Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tukitumia kiswahili kufundishia tunaweza kuweka hata utani ili wanafunzi waelewe zaidi

Beni, mji ulioko kaskazini mwa jimbo la Kivu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo DRC
© UNICEF/Arlette Bashizi
Beni, mji ulioko kaskazini mwa jimbo la Kivu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo DRC

Tukitumia kiswahili kufundishia tunaweza kuweka hata utani ili wanafunzi waelewe zaidi

Utamaduni na Elimu

Ikiwa ni wiki moja baada ya dunia kuadhimisha kwa mara ya kwanza siku ya Kimataifa ya Kiswahili tarehe 7 Julai, wadau wa elimu nchini Jamuhuri ya kidemokrasia ya congo DRC wamesema nimuda muafaka wa Kiswahili kuchukua nafasi kubwa ya kufundishia wanafunzi badala ya lugha ya kiingereza na kifaransa zinazo tumika sasa. 

Wadau hao wamemueleza mwandishi wa idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa Byobe Malenga kuwa tayari wana sehemu nzuri ya kuanzia iwapo ombi hilo litakubalika kwakuwa nchini huko katika baadhi ya vyuo vikuu wanafundisha lugha hiyo.

Byobe Malenga alitembelea Chuo Kikuu cha ualimu cha ISP cha Bukavu jimboni Kivu Kusini pamoja na Beni jimboni Kivu Kaskazini ambapo katika mahojiano yake na mwalimu Kambale Muingieti Chirck amemueleza amekuwa akifundisha lugha ya Kiswahili kwenye Chuo Kikuu cha ualimu katika mji wa Beni kwa miaka mingi na angetamani masomo yote yafundishwe katika lugha ya Kiswahili.

“Wakati nafundisha kwa lugha ya Kiswahili najisikia vizuri sana kwani ni lugha ambayo tunaizungumza muda wote na makabila mengi wanaizungumza hivyo tunaelewana. Hapa shule kama masomo yote yangefundishwa kwa lugha ya Kiswahili wanafunzi wameengela zaidi na wangefaulu mitihani kwani hata tungeweza kutumia utani wakati wa kufundisha kwakuwa tunajaua wanafunzi wanazungumza kiswahili.” 

Profesa Kambale pia anapendekeza serikali iweke amri ya lugha ya Kiswahili kama lugha rasmi ya mazungumzo mashuleni kuliko sasa ambapo lugha zinazotumika ni Kifaransa na kingereza.

“Napenda kushauri mamlaka za usajili wa shule waweke lugha hii kama namba moja ya kujifunza na pia kuwe na somo la kiswahili ili wanafunzi waweze kuzungumza kwa ufasaha kama ambavyo sasa wanamasomo ya kifaransa na kingereza. Na muhimu zaidi ni kuhamasisha kipindi cha mapumziko hapa shuleni wanafunzi wahamasishwe kuzungumza lugha ya Kiswahili.”  

Lokua Kanza, balozi wa kitaifa wa UNICEF nchini DRC kuhusu elimu ametembelea shule aliyosoma utotoni na kusihi wanafunzi kuzingatia umuhimu wa elimu.( Maktaba)
UNICEF/Josue Mulala
Lokua Kanza, balozi wa kitaifa wa UNICEF nchini DRC kuhusu elimu ametembelea shule aliyosoma utotoni na kusihi wanafunzi kuzingatia umuhimu wa elimu.( Maktaba)

Wanafunzi nao wanena

Sio BENI tu ndipo lugha ya kiswahili inafundishwa, katika Chuo Kikuu cha Bukavu lugha ya Kiswahili pia ni miongoni mwa somo sinazo fundishwa. Baadhi ya wanafunzi hapa wanaelezea. 

“Kiswahili kwangu kipo na maana kubwa sana na muhimu kwakuwa kitanisaidia kuelewana ana watu wengi, nikienda Lubumbashi nikiongea Kiswahili na nikiwa hapa Beni nitaongea Kiswahili. Kwa sasa Kiswahili chetu kinatofautiana lakini nikijifunza tutaweza kuelewana.” amesema Amina juma

Mwanafunzi mwingine aliyezungumza ni Neema Kishiganyi mwanafunzi wa chuo kikuu huko Bukavu amesema yeye anasoma Kiswahili darasani kwakuwa ni moja ya lugha zinazo zungumzwa nchini DRC na moja ya lugha zinazo zungumza zaidi barani Afrika

“Ushawishi ambao lugha ya Kiswahili unao ni kuwa inazungumzwa na watu katika dunia nzima, ni lugha rahisi kujifunza na inatusaidia kuongea na watu wengi duniani wakubwa kwa Watoto.”

Wanafunzi wengine walieleza wanatamani zaidi kama wakijifunza Kiswahili rasmi ili wanapomaliza masomo yao waweze kuzungumza na wale watakao wahudumia akitolea mfano mwanafunzi anayesomea udaktari ataweza kuwahudumia wagonjwa wanaozungumza Kiswahili kwa urahisi zaidi kwakuwa watakuwa wanazungumza lugha moja.

DRC ina lugha nne za taifa ambazo ni Kiswahili, Lingala, Kikongo na Chiluba huku lugha ya Kiswahili ikizungmzwa na watu wengi zaidi katika nchi hiyo yenye zaidi ya watu milioni tisini iliyoko Afrika Mashariki.