Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatuwezi kuruhusu tatizo la mihadarati kuendelea kuathiri mamilioni ya watu:Guterres

Dawa za kulevya
UNIS
Dawa za kulevya

Hatuwezi kuruhusu tatizo la mihadarati kuendelea kuathiri mamilioni ya watu:Guterres

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema siku ya kimataifa ya ya kupambana na matumizi mabaya ya dawa za kulevya na usafirishaji haramu ya mwaka huu inaangazia athari za changamoto za dawa za kulevya katika majanga ya kiafya na kibinadamu.

Kupitia ujumbe wake wa siku hii Katibu Mkuu amesema “Migogoro, majanga ya tabianchi, watu kulazimishwa kuhama makazi yao na umaskini uliokithiri hutengeneza mazingira mazuri ya matumizi mabaya ya dawa za kulevya huku janga la COVID-19 ikifanya hali kuwa mbaya zaidi.” Wakati huo huo, ameongeza kuwa watu wanaoishi katika hali za dharura za kibinadamu wana uwezekano mdogo sana wa kupata huduma na matibabu wanayohitaji na kustahili. Wakati huo huo, amesema wahalifu wananufaika kutokana na masaibu ya watu, huku uzalishaji wa dawa aina ya coceine ukiwa katika kiwango cha juu sana, na kukiwa na ongezeko la mara tano la kunaswa kwa madawa aina ya methamphetamines na karibu ongezeko la mara nne ya kukamatwa kwa madawa aina ya amfetamini katika muongo mmoja uliopita. Dhamira ya kukomesha janga hili Katika siku hii ya kimataifa dhidi ya matumizi mabaya wa madawa ya kulevya na usafirishaji haramu, Guterres amesema “Tunarejelea dhamira yetu ya kukomesha janga hili na kusaidia wale wanaoangukia kwenye janga hilo.” Ameongeza kuwa hii ni pamoja na kupata suluhisho za sera zisizo za kibaguzi zinazohusu watu, afya na haki za binadamu, zikiungwa mkono na kuimarishwa kwa ushirikiano wa kimataifa ili kukomesha biashara haramu ya dawa za kulevya na kuwawajibisha wale wanaonufaika kutokana na taabu za binadamu wengine. Amesisitiza kuwa ni lazima pia kuimarisha huduma za matibabu na usaidizi zinazotegemea sayansi kwa watumiaji wa dawa za kulevya, na kuwachukulia kama waathiriwa wanaohitaji matibabu badala ya adhabu, ubaguzi na unyanyapaa ikiwa ni pamoja na matibabu kwa wale wanaoishi na magonjwa ya kuambukiza kama vile VVU/UKIMWI na homa ya ini. “Hatuwezi kuruhusu tatizo la dawa za kulevya duniani kuathiri zaidi maisha ya makumi ya mamilioni ya watu wanaoishi katika majanga ya kibinadamu.” Kwa mantiki hiyo amehimiza “Katika siku hii muhimu, tujitolee kuondoa kivuli hiki mara moja na kwa wote, na kulipa suala hili umakini mkubwa na hatua zinazostahiki.”