Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Matumbawe ya asili yaharibiwa, wanakijiji Kuruwitu waunda ya saruji na kuyaweka baharini

Wananchi wa kijiji cha Kuruwitu wakipakia matumbawe ya saruji kwenye boti tayari kwa kwenda kuyaweka katika eneo lililojitenga baharini.
UN/Thelma Mwadzaya
Wananchi wa kijiji cha Kuruwitu wakipakia matumbawe ya saruji kwenye boti tayari kwa kwenda kuyaweka katika eneo lililojitenga baharini.

Matumbawe ya asili yaharibiwa, wanakijiji Kuruwitu waunda ya saruji na kuyaweka baharini

Tabianchi na mazingira

Maeneo ya ufukweni katika Kaunti ya Kilifi, Kenya yanavutia kwani ni tulivu na makazi ya viumbe mbalimbali. Matumbawe yana uhai na ni kiungo muhimu katika mfumo wa uhai kwenye mazingira ya baharini lakini katika baadhi ya maeneo kama Kuruwitu, kuna nyakati ambapo matumbawe yalikuwa hatarini kutoweka. Mwaka 2003 wakaazi wa Kuruwitu waliamua kuanzisha mpango wa kuimarisha hali ya bahari baada ya samaki kupungua na biashara ya matumbawe kuleta madhara. 

Eneo tengefu 

Miaka 12 iliyopita wanakijiji wa Kuruwitu walilitenga eneo la ukubwa wa hekari 30 baharini ili kulipa nafasi lipate uhai mpya. Uvuvi na shughuli zozote zilipigwa marufuku kwa kipindi hicho. Kwa sasa wavuvi na wakaazi wameona tija. Dickson Gereza ni msimamizi wa mradi na mlinzi wa bahari katika shirika la Kuruwitu Conservancy lililoko Kilifi na anaelezea akisema, “tangu jadi wakaazi wa Kuruwitu tumekuwa tukitegemea bahari kwa uvuvi. Awali tuliona samaki wengi na wavuvi walifurahi.Samaki walipoanza kupotea tukaamua kuunda eneo tengefu mwaka 2003 ili tuipe fursa bahari kupata uhai mpya.” 

Eneo la pwani lililojitenga katika kaunti  ya Kilifi nchini Kenya.
UN/ Thelma Mwadzaya
Eneo la pwani lililojitenga katika kaunti ya Kilifi nchini Kenya.

Uvuvi na matumbawe kuvunjika 

Eneo hilo sasa limenawiri na kuwa mazalio ya samaki.Samaki na viumbe vidogo hujificha na kupata stara kwenye matumbawe na mapango ya bahari.Matumbawe ya eneo la Kuruwitu yalikuwa yameharibiwa na nyavu, uvuvi na shughuli nyingine za baharini. Ili kuinusuru hali, wataalam waliingilia kati na kuchukua hatua mikononi mwao. Katana Hinzano ni mwanasayansi na mtengezaji matumbawe ya saruji kwenye shirika la ulinzi wa bahari la Oceans Alive na anafafanua kinachoharibu matumbawe kuwa ni, “baadhi wanavua kwa kutega baruti (fataki) majini. Milipuko hiyo inapofyatuka matumbawe yanavunjika na mazingira yote ya baharini yanaharibika. Pia kuna ongezeko la viwango vya joto ulimwenguni ambavyo vinachangia matumbawe kupauka. Kadhalika kuna mavuvi mabaya ya kutumia nyavu kubwa ambazo zinatandazwa kwenye sehemu pana kisha zinaburutwa. Zinapoburutwa matumbawe yanavunjika.” 

Bahari inaleta biashara 

Wakaazi wa Kuruwitu wamekuwa wakiitegemea bahari kwa mahitaji ya kila siku tangu jadi. Eneo hilo la urefu wa kilomita 12 ufuoni mwa bahari lina wakaazi wasiopungua alfu 30 kutokea vijiji vitatu na bandari 6. 

Kenya ina ukanda wa pwani ulio na urefu wa kilomita 500 kutokea Lamu hadi Mombasa. Mbali ya uvuvi, shughuli za utalii na usafirishaji wa biashara ni nguzo muhimu ya uchumi wa pwani. Biashara ya rasilmali za bahari nayo pia ina mchango muhimu. Goodluck Mbaga ni mwanamazingira na afisa wa hiari ya shirika la wanyamapori nchini Kenya, KWS, na anaelezea umuhimu wa bahari kwa mkaazi wa pwani akisema, “baada ya kujifunza kuhusu ulinzi wa mazingira, sasa tumekuja kuona umuhimu wa kuitunza bahari. Pale samaki walipoanza kutoweka wavuvi waliridhia kuelezwa na wakachukua hatua. Kwa sasa samaki wamerejea na biashara nyingine zimeibuka kama uuzaji wa vyakula na vinywaji kwa watalii wanaokuja kupiga mbizi.” 

Hapa ni mfano wa kitanda cha chuma kikiwa na nyavu moja ya mbinu ya kupandikisha matumbawe baharini katika kaunti ya kilifi nchini Kenya.
UN/ Thelma Mwadzaya
Hapa ni mfano wa kitanda cha chuma kikiwa na nyavu moja ya mbinu ya kupandikisha matumbawe baharini katika kaunti ya kilifi nchini Kenya.

Matumbawe yaunganishwa na gundi maalum 

Je, matumbawe ya saruji yanaandaliwa vipi kabla ya kutumbukizwa baharini? Katana Ngala Hinzano ni mwanasayansi na mlinzi wa bahari kutokea Kuruwitu na anafafanua akisema, “kwanza tunaandaa ‘nasari’ kwa kutengeza kitanda maalum cha chuma na nyaya za plastiki. Baada ya hapo tunaunda vigingi vidogo kwa simiti (Simenti/Saruji) na mchanga kisha kuviacha vikauke kwa siku 14. Siku moja kabla tunakagua matumbawe yalivyo kisha tunaunganisha vigingi vile kwa gundi maalum na kuviacha vishikane. Kinachofuatia ni kusafisha eneo zima kuondoa mwani ili tumbawe lipate hewa na nafasi ya kuota upya.” 

Mfano wa matumbawe na haya yametengenezwa kwa zege tayari kutumbukizwa baharini kama sehemu ya kurejesha matumbawe halisi.
UN/ Thelma Mwadzaya
Mfano wa matumbawe na haya yametengenezwa kwa zege tayari kutumbukizwa baharini kama sehemu ya kurejesha matumbawe halisi.

Kwa sasa hifadhi ya KWCA inashirikiana na vitengo vya usimamizi wa uvuvi na masuala ya ufukweni, BMU, serikali na wadau wengine kuandaa mkakati na mpango mpya utakaohifadhi eneo kubwa zaidi la bahari la ekari 800 yaliko matumbawe.Azma ni kuwawezesha wavuvi kuelewa matumizi sahihi ya rasilmali za bahari,kupungua hasara ya samaki kuharibika na pia kuimarisha mifumo ya soko la bidhaa za baharini. 

Tuzo ya Equator ya UNDP 

Kwa mujibu wa takwimu, maeneo 3844 ya baharini yanalindwa na kuhifadhiwa na jamii kote ulimwenguni ila kwa eneo la magharibi ya bahari ya Hindi bado ni machache. 

Misumari iliyotengenezwa kwa zege na hii hutumika kwenye harakati za kurejesha matumbawe huko Kilifi nchini Kenya.
UN/Thelma Mwadzaya
Misumari iliyotengenezwa kwa zege na hii hutumika kwenye harakati za kurejesha matumbawe huko Kilifi nchini Kenya.

Mwaka 2017 mradi huu wa ulinzi wa matumbawe na eneo la bahari ulijinyakulia tuzo ya Equator ya shirika la Umoja wa Mataifa la maendeleo, UNDP, kupitia mpango wa Equator Initiative.Tuzo hiyo hutolewa mara mbili kwa mwaka kuzitambua juhudi za wanakijiji na jamii za kupunguza umasikini kwa kuhifadhi na kulinda mazingira kadhalika matumizi mbadala ya viumbe anuwai. Juhudi zote hizo zinaelekea katika kutimiza malengo endelevu ya milenia ya maendeleo ya Umoja wa Mataifa.