Kiwango cha kujua kusoma chaporomoka ikilinganishwa na kabla ya COVID19 :UNESCO

30 Juni 2022

Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na utamaduni UNESCO limesema kunahitajika uhamasishaji wa pamoja ili lengo namba 4 la elimu sawa kwa wote la Malengo ya maendeleo endelevu SDGs liweze kufikiwa.

UNESCO limeeleza hayo hii leo jijini Paris, Ufaransa mbele ya zaidi ya mawaziri kutoka katika nchi 150 duniani wanao hudhuria mkutano wa siku tatu (Juni 28-30) wa maandalizi ya mkutano wa wakuu wa nchi unaotarajiwa kufanyika mwezi Septemba.

Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Audrey Azoulay amesema ni lazima nchi ziweke ajenda hii juu ya ajenda zao za kufikia malengo ya SDGs kwakuwa janga la COVID-19 limefifisha maendeleo yaliyofikiwa kabla kwa sababu mbalimbali ikiwemo mataifa kupunguza bajeti zilizokuwa zimeelekezwa kusaidia masuala ya elimu.

Pengo kubwa kwenye kujifunza

“Janga la COVID-19 limezidisha tatizo la elimu, shule kufungwa kumesababisha hasara kubwa ya kujifunza. Kwenye nchi za kipato cha chini na cha kati asilimia 70ya watoto wenye umri wa miaka 10 hawawezi kuelewa sentensi rahisi ikilinganishwa na mwaka 2019 ambapo walioshindwa kuelewa ilikuwa asilimia 57.” Amesema Azoulay na kuongeza kuwa bila ya kuja na mbinu mpya za kuwasaidia kwa haraka watoto hao watapata matatizo makubwa wakati wakiendelea kupata elimu na kuingia katika soko la ajira. “Na kisha tutapata tatizo kubwa la kijamii.”

Mkurugenzi Mkuu huyo wa UNESCO ametoa wito kwa na kuhamasisha jumuiya za kimataifa kuhakikisha elimu unarejea kuwa kileleni kwenye kutaka kufikia malengo ya maendeleo endelevu.

Mvulana wa miaka minne mwenye usonji wa wastani anapewa usaidizi nyumbani huko Kambodia kwa sababu ya kufungwa kwa shule kwa kukabiliana na COVID-19.
© UNICEF/Thomas Cristofolett
Mvulana wa miaka minne mwenye usonji wa wastani anapewa usaidizi nyumbani huko Kambodia kwa sababu ya kufungwa kwa shule kwa kukabiliana na COVID-19.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF pamoja na Benki ya Dunia tarehe 24 mwezi juni, ucheleweshaji huu wa masomo pia itakuwa na atakuwa na athari kiuchumi. 

katika kiwango cha kimataifa utasababisha jumla ya hasara ya mali kwa kizazi chas asa cha watoto walio shuleni ni dola trilioni 21. Makadirio yaliyotolewa awali mwaka 2021 yalikuwa ni trilioni 17.

 Fedha hakuna

Mbali ya changamoto ya watoto kujifunza tatizo lingine lililo elezwa na UNESCO ni shida ya ufadhili .

Kulingana na utafiti mwingine wa UNESCO na Benki ya Dunia, asilimia 40 ya nchi za kipato cha chini na cha kati zilipunguza matumizi yao ya elimu wakati wa janga la COVID-19. Punguzo la wastani lilikuwa asilimia 13.5. 

Hatahivyo taarifa zilizopatikana mpaka kipindi hiki cha msimu wa joto  mwaka 2022, bajeti bado hazijarejea kwenye viwango vya mwaka 2019.

“Tuna wasiwasi kuhusu kuyumba kwa ufadhili wa elimu katika wakati huu muhimu,” alisema Stefania Giannini, Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa Elimu katika UNESCO. “Ufadhili wa umma unapopungua, familia zinapaswa kuongeza mchango wao wa kifedha. Na kadiri mzigo wa kifedha wa elimu unavyoangukia familia, ndivyo hatari ya kuongezeka kwa kukosekaana kwa  usawa.”

UNESCO wamewakumbusha mawaziri pamoja na wahudhuriaji wengine wa mkutano huo kuwa suala la upatikanaji wa rasilimali ni muhimu zaidi kwani elimu lazima pia ibadilishwe ili kukabiliana na changamoto mpya za karne ya 21.

Ripoti iliyotolewa hivi karibuni na UNESCO kuhusu Mustakabali wa Elimu imeoyesha, mitaala na ufundishaji lazima irekebishwe kulingana na maswala ya sasa kama vile mabadiliko ya tabianchi na mapinduzi ya kidijitali.

Mkutano huo wa UNESCO umehudhuriwa na zaidi ya watu 2000 waliwemo mawaziri manaibu mawaziri na wadau wengine.

Majadiliano hayo yataendelea tarehe 19 Septemba jijini New York, Marekani wakati wa Mkutano wa Kilele wa Mabadiliko ya Elimu, utakaowaleta pamoja wakuu wa nchi na serikali ikiwa ni tukio kubwa lililoitishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres lenye lengo la kuweka elimu katika kilele cha ajenda ya kimataifa.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter