Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bahari inatupeleka popote, tuitunze- Guterres

Ufunguzi wa mkutano kuhusu bahari huko Lisbon, Ureno 27 Juni 2022
UN /Eskinder Debebe
Ufunguzi wa mkutano kuhusu bahari huko Lisbon, Ureno 27 Juni 2022

Bahari inatupeleka popote, tuitunze- Guterres

Tabianchi na mazingira

Mkutano wa pili wa Umoja wa Mataifa kuhusu bahari umeanza leo huko Lisbon Ureno ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ni lazima kubadili mwelekeo na mwenendo wa shughuli za binadamu kwa bahari la sivyo uchafuzi wa bahari utavuruga harakati zote za kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs

Mchango wa bahari kwa binadamu

"Bahari inatupeleka popote", ndivyo alivyokuwa anatamatisha hotuba yake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo huko Lisbon kwa lugha ya kiswahili kwenye mkutano huo wa baharí ulioandaliwa kwa pamoja na Kenya na Ureno.

Katibu Mkuu alitumia methali hiyo ya Kiswahili kwa kuwa alianza hotuba yake kwa lugha ya kireno.
Guterres amesema Bahari inatupeleka popote  kwa kuzingatia kuwa inaweza kufungua fursa mpya na mustakabali endelevu iwapo itatunzwa na kuwa na afya kwa sababu, “ni tegemeo la lishe kwa zaidi ya watu bilioni moja. Ni chanzo cha ajira kwa watu wapatao milioni 40. Na baharí yenye afya na fanisi ni muhimu kwa mustakabali wetu wa pamoja.”

Amesema baharí inazalisha zaidi ya nusu ya hewa ya oksijeni inayovutwa na binadamu.

Hali ni tete

Hata hivyo amesema hali ni tete, “hatukujali baharí hadi tunakabiliwa na kile ninachokiita dharura ya baharí.”
 

Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia wakati wa ufunguzi wa mkutano kuhusu bahari unaofanyika Lisbon, Ureno.
UN /Eskinder Debebe
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia wakati wa ufunguzi wa mkutano kuhusu bahari unaofanyika Lisbon, Ureno.

Amesema kiwango cha maji ya bahari kinaongezeka, visiwa vidogo vinazama, kiwango cha tindikali kwenye baharí kinaongezeka na takribani asilimia 80 ya majitaka yanaingia baharini bila kuondolewa sumu.

Kama hiyo haitoshi, matumbawe yanabadilika rangi na yanatokomea kwa sababu ya tindikali.
 
Mifumo ya anuwai hasa maeneo ya fukwe na pwani kama vile mikoko na maeneo oevu yanaharibika.

Uchafuzi kutoka maeneo ya barani yanasababisha fukwe za baharí kufa, “na tani milioni 8 za taka za plastiki zinaingia baharini kila mwaka. Bila hatua za dharura, taka za plastiki zinaweza kuwa nyingi baharini kuliko samaki ifikapo mwaka 2050.”
 
Guterres amesema si jambo la ajabu hivi sasa kukuta taka za plastiki kwenye maeneo ya ndani zaidi ya dunia na hata chini kabisa ya bahari.

“Taka za plastiki zinaua viumbe vya baharini na zina madhara makubwa kwa jamii za pwani ambazo zinategema baharí kama chanzo cha kujipatia kipato bila kusahau utalii,” amesema Katibu Mkuu akitaja pia uvuvi usio endelevu ambao amesema umeshamiri.

Hata hivyo apongeza hatua zinazochukuliwa

Anold Kayanda
Ni muhimu kuanza kufundisha watoto kuhusu kuilinda bahari - Katana Charo Hinzano wa Kilifi, Kenya.

Katibu Mkuu amesema anatambua kuwa kuna hatua bora zinachukuliwa kulinda baharí akitaja wito wa kuchukua hatua kufuatia mkutano wa kimataifa wa baharí uliofanyika miaka mitano iliyopita wa kutaka kurejesha afya ya baharí na shughuli zake za kuleta tija.

“Tangu wakati huo, jamii zimekuwa pamoja kulinda rasilimali za baharini ambazo wanazitegemea. Ubia wa kimataifa umefanya kazi kutenga maeneo ya bahari ili kuwezesha kurejea katika hali ya kawaida. Na kule ambako hatua bora za usimamizi zimechukuliwa, uvuvi umerejea tena,” amesema Katibu Mkuu.
 
Amepongeza pia hatua zinazoendelea za kupitisha mkataba mpya wa kimataifa wa kushughulikia janga la taka za plastiki ambazo zinaharibu bahari.

Mapendekezo manne kutoka kwa Guterres

Ametaja mambo manne ya kuzingatiwa kuwa ni pamoja na,  Mosi, wadau wote kuwekeza kwenye matumizi endelevu ya baharí.

Amesema lengo namba 14 la malengo ya maendeleo endelevu kuhusu Uhai chini ya Maji hufadhiliwa au hupatiwa mkazo kidogo ikilinganishwa na malengo mengine “Usimamizi endelevu wa baharí unaweza kusaidia baharí kuzaliha chakula mara sita zaidi na kutoa nishati rejelezi mara 40 zaidi kuliko hivi sasa,” amesema Guterres.

Amesema dunia inahitaji miundo ya biashara endelevu kwa ajili ya uchumi utokanao na baharí ili kuweko na mazingira bora ya baharí na upatikanaji endelevu wa vyakula kutoka baharini.

Pili Bahari iwe muundo wa kuonesha jinsi ya kutumia kwa pamoja rasilimali kwa faida ya wote, akimaanisha kuzuia na kupunguza uchafuzi wa aina yoyote kwa baharí iwe kutoka maeneo ya bara au vyanzo vingine vya maji.

Tatu amesema, “sote lazima tulinde baharí na watu wanaoishi na kuitegemea na nne, sayansi na ugunduzi vituchagize kufungua sura mpya ya hatua za kulinda baharí.”

Katibu Mkuu ametaka kila mtu atekeleze wajibu wake ili kuleta mabadiliko chanya kwa baharí na kwa binadamu.