze ukubwa wa chapati.

COVID-19 na Ukraine vimetulazimu tupunguze ukubwa wa chapati- Prince

Wahamiaji na Wakimbizi

Athari za kibiashara kutokana na COVID-19 pamoja na vita nchini Ukraine zinaendelea kusambaa duniani na zimebisha hodi hadi kwenye kambi ya wakimbizi ya Dzaleka nchini Malawi ambako ,mkimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC amelazimika kupunguza ukubwa wa chapati ili angalau aweze kuendelea kutoa huduma hiyo pendwa kwa wakimbizi na wakati huo huo apate angalau faida kidodo ili akidhi mahitaji yake na aweze kujitegemea

Mkimbizi huyo si mwingine bali ni Prince Emmanuel kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambaye akiwa kwenye kibanda chake cha kupika chapati kiitwacho, King Chapati katika kambi ya Dzaleka anasema alifika kambini hapa nchini Malawi mwaka 2019.

Baada ya kufika hapa, changamoto za nyumbani na fursa kambini vikawa fursa kwake!! Alilazimika kujifunza kupika chapati akisema, “Nilitafuta kazi ili nisaidie wazazi wangu Nilipata bahati ya kujifunza kupika chapati. Wakimbizi na wenyeji wanapenda chapati. Duka letu ndio ya zamani zadi katika kupika chapati hapa kambini na kila mtu anapenda King Chapati.”

COVID-19 na sasa vita ya Ukraine ikaongeza bei za malighafi yake ambayo ni unga na mafuta.

Bei ya unga na mafuta iliongezeka

Prince anasema “bidhaa zilipanda sana bei,” ambapo akizungumza kwa kuchanganya kiswahili na kifaransa anasema gharama ya unga iliongezeka kutoka dola senti 30 hadi dola senti 90 ilhali lita moja ya mafuta ilipanda kutoka dola senti 68 hadi dola 2 na senti 50. Hivyo ilibidi achukue hatua kwa kuzingatia kaulimbiu yake kwenye kibanda chake ni King Chapati, Adui wa Njaa!

Tuliamua kupunguza ukubwa wa chapati, wateja walilalama

Ilibidi wachukue hatua ili kuweza kupata faida akisema, “Kwa hiyo tukapunguza unene wa chapati na kisha tunatumia mafuta kidogo. Watu hawana fedha kambini na tukaona tukiongeza bei ya chapati tutakimbiza wateja.  Lakini wateja wetu hawafurahi sana kwa vile tulipunguza ukubwa wa chapati. Lakini tuliwaambia hakuna jinsi ni lazima tufanye vile ili wasitukimbie. Na yote ishakuwa bei kabisa.”

Takribani wakimbizi na wasaka hifadhi 43,000 wamesajiliwa katika kambi ya Dzaleka na WFP inaendelea kuwapatia mgao wa chakula pamoja na fedha taslimu ili waweze kukidhi mahitaji.

TAGS: Malawi, WFP, Dzeleka, Chapati, Ukraine, COVID-19