Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Janga la chakula duniani: Mwale wa matumaini waonekana – Guterres

Kinu cha kuhifadhi nafaka huko Lvivska nchini Ukraine
© FAO/Viktoriia Mykhalchuk
Kinu cha kuhifadhi nafaka huko Lvivska nchini Ukraine

Janga la chakula duniani: Mwale wa matumaini waonekana – Guterres

Masuala ya UM

Hii leo huko Istanbul Uturuki tumeshuhudia hatua muhimu ya kuhakikisha kuwa mazao ya chakula zikiwemo nafaka kutoka Ukraine yanasafirishwa na kuuzwa nje ya nchi hiyo kwa usalama kupitia Bahari Nyeusi, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani baada ya makubaliano ya kuwezesha hatua hiyo iliyochukua muda mrefu kufikiwa.

Mwale wa matumaini katikati ya kiza kinene duniani

Vyombo vya habari vinaripoti kuwa kutokana na makubaliano hayo, sasa Ukraine itaweza kuuza nje ya nchi mazao ya nafaka baada ya kuzuiliwa kufanya hivyo na Urusi.

Pande hizo husika zitakutana wiki ijayo kutia Saini makubaliano hayo ikiwemo maeneo ya pamoja ya udhibiti wa usafirishaji wa nafaka hizo ambazo uhaba wake ulileta machungu kwa mamilioni ya watu duniani.

Guterres amefananisha hatua hiyo na mwale wa matumaini katikati ya kiza kilichoghubika dunia iliyosheheni majanga.

Tweet URL

“Mwale wa matumaini kupunguza machungu ya binadamu na kuondoa njaa duniani kote. Mwale wa matumaini wa kusaidia nchi zinazoendelea na watu walio hatarini zaidi. Mwale wa matumaini wa kuleta kile kinachohitajika zaidi ili kuweko na utulivu kwenye mfumo wa chakula duniani, » amesema Katibu Mkuu.

Tangu kuanza kwa vita nchini Ukraine tarehe 24 mwezi Februari mwaka huu, Katibu Mkuu amekuwa akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha bidhaa za vyakula kutoka Ukraine na Urusi pamoja na mbolea kutoka Urusi vinapatikana kwenye soko la dunia.

Nilisafiri hadi Moscow, Urusi na Kyiv nchini Ukraine kupendekeza suluhu za matatizo hayo mawili.  Tangu wakati huo, kila siku tumekuwa tukihangaika kutwa kucha kupitia mazungumzo lukuki,” ametanabaisha Katibu Mkuu.

Mambo ni shwari, lakini bado kuna hatua za kuchukua

Bwana Guterres amesema hatua zaidi za kiufundi zinahitajika ili sasa kuweza kutekeleza kivitendo kile kilichokubaliwa hii leo.

“Hatimaye lengo si makubaliano tu kati ya Urusi na Ukraine, bali makubaliano ya Dunia nzima,” amesema Katibu Mkuu huku akitoa shukrani za dhati kwa serikali ya Uturuki kwa jitihada zake za kipekee za kuitisha mazungumzo hayo na nafasi yake pia katika kusonga mbele.

Lori likishusha mahindi kwenye kiwanda cha kuchakata nafaka hiyo huko Skvyra nchini Ukraine
© FAO/Genya Savilov
Lori likishusha mahindi kwenye kiwanda cha kuchakata nafaka hiyo huko Skvyra nchini Ukraine

Ameshukuru pia maafisa wa Urusi na Ukraine kwa ushiriki wao wa dhati kwenye mazungumzo hayo huku akisema, “napongeza azma ya pande zote ya kuhakikisha wanafikia makubaliano kwa ajili ya utu wa binadamu.”

UN imejipanga kusonga mbele

Guterres amesema Umoja wa Mataifa kwa upande wake utatekeleza wajibu wake kusaidia kufuatialia, “nashukuru timu ya Umoja wa Mataifa ikiongozwa na Rebeca Grynspan na Martin Griffiths, ambao walikuwa na jukumu la kuandaa Mpango wa Umoja wa Mataifa.”

Katibu Mkuu amekumbusha kuwa  hatua ya leo ni kiashiria cha manufaa ya mazungumzo pindi kunapokuwa na mzozo.

“Hebu tusisahau kuwa mazungumzo yamefanyika wakati umwagaji damu unaendelea. Lakini habari njema kutoka Istanbul zinaonesha umuhimu wa mazungumzo, na tutumie mfano huo kutekeleza hilo kwa mujibu wa Chata ya  Umoja wa Mataifa,” amesema Guterres.