Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yatoa mwongozo mpya kwa wagonjwa wa kifua Kikuu

Nchini India, daktari akiangalia picha ya X-ray kama inauharibifu kutokana na kifua kikuu.
© ILO/Vijay Kuty
Nchini India, daktari akiangalia picha ya X-ray kama inauharibifu kutokana na kifua kikuu.

WHO yatoa mwongozo mpya kwa wagonjwa wa kifua Kikuu

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO hii leo limetoa kitabu kipya cha mwongozo kilicho sheheni maelekezo pamoja na sura mpya kadhaa za namna ya kuwahudumia wagonjwa wa Kifua kikuu au TB lengo likiwa ni kuboresha maisha yao pamoja na kuwapa matokeo bora ya kitabibu.  

Taarifa iliyochapishwa kwenye wavuti wa WHO imesema mwongozo huo umetolewa mahususi ukiwalenga watendaji katika sekta ya afya wanaohusika na program za kitaifa za TB, au washirika wake katika wizara za afya, watunga sera, mashirika ya kiufundi yanayoshughulikia masuala ya TB na magonjwa ya kuambukiza katika sekta ya umma na binafsi lengo likiwa ni kuhakikisha wanapitia mwongozo huo mpya ili kutoa tiba stahili kwa upekee kulingana na makundi mbalimbali ya wagonjwa wa TB kwenye jamii.

Mkurugenzi wa WHO anyehusika na mpango wa kifua kikuu duniani Dkt.Tereza Kasaeva amesema mwongozo huo umetolewa kwakuzingatia zaidi wagonjwa na kuhakikisha wanapata kiwango cha juu zaidi ya huduma. 
“Ni muhimu kuhakikisha kwamba watu wote wanaougua TB wanapata huduma ya kutosha na usaidizi unaohitajika wakati wote wamatibabu ili kuwawezesha kukamilisha matibabu yao na kuwa na matokeo chanya.”

Mchoro wa mfano wa bakteria sugu ya kifua kikuu ya Mycobacterium.
CDC/Alissa Eckert, James Archer
Mchoro wa mfano wa bakteria sugu ya kifua kikuu ya Mycobacterium.

Yapi mapya kwenye mwongozo

Kwa mara katika mwongozo mzima wa matibabu ya TB kumewekwa mwongozo mahususi wa kutekeleza utoaji elimu ya afya, ushauri nasaha, huduma shufaa pamoja na usaidizi wa kijamii, kuweko na chaguzi za usimamizi wa matibabu bila kusahau teknolojia ya ufuatiliaji kidigitali.

Kitabu hicho pia kimetoa mwongozo wa vitendo kuhusu jinsi ya kuweza chaguzi za matibabu zinazopendekezwa kwa kiwango kinachohitajika ili kufikia matokeo ya kitaifa na kimataifa yanayotakiwa katika kuboresha matokeo ya matibabu ya kifua kikuu. 

Mwongozo huo umehimiza nchi na watunga sera kusimamia sura mbili ambazo wamezitaja kuwa ‘muhimu zaidi” ambazo ni elimu ya afya na ushauri nasaha, na huduma shufaa.
Pia mwongozo umetoa taarifa ya masuala mbalimbali ya matunzo pamoja na usaidizi wa wagonjwa wa Kifua kikuu katika umri tofauti ikimaanisha Watoto, vijana, watu wanaoishi na VVU na magonjwa nyemelezi yanayoambatana na ugonjwa huo. 

Mwongozo umejadili pia namna ya usimamizi wa TB wakati wa dharura za kiafya. (Mfano janga la COVID-19)

Kusoma kwa undani mwongozo huo bofya hapa.