Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sayansi na sera zishirikiane ili kusaidia bahari

Wanabiolojia wa baharini hufanya utafiti kuhusu miamba ya matumbawe
Great Barrier Reef Marine Park Authority/Daniel Schultz
Wanabiolojia wa baharini hufanya utafiti kuhusu miamba ya matumbawe

Sayansi na sera zishirikiane ili kusaidia bahari

Tabianchi na mazingira

Baada ya siku tano za mijadala na maonesho mbalimbali, mkutano wa pili kuhusu baharí umefikia tamati huko Lisbon nchini Ureno ambako Miguel de Serpa Soares ambaye ni Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya kisheria amesema mwelekeo wa kulinda na kuhifadhi baharí unatia matumaini kwa kuzingatia yaliyokubaliwa, changamoto zilizoko sambamba na fursa.  

Bwana Soares anasema suala la sayansi ya baharí akisema linapaswa kupatiwa kipaumbele. Ni katika mahojiano yake na Idhaa ya Umoja wa Mataifa kando ya mkutano huo akisema tumeweka malengo kupitia tamko la kisiasa lakini, tunapaswa kuhakikisha sayansi inachangia kwenye será na hii itawezesha uchukuaji haraka wa hatua  iwapo kuna dalili za kutofikia malengo yetu.” 

Kisha akagusia jamii zinazotegemea baharí akisema, “nadhani tutahitaji pia kutegemea zaidi jamii za maeneo hayo na wenye ufahamu wa kiasili kwa sababu wao wanaathiriwa kila siku na mabadiliko ya baharí, na mchango wao utakuwa muhimu katika kufuatilia maendeleo.” 

Msaidizi huyu wa Katibu Mkuu akataja pia usawa wa kijinsia kwenye sayansi na maeneo mengine akisema, “nadhani wanawake nao ni nguvu kazi kwenye sekta ya baharí na majini na hivyo wao watakuwa pia na mchango mkubwa kwenye michakato ya ufuatiliaji.” 

Amesema ingawa kuna changamoto kama vile kila mtu au kikundi kujifanyia kazi mwenyewe, cha msingi ni ushirikiano, wanasayansi washirikiane na watunga será na bila kusahau ubunifu wa kiteknolojia na ufadhili kuwa ni fursa ya kuleta mabadiliko. 

Bwana Soares amesema mikutano ijayo kama vile wa mkataba wa kimataifa wa kulinda bayoanuai CBD, na ule wa tabianchi huko Misri utaweka fursa wa kufuatilia mkutano kuhusu Bahari ili hatimaye kuweko na matumizi endelevu ya bahari.