Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miji kuendelea kukua na watu kuongezeka kwa bilioni 2.2 ifikapo 2050: UNHABITAT

Huduma za usafiri wa mwendokasi jijini Dar es salaam nchini Tanzania ni miongoni mwa mipango ya miji ya kuimarisha huduma kwa wakazi kadri inavyozidi kukua
World Bank/Hendri Lombard
Huduma za usafiri wa mwendokasi jijini Dar es salaam nchini Tanzania ni miongoni mwa mipango ya miji ya kuimarisha huduma kwa wakazi kadri inavyozidi kukua

Miji kuendelea kukua na watu kuongezeka kwa bilioni 2.2 ifikapo 2050: UNHABITAT

Masuala ya UM

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo  na shirika la Umoja wa Mataifa la makazi UN-HABITAT kuhusu hali ya miji mwaka 2022 inasema ukuaji wa haraka wa miji ulicheleweshwa kwa muda tu na janga la COVID-19, na sasa idadi ya watu mijini duniani kote inatarajiwa kuongezeka kwa watu wengine bilioni 2.2 ifikapo 2050. 

Ripoti hiyo imesema kuathirika kwa kiwango kikubwa kwa safari za ndege kutoka kwenye miji mikubwa katika hatua za mwanzo za janga la COVID-19 hadi suala la usalama mashambani au kwenye miji midogo ilikuwa hatua za muda mfupi ambazo hazitabadilisha mwenendo wa ukuaji wa miji ulimwenguni. 

“Licha ya matukio makubwa ya virusi hivyo katika maeneo ya mijini na matatizo ya kiuchumi yanayotokana na janga hili, miji inatumika tena kama miale ya fursa kwa watu wanaotafuta kazi, elimu na mafunzo au kwenda kupata hifadhi kwa sababu ya migogoro.” 

Miji itashamiri kwa kuchukua hatua Madhubuti 

Akizungumzia ripoti hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa UN-HABITAT Maimunah Mohd Sharif amesema “ukuaji wa miji unasalia kuwa mwenendo mkubwa na wenye nguvu katika karne ya 21.  Hiyo inajumuisha pia changamoto nyingi, ambazo zilifichuliwa na kuchochewa zaidi na janga la COVID-19. Lakini kuna hali ya matumaini kwamba COVID-19 imetupa fursa ya kujijenga upya kwa kwa njia tofauti."

Ujenzi wa nyumba zinazohimili mabadiliko ya tabianchi huko Msumbiji baada ya miji ya pwani kupigwa na vimbunga Idai na Kenneth.
UN-Habitat/Veridiana Mathieu
Ujenzi wa nyumba zinazohimili mabadiliko ya tabianchi huko Msumbiji baada ya miji ya pwani kupigwa na vimbunga Idai na Kenneth.

Amesisitiza "kwa sera zinazofaa na dhamira sahihi kutoka kwa serikali, watoto wetu wanaweza kurithi maisha ya baadaye ya mijini ambayo ni jumuishi zaidi, yanayojali mazingira, salama na yenye afya zaidi. Lazima tuanze kwa kukiri kwamba hali iliyotangulia hadi 2020 ilikuwa kwa njia nyingi mfano usio endelevu wa maendeleo ya mijini, na kuzingatia tuliyojifunza katika mhatua zetu dhidi ya COVID-19 na mabadiliko ya tabianchi." 

Mkuu huyo wa UNHABITAT pia ameonya kwamba "maono ya mustakabali endelevu na wenye usawa mijini hayatafikiwa hadi pale miji na serikali zitakapochukua hatua muhimu na madhubuti kushughulikia changamoto sugu na zinazoibuka za mijini" 

Ripiti imeongeza kuwa huku idadi ya watu waliopo mijini pia ikiendelea kukua kutokana na ongezeko la watu wanaozaliwa haswa katika nchi za kipato cha chini, idadi ya watu mijini inatabiriwa kuongezeka kutoka asilimia 56 ya jumla ya watu wote duniani 2021 hadi asilimia 68 ifikapo 2050. 

Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba asilimia 68 ya wakazi wa dunia watakuwa wanaishi katika miji kwa mfano Nairobi nchini Kenya.
© UN-Habitat/Kirsten Milhahn
Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba asilimia 68 ya wakazi wa dunia watakuwa wanaishi katika miji kwa mfano Nairobi nchini Kenya.

Miji itaendelea kuwepo daima 

Ripoti imehitimisha kuwa "miji iko hapa daima, na mustakabali wa binadamu bila shaka ni wa mijini,” ingawa inasema kuwa viwango vya ukuaji wa miji havilingani, huku ukuaji ukipungua katika nchi nyingi za kipato cha juu. 

Ripoti hiyo ya mustakbali wa miji iliyotolewa wiki hii ili kwenda sanjari na mkutano wa 11 wa Jukwaa la miji duniani, ambao ni mkutano mkuu wa kimataifa wa maendeleo endelevu ya miji unaonafanyika Katowice, Poland, kuanzia tarehe 26-30 Juni, ukiandaliwa kwa ushirikiano wa UN-Habitat na kuratibiwa pamoja na serikali ya Poland na jiji la Katowice. 

Huku kukiwa na onyo kuhusu hatari zinazoikabili miji, kutokana na ongezeko la ghafla la mfumuko wa bei duniani na gharama ya maisha, changamoto za ugavi, mabadiliko ya tabianchi na migogoro mipya ya kivita, ripoti hiyo inaeleza maono yenye matumaini ambapo miji itakuwa na usawa zaidi, kujali mazingira na yenye msingi wa maarifa zaidi. 

Ripoti hiyo ya kila mwaka ni mtazamo wa mamlaka, wa kina na wenye kuona mbali kuhusu hali ya miji duniani, ikitoa mwelekeo wa sera ya miji na mtazamo wa maendeleo endelevu.