Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Botswana mbioni kufikia malengo ya UN ya kupambana na UKIMWI

UNAIDS
Photo: UNAIDS
UNAIDS

Botswana mbioni kufikia malengo ya UN ya kupambana na UKIMWI

Afya

Botswana inatarajiwa kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kufikia malengo ya kutafiti, kugundua na kuwapatia matibabu wanaogundulika kuwa na UKIMWI,  yaliyowekwa na Baraza kuu la Umoja wa Mataifa miaka minane kabla ya muda uliowekwa. 

Ripoti iliyotolewa leo na timu ya Umoja wa Mataifa ikiongozwa na Mratibu Mkaazi nchini Botswana Zia Choudhury imesema lengo la Baraza Kuu la UN la 95-95-95 ifikapo mwaka 2030 linakaribia kufikiwa na maeneo mengine limeshafikiwa.

“Kulingana na utafiti wa hivi karibuni, asilimia 93 ya makadirio ya watu wanaoishi na Virusi Vya UKIWMI- VVU wanafahamu hali zao, asilimia 97.9 waliokuwa wameshafahamu wapo kwenye tiba ya kurefusha maisha na asilimia 98 ya wale walio kwenye tiba wameweza kufifisha na kupunguza wingi wa virusi ili kupunguza kiwango cha VVU hadi kufikia kiwango kisichoweza kutambulika.”

Timu ya Umoja wa Mataifa pia imeongeza usaidizi wake kwa mamlaka ya Botswana kwenye programu ya kuzuia maambukizi kwa jamii huku ikiweka mkazo zaidi kwa barubaru na wanawake.

Timu hiyo pia imeeleza inafanya kazi kuhakikisha uthabiti wa mwitikio ili kuboresha ufanisi wake na kushughulikia vizuizi vya kimuundo, vinavyojumuisha unyanyapaa ambao unawazuia watu kupata huduma.