Tuliangushana na sasa tutainuka pamoja kuilinda baharí

Baada ya wiki ya majadiliano na matukio mbalimbali huko Lisbon, Ureno, hatimaye mkutano wa pili wa Umoja wa Mataifa kuhusu bahari umefunga pazia leo huku wakuu wa serikali na nchi wakipitisha azimio la kisiasa kwa lengo la kuokoa bahari.
Azimio hilo limekiri kuwa hatua za pamoja za mataifa duniani zilikwamisha hatua za kulinda bahari, na hivyo, “viongozi wa dunia wametoa wa hatua makini zaidi na zenye matarajio makubwa kuhakikisha kuwa hali mbaya ya bahari hivi sasa inashughulikiwa,” na wamekiri kwa dhati kuwa wanatiwa hofu kubwa na dharura ya kimataifa inyokumba dunia.
Akizungumza wakati wa ufungaji wa mkutano huo, Mkuu wa masuala ya sheria kwenye Umoja wa Mataifa, Miguel de Serpa Soares, amepongeza serikali za Kenya na Ureno kwa maandalizi bora ya pamoja ya mkutano huo na mafanikio yake.
“Mkutano huu umetupatia fursa ya kujadili masuala mazito na kuibuka na mawazo mapya. Pia umeweka dhahiri kuhusu jukumu lililosalia, na umuhimu wa kuongeza juhudi zaidi katika kunusuru bahari yetu,” amesema Bwana Serpa Soares akiongeza kuwa ni muhimu kuliko wakati wowote ule , kubadili mwekeleo.
Zaidi ya washiriki 6,000 wakiwemo wakuu wa serikali n anchi 24 na zaidi ya wawakilishi 2,000 kutoka mashirika ya kiraia walihudhuria mkutano huo, wakichechemua uharaka au udharura wa hatua makini za kutatua janga linalokumba baharí.
Wakitambua kuwa kwa pamoja dunia imejiangusha katika kufikia malengo ya kunusuru bahari, viongozi wamerejelea upya ahadi zao za kuchukua hatua za dharura na kushirikiana katika ngazi mbalimbali ili kufanikisha malengo yanayotakiwa haraka iwezekanavyo.
Miongoni mwa changamoto zinazokabili dunia, ni pamoja na mmomonyoko wa fukwe, uchafuzi wa bahari, uvuvi wa kupindukia na kupungua kwa bayonuai ya baharini.
Wakikiri kuwa mabadiliko ya tabianchi ni “moja ya changamoto kuwa zaidi ya zama zetu za sasa,” na umuhimu wa “kuamua na kuchukua hatua tena kwa dharura ili kuboresha afya ya bahari, tija, matumizi endelevu ya bahari na mifumo anuai yake,” viongozi hao waliokutana Lisbon wamesisitiza kuwa vitendo bunifu vinavyozingatia sayansi sambamba na ushirikiano wa kimataifa ni muhimu ili kupata majawabu sahihi.
Wakitoa wito kwa mabadiliko ya kina, viongozi hao wamesisitiza umuhimu wa kushughulikia madhara ya muda mrefu ongezeko la joto duniani kwa bahari ikiwemo kumomonyoka kwa mifumo anuai na kutoweka kwa viumbe.
Wakisisitiza kuwa bahari ni msingi wa uhai kwa sayari dunia na mustakabli wa dunia, viongozi hao katika azimio hilo wamesisitiza hasa umuhimu wa kutekeleza Mkataba wa Paris wa Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka 2015, na makubaliano ya mwezi Novemba mwaka jana kutoka mkutano wa mabadiliko ya tabianchi huko Glasgow ili kusaidia kuhakikisha kuwa bahari ina afya, inaleta tija na ina mnepo na zaidi ya yote inatumiwa kiuendelevu.
“Tumeajikita kukomesha na kubadili mwelekeo wa kuporomoka kwa afya ya bahari na mifumo anuai yake na vile vile tumeamua kurejesha mnepo na mfumo ikolojia,” limesema azimio hilo la kisiasa.
Katika mkutano huo, zaidi ya nchi wanachama 150 zilitoa ahadi za kuwa zimelinda au kuhifadhi angalau asilimia 30 ya bahari kwenye maeneo yao tengwa ya hifadhi baharini ifikapo mwaka 2030.
Akizungumzia ahadi hiyo wakati akifunga mkutano kwa niaba ya Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres, Bwana Serpa Soares amesema, “nimetiwa moyo sana na ahadi hizo mpya.”
Wezesha vijana, wanawake na watu wa jamii ya asili
Kwa kutambua umuhimu na dhima ya ufahamu wa kijadi, ubunifu na hatua zinaochukuliwa na jamii ya watu wa asili katika kulinda bahari, bila kusahau yanasi katika mipango na kufanya maamuzi, viongozi hayo wametoa wito wa ushiriki bora zaidi wa jamii zilizo karibu na bahari.
“Kuwezesha wanawake na wasichana kama washiriki wakuu na sawa, ni muhimu katika kufikia lengo namba 14 la malengo ya maendeleo endelevu, SDGs kuhusu Uhai chini ya Maji” limesema azimio hilo huku pia likitaka vijana wapatiwe mamlaka ya kuwawezesha kuchangia katika afya ya bahari ikiwemo kwenye maamuzi na mipango.