Skip to main content

WHO kuchunguza kuenea kwa homa kali ya ini isiyojulikana

Chanjo dhid ya homa ya Ini aina ya B Argentina
Photo: WHO/PAHO
Chanjo dhid ya homa ya Ini aina ya B Argentina

WHO kuchunguza kuenea kwa homa kali ya ini isiyojulikana

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO limezindua utafiti duniani kote wenye lengo la kubaini idadi halisi na kiwango cha aina ya ugonjwa wa homa ya ini kali, Hepatitis miongoni mwa watoto, ambao ni tofauti na aina zote za homa ya ini zinazotambulika, wakati huu ambao ugonjwa huo umeripotiwa katika kanda 5 za WHO isipokuwa barani Afrika.

Taarifa ya WHO iliyotolewa leo jijini Geneva, Uswisi inasema Kati ya tarehe 5 mwezi Aprili mwaka huu ugonjwa huo wa homa ya ini kali ulipobainika mara ya kwanza na tarehe 8 mwezi huu wa Julai mataifa 35 katika kanda 5 za shirika hilo yaliripoti jumla ya watoto 1010 wanaoshukiwa kuwa na aina hiyo kali ya homa ya ini ambapo kati yao hao watoto 22 wamefariki dunia.

WHO inasema tangu ripoti ya tarehe 24 mwezi uliopita, kumekuwepo na wagonjwa wapya 90 wanaoshukiwa kuugua ugonjwa huo na vifo vinne huku mataifa mengine mawili ambayo ni  Luxembourg na Costa Rica, yakiripoti kuwa na washukiwa wa ugonjwa huo.

Shirika hilo linasema lengo la utafiti wake pia ni kuonga kama kuna ongezeko la wagonjwa kati ya sasa na miaka mitano ilioypita, kuelewa umri wa wagonjwa sambamba na iwapo ni kwa kiasi gani ini la mtoto mwenye umri wa chini ya miaka 16 limeharibika hadi mgonjwa anahitaji kupandikizwa ini jipya.

Takribani nusu ya wagonjwa washukiwa wako kanda ya WHO barani Ulaya, ikifuatiwa na Amerika, halafu Pasifiki Magharibi, kisha Kanda ya Kusini-Mashariki mwa Asia na mwisho kanda ya Mediteranea Mashariki.

WHO inasema kati ya wagonjwa 100 ambao takwimu zao za hospitali zimepatikana, wengi wao wameripoti kupata kichefuchefu au kutapika, wengine homa ya manjano, uchovu wa mwili na maumivu ya tumbo.

WHO inasema takwimu halisi zinaweza kuwa juu kwa sababu ya changamoto katika mfumo wa ufuatiliaji na kwamba idadi inaweza kuongezeka kadri taarifa zinavyozidi kuthibitishwa.

Wakati utafiti ukiendelea WHO inataka hatua za kujikinga dhidi ya homa ya ini ikiwemo usafi wa mikono, kuepuka maeneo yenye mikusanyiko, kunywa maji safi na salama, kula chakula kilichopikwa kwa usafi na kilichoiva vizuri na kuepuka maeneo yasiyo na hewa.