Uhalalishaji bangi umeongeza matumizi ya kila siku – Ripoti

27 Juni 2022

Ripoti ya Dunia ya Dawa za Kulevya ya UNODC 2022 inaangazia mwelekeo wa kuhalalisha bangi baada ya kuhalalishwa, athari za kimazingira za dawa haramu, na matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa wanawake na vijana. 

Uhalalishaji wa bangi katika sehemu kadha za dunia unaonekana kuongeza kasi matumizi ya kila siku na athari zinazohusiana na afya, kwa mujibu wa Ripoti ya kimataifa ya mwaka huu 2022 iliyotolewa leo kuhusu Dawa za Kulevya ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Dawa na Uhalifu (UNODC). 

Ripoti hiyo pia inaeleza kuongezeka kwa rekodi katika utengenezaji wa cocaine, kuongezeka kwa dawa za kemikali kwenye masoko mapya, na kuendelea kwa mapungufu au mapengo katika upatikanaji wa matibabu ya madawa ya kulevya, hasa kwa wanawake. 

Mifereji ya kuvutia bangi ikiuzwa mjini New York, Marekani
UN News/Elizabeth Scaffidi
Mifereji ya kuvutia bangi ikiuzwa mjini New York, Marekani

Vile vile kwa mujibu wa ripoti hiyo, takribani watu milioni 284 wenye umri wa miaka 15-64 walitumia dawa ulimwenguni kote mnamo 2020, ongezeko la asilimia 26 katika muongo uliopita. “Vijana wanatumia dawa nyingi zaidi, na viwango vya matumizi leo katika nchi nyingi ni vya juu kuliko kizazi kilichopita. Barani Afrika na Amerika Kusini, watu walio chini ya umri wa miaka 35 wanawakilisha watu wengi wanaotibiwa matatizo ya matumizi ya dawa za kulevya.” Imeeleza taarifa ya UNODC iliyotolewa kwa vyombo vya habari hii leo mjini Vienna, Austria.  

Ulimwenguni, ripoti hiyo inakadiria kuwa watu milioni 11.2 kote ulimwenguni walikuwa wakijidunga madawa ya kulevya. Karibu nusu ya idadi hii walikuwa wanaishi na ugonjwa wa hepatitis C, milioni 1.4 walikuwa wanaishi na Virusi Vya UKIMWI, VVU, na milioni 1.2 walikuwa wanaishi na magonjwa yote mawili. 

Akitoa maoni yake kuhusu matokeo haya, Mkurugenzi Mtendaji wa UNODC Ghada Waly amesema: "Idadi za utengenezaji na ukamataji wa dawa nyingi haramu zinafikia rekodi ya juu, wakati dharura za kimataifa zinazidisha udhaifu. Wakati huo huo, imani potofu kuhusu ukubwa wa tatizo na madhara yanayohusiana nayo ni kuwanyima watu matunzo na matibabu na kuwafanya vijana kuelekea kwenye tabia mbaya. Tunahitaji kutoa rasilimali zinazohitajika na umakini katika kushughulikia kila kipengele cha tatizo la madawa ya kulevya duniani, ikiwa ni pamoja na utoaji wa huduma inayotegemea ushahidi kwa wote wanaohitaji, na tunahitaji kuboresha msingi wa maarifa kuhusu jinsi dawa haramu zinavyohusiana na changamoto zingine za dharura kama vile migogoro na uharibifu wa mazingira.” 

Shamba la bangi Pitomača, Croatia.
Unsplash/David Gabrić
Shamba la bangi Pitomača, Croatia.

Ripoti hiyo pia inasisitiza zaidi umuhimu wa kuitia nguvu jumuiya ya kimataifa, serikali, mashirika ya kiraia na wadau wote kuchukua hatua za haraka za kuwalinda watu, ikiwa ni pamoja na kuimarisha kinga na matibabu ya matumizi ya dawa na kukabiliana na usambazaji wa dawa haramu.  

