Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa DRC waliokuwa nchini Angola waanza kurejea makwao kwa hiari

Mkimbizi wa Kongo Verónica Angélica anatazamia kurejea nyumbani kutoka katika makazi ya wakimbizi ya Lôvua nchini Angola.
© UNHCR/Lina Ferreira
Mkimbizi wa Kongo Verónica Angélica anatazamia kurejea nyumbani kutoka katika makazi ya wakimbizi ya Lôvua nchini Angola.

Wakimbizi wa DRC waliokuwa nchini Angola waanza kurejea makwao kwa hiari

Wahamiaji na Wakimbizi

Wakimbizi kutoka Jamhuri ya kidemokrasia kongo DRC waliokuwa wamekimbilia nchini Angola wameanza kurejea kwa hiyari nchini mwao hii leo, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi duniani UNHCR. 

Taarifa iliyotolewa leo na UNHCR jijini Geneva Uswisi imesema kundi la kwanza la w akimbizi 88 limeanza safari yake kutoka Angola kwa kutumia magari ya Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM na wameeleza japo kuna vita inaendelea mashariki mwa DRC, kuimarika kwa usalama Magharibi mwa DRC kumewezesha wananchi hao kuamua kurejea nchini mwao kwa utu na usalama. 

Urejeshwaji huo wa hiari wa wakimbizi wa DRC umeratibiwa na UNHCR kwakushirikiana na serikali ya Angola, DRC, Shirika la IOM pamoja na wadau wengine mbalimbali. 

Baada ya kuwasili nchini DRC wakimbizi hao watapatiwa msaada wa fedha taslimu ili kusaidia kujikimu na mahitaji ya kimsingi kama vile usafi na vifaa vya nyumbani. Usaidizi wa ziada pia utatolewa kwenye maeneo muhimu zaidi kama vile Watoto kuandikishwa shule. 

Taarifa hiyo imeeleza msafara huo unaopitia mpaka wa Chicolondo unatarajiwa kuvuka mpaka wa kuingia DRC hapo kesho. Misafara mingine imepangiwa kutumia mpaka wa Chiddanda katika wiki zijazo  ambapo wakimbizi watapelekwa katika kambi mbalimbali zilizopo magharibi mwa DRC ikiwemo Kasai, Kasai Kati, Kwilu, Sankuru, Lomami, Lualaba na Makao Makuu ya DRC Kinshasa. 

Familia ya wakimbizi nchini Angola yakutana na mamlaka na maafisa wa UNHCR kabla ya kurejea kwa hiari katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
© UNHCR/Lina Ferreira
Familia ya wakimbizi nchini Angola yakutana na mamlaka na maafisa wa UNHCR kabla ya kurejea kwa hiari katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Tunafuraha kurejea nyumbani 

Zaidi ya wakimbizi 600 wa DRC wameonesha nia na utayari wa kurejea nchini mwao kwa hiyari. UNHCR imesema wanatarajia wengi zaidi kujitokeza wakati zoezi hilo likiendelea. 

Programu ya kuwarejesha wakimbizi kwa hiari kutoka nchini Angola ilianza mwaka 2019 lakini ilivurugika mwaka 2022 kutokana na ubovu wa barabara na madaraja katika eneo la mto Kasai pamoja na janga la COVID-19 lililo sababisha mipaka ya nchi kufungwa. 

Takriban wakimbizi 3000 walirejea nchini DRC katika awamu ya kwanza ya urejeshaji wa hiari. 

Tweet URL

Shughuli za UNHCR nchini Angola na DRC

UHNCR inasaidia takriban wakimbizi na wasaka hifadhi 57,000 nchini Angola ambao wengi wao wanaishi maeneo ya mijini. Ingawa mahitaji ya kifedha kwa mwaka huu ni dola milioni 29.8 lakini wamepokea dola milioni 10.3 tu hali inayowaacha katika ukata mkubwa wa kuwapatia wahitaji mahitaji muhimu ya kibinadamu.
Wakati huo huo UNHCR imepokea asilimia 19 pekee ya jumla ya dola milioni 225 zinazohitajika kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya kibinadamu ya wakimbizi wa ndani nchini DRC.

Takwimu za wakimbizi wanaorejea duniani kote

Takwimu za mwaka 2021 za UNHCR zinaonesha ulimwenguni kote takriban watu 430,000 waliweza kurejea makwao kwa utu na usalama ikiwa ni ongezeko la asilimia 71 ikilinganishwa na mwaka uliopita. 

Karibu theluthi mbili ya wakimbizi hao waliorejea walikuwa kutoka Sudan kusini. Idadi hii inawakilisha asilimia mbili tu ya wakimbizi wote duniani. 

UNHCR inasema wakimbizi wengi hawataki jingine lolote isipokuwa kurejea mwakao. 

Jumuiya ya kimataifa ina uwezo wakupunguza idadai ya miaka wakimbizi wanayoishi uhamishoni. Hili linawezekana iwapo kwa pamoja watasaidia kushughulikia sababu za migogoro na kusaidia nchi kuzifanya ziwe salaam na rahisi kwa watu wao kurejea.