Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lajadili ripoti ya mwaka 2021 ya watoto katika maeneo yenye mizozo

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto kwenye maeneo ya mizozo, Virginia Gamba amewasilisha ripoti ya mwaka ya Katibu Mkuu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
UN Photo/Eskinder Debebe
Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto kwenye maeneo ya mizozo, Virginia Gamba amewasilisha ripoti ya mwaka ya Katibu Mkuu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lajadili ripoti ya mwaka 2021 ya watoto katika maeneo yenye mizozo

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekuwa na mjadala wake wa mwaka kuhusu watoto kwenye maeneo yenye mizozo ambapo Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto hao, Virginia Gamba amewasilisha ripoti ya mwaka ya Katibu Mkuu ambayo iliwekwa bayana kwa umma tarehe 11 mwezi huu wa Julai ikitaja aina sita ya vitendo vibaya zaidi vya ukiukwaji dhidi ya watoto. 

Ripoti ni ya kuanzia mwezi Januari hadi Desemba 2021 na imerekodi matukio 23,982 ya vitendo hivyo ambavyo ni watoto kuuawa na kujeruhiwa, kutekwa nyara, kubakwa na aina nyingine za ukatili wa kingono, mashambulizi dhidi ya shule na hospitali na kunyimwa huduma za kibinadamu. 

Maeneo ambako vitendo hivyo vimeshamiri zaidi ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Israel na eneo linalokaliwa la wapalestina, Somalia, Syria na Yemen. 
 

Patrick Kumi, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa NGO ya Mazingira Sawa Kutoka Sudan Kusini, akitoa maelezo kwa wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu watoto na migogoro ya silaha.
UN Photo/Eskinder Debebe
Patrick Kumi, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa NGO ya Mazingira Sawa Kutoka Sudan Kusini, akitoa maelezo kwa wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu watoto na migogoro ya silaha.

Akihutubia Baraza hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, Catherine Russell, ametoa wito kwa nchi wanachama, "kufanya zaidi" na "kwenda zaidi ya matakwa ya sheria" kulinda watoto. 

Bi.Russell amesema, “mna uwezo wa kutumia amri za kijeshi zisizo na sera za kutovumilia ukiukwaji mkubwa dhidi ya watoto. Tafadhali tumia nguvu hiyo. Kuidhinisha na kutekeleza tamko la Shule salama ili kuwalinda watoto na shule dhidi ya mashambulizi na matumizi mabaya ya pande zinazozozana. Kuidhinisha na kutekeleza Kanuni za Paris za kuwaondoa na kuwaunganisha tena katika jamii watoto ambao wametumiwa na vikosi vya kijeshi na vikundi. Tunatoa wito mtumie ushawishi wenu kusukuma mataifa na makundi yenye silaha yasiyo ya serikali kuzuia na kukomesha ukiukaji mkubwa dhidi ya watoto. " 

Hali nchini Ethiopia, Msumbiji, na Ukraine, zimeongezwa katika ajenda ya watoto na mizozo ya kivita katika ripoti ya mwaka 2021. 

Ushuhuda wa Patrick Kumi  

Mnamo mwaka wa 2016, Patrick Kumi, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali, NGO inayoitwa Similar Ground, alikuwa na umri wa miaka 15 wakati mwanachama wa kundi lenye silaha walipoteka nyara familia yake huko Sudan Kusini. 

"Walitutesa kwa kutusimamisha siku nyingi kwenye shimo lililojaa maji hadi shingoni na kutupiga," Patrick anasimulia yaliyotokea kabla hawajamuua baba yake mbele ya macho yake, anasimulia zaidi akisema, "niliambiwa nijiunge na jeshi au nife". 

Watoto wengi waliokuwa na bunduki walikuwa na wasichana waliowaita ‘wake’ na watu wazima pia walioa wenye umri wa miaka 14 au 15, aliendelea kueleza Patrick Kumi. 

Wakati wa shambulio la vikosi vya serikali, Kumi alieleza jinsi "aliponea chupuchupu kifo" alipotembea kwa siku mbili hadi Uganda. Miezi kumi na moja baadaye alipata wanafamilia ambao pia walikuwa wamenusurika. 

Mnamo mwaka 2018, kijana huyo alijiunga na mpango wa uchemuzi unaoongozwa na vijana, ambapo aliendesha mradi wa kuwalinda yatima na watoto waliotenganishwa. 

Ilimchukua miaka mitatu kupata nafuu, na kwa sasa amejiandikisha kupata shahada ya Haki za Kibinadamu, Amani, na Mwitikio wa Kibinadamu. 

Mchechemuzi huyo mdogo ametoa mapendekezo kadhaa kusaidia maelfu ya watoto wanaopitia mfadhaiko huo kama alivyokuwa ameishi. 

"Children leaving armed groups need our full support to heal" | United Nations Security Council

Mapendekezo hayo ni pamoja na ujumuishaji bora zaidi kwa ushirikiano ulioboreshwa wa serikali na miradi ya kitaifa na kimataifa, pamoja na kuwapa waathirika fursa ya kushiriki katika "vipengele vyote" vya sera na programu, kuhusu kupona kwao. 

"Ikiwa imekusudiwa kwa ajili ya watoto na vijana, basi achene iwe kwa ajili yao." Amesema. 

Kusoma taarifa ya ripoti hiyo iliyowasilishwa Julai 11, 2022 bofya hapa