Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi wa Afrika wazindua mpango wa ‘Eduation Plus’ kusaidia wasichana kuendelea na shule 

Kuwekeza katika elimu kunaweza kuwalinda wanawake na wasichana dhidi ya Virusi Vya Ukimwi.
UNAIDS
Kuwekeza katika elimu kunaweza kuwalinda wanawake na wasichana dhidi ya Virusi Vya Ukimwi.

Viongozi wa Afrika wazindua mpango wa ‘Eduation Plus’ kusaidia wasichana kuendelea na shule 

Utamaduni na Elimu

Viongozi waliokutana katika mkutano wa Muungano wa Afrika mjini Lusaka, Zambia hii leo wameahidi kuunga mkono mpango wa ‘Education Plus’ wakijitolea kuchukua hatua ya kuwafanya wasichana kubaki shuleni, jambo ambalo litapunguza kwa kiasi kikubwa uwezekano wao wa kuambukizwa Virusi Vya UKIMWI, VVU. 

Katika taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na UKIMWI, UNAIDS iliyotolewa hii leo jijini Lusaka, Zambia na Geneva, Uswisi, imeeleza kuwa Kila wiki, takriban wasichana 4,200 na wanawake vijana katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara hupata VVU. Mnamo mwaka 2020, vijana sita kati ya saba wenye umri wa kati ya miaka 15-19 waliopata VVU katika eneo hilo, walikuwa wasichana. “Zaidi ya wanawake vijana 23,000 walikufa kutokana na magonjwa yanayohusiana na UKIMWI mwaka 2020, na kuifanya kuwa sababu ya pili ya vifo kati ya wanawake wenye umri wa miaka 15-29 baada ya vifo vya uzazi katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.” Imeeleza taarifa hiyo.  

Kuwafanya wasichana wabaki katika shule za upili au sekondari na kuwapa stadi za maisha, mafunzo na fursa za ajira "ni muhimu katika kumaliza janga la UKIMWI barani Afrika". Utafiti wa UNAIDS unaonesha kuwa kuhakikisha kuwa wasichana wanamaliza elimu ya sekondari kunapunguza hatari ya kupata VVU kwa hadi nusu, na kwamba kuchanganya hii na mfuko wa huduma na haki za uwezeshaji wa wasichana kunapunguza hatari yao bado. 

Education Plus inataka elimu ya sekondari iwe ya bila kulipia na bora kwa wasichana na wavulana wote katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ifikapo mwaka 2025; upatikanaji wa elimu ya kina ya ujinsia kwa wote; utimilifu wa afya na haki za ngono na uzazi; uhuru dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia na kingono; mabadiliko ya kutoka shule hadi kazini, na uhakika wa kiuchumi na uwezeshaji. 

"Serikali yangu imejitolea kutoa elimu ya bure (bila malipo) ya msingi na sekondari kwa wote," amesema Rais Hakainde Hichilema wa Zambia, ambaye alikuwa mwenyeji wa mkutano huo na kisha akaongeza akisema, "elimu ni kitu muhimu cha kuleta usawa mkubwa na kwa elimu ifaayo, kila mtu anapewa fursa ya kuchunguza uwezo wake kamili na kuweza kushiriki katika mchakato wa maendeleo. Upatikanaji wa elimu unawapa uwezo wasichana na wavulana kwani inawaongezea uwezo wa kupata kazi zenye staha na mengineyo." njia za uzalishaji na hivyo kupunguza umaskini." 

Rais wa Senegal na ambaye mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika, Macky Sall, akizindua mpango huo akiwa na marais wengine watatu na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Muungano wa Afrika Moussa Faki Mahamat. 

Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS, Winnie Byanyima, katika hotuba yake kwenye uzinduzi huo amesema, “tunapiga hatua barani Afrika lakini hatuna kasi ya kutosha. Tunahitaji kushughulikia kwa haraka ukosefu wa usawa wa kijinsia ambao bado unasumbua bara la Afrika, na athari mbaya kwa wasichana maskini na wanawake vijana. Hatuna dakika ya kusubiri. Tukifanya kazi pamoja, sote tunaweza kukomesha sheria za ubaguzi na kanuni za kijamii zenye madhara, hivyo kwamba wasichana wetu wana afya, wamesoma na wamewezeshwa na wanaweza kuliongoza bara letu la Afrika mbele." 

Mpango wa Education Plus umechukua uharaka zaidi kutokana na kwamba janga la COVID-19 limesaukuma mamilioni ya wasichana nje ya shuleni. Hata kabla ya janga hili, karibu wasichana milioni 34 waliobalehe wenye umri wa miaka 12 hadi 17 katika eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara hawakuwa katika shule za sekondari. Ushahidi pia unaonesha kuwa wasichana wana uwezekano mdogo wa kuanza tena shule mara tu wanapoacha shule. 

Nchi kumi za Afrika - Benin, Cameroon, Eswatini, Gabon, Gambia, Lesotho, Malawi, Sierra Leone, Afrika Kusini na Uganda, hadi sasa zimejitolea kutekeleza mpango huo ambao umeitishwa kwa pamoja na mashirika matano ya Umoja wa Mataifa, UNAIDS, UNESCO, UNFPA, UNICEF na UN Women, na unaleta pamoja serikali, mashirika ya kiraia na washirika wa kimataifa.