Dalili za mapema na athari za kuhalalisha bangi 

“Uhalalishaji wa bangi huko Amerika Kaskazini inaonekana kumeongeza matumizi ya kila siku ya bangi, hasa bidhaa zenye nguvu za bangi na hasa miongoni mwa vijana.” Ongezeko linalohusishwa la watu walio na shida ya akili, kujiua na kulazwa hospitalini pia kumeripotiwa. “Uhalalishaji pia umeongeza mapato ya ushuru na kwa ujumla kupunguza viwango vya kukamatwa kwa umiliki wa bangi.” 

Kuendelea kukua kwa uzalishaji na biashara ya madawa ya kulevya 

Utengenezaji wa Cocaine ulikuwa wa juu zaidi mnamo mwaka 2020, ukikua kwa asilimia 11 kutoka mwaka 2019 hadi tani 1,982. Ukamataji wa Cocaine pia uliongezeka, licha ya janga la Covid-19, hadi rekodi ya tani 1,424 mnamo mwaka 2020. Takriban asilimia 90 ya Cocaine iliyokamatwa ulimwenguni mnamo mwaka 2021 ilikuwa inasafirishwa katika kontena au baharini.  Takwimu za ukamataji zinapendekeza kuwa ulanguzi wa Cocaine unaenea hadi maeneo mengine nje ya soko kuu la Amerika Kaskazini na Ulaya, na viwango vya kuongezeka kwa usafirishaji hadi Afrika na Asia. 

Katika nchi nyingi barani Afrika na Amerika Kusini na Kati, idadi kubwa zaidi ya watu wanaotibu matatizo ya matumizi ya dawa za kulevya wapo hasa kwa matatizo ya utumiaji bangi. Katika Ulaya ya Mashariki na Kusini-Mashariki na Asia ya Kati, watu mara nyingi wako katika matibabu ya matatizo ya matumizi ya madawa mengine ya kulevya, ‘unga’. 

Athari za kimazingira za soko la dawa 

Masoko haramu ya dawa za kulevya, kwa mujibu wa Ripoti ya Dunia ya Dawa za Kulevya ya 2022, inaweza kuwa na athari za kimaeneo, jamii au kiwango cha mtu binafsi kwa mazingira. Matokeo muhimu ni pamoja na kwamba alama ya ukaa ya bangi inayolimwa ndani ni kati ya mara 16 na 100 zaidi ya bangi ya nje kwa wastani na kwamba alama ya kilo 1 ya cocaine ni kubwa mara 30 kuliko ile ya maharagwe ya kakao. 

Athari zingine za kimazingira ni pamoja na ukataji mkubwa wa miti unaohusishwa na kilimo haramu cha Cocaine, taka zinazozalishwa wakati wa utengenezaji wa dawa haramu za kemikali za ambazo zinaweza kuwa mara 5-30 ya ujazo wa bidhaa iliyokamilika, na utupaji wa taka ambayo inaweza kuathiri udongo, maji na hewa moja kwa moja, na vile vile viumbe, wanyama na mnyororo wa chakula kwa njia isiyo ya moja kwa moja. 

Pengo linaloendelea la matibabu ya kijinsia na tofauti katika matumizi na matibabu ya dawa za kulevya 

Wanawake wamesalia katika kundi la wachache wa watumiaji wa madawa ya kulevya duniani kote lakini bado wana mwelekeo wa kuongeza kiwango chao cha matumizi ya madawa ya kulevya na kuendelea na matatizo ya matumizi ya madawa ya kulevya kwa kasi zaidi kuliko wanaume. Wanawake sasa wanawakilisha wastani wa asilimia 45-49 ya watumiaji wa ‘amphetamines’ na watumiaji wasio wa kimatibabu wa vichangamshi vya dawa na dawa za kutuliza mwili.  

“Pengo la matibabu bado ni kubwa kwa wanawake ulimwenguni kote.” UNODC inaeleza.   

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter