Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres azindua ajenda ya hatua kukabili ukimbizi wa ndani

Mtoto mkimbizi raia wa Angola akiwa mapumziko katika shule nchini Zambia
UN News
Mtoto mkimbizi raia wa Angola akiwa mapumziko katika shule nchini Zambia

Guterres azindua ajenda ya hatua kukabili ukimbizi wa ndani

Wahamiaji na Wakimbizi

Dunia yetu inakabiliwa na janga la ukmbizi wa ndani! Ndivyo alivyoanza ujumbe wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ujumbe ambao ametoa leo kwa njia ya video kuzindua ajenda yake ya hatua dhidi ya ukimbizi wa ndani.

Katibu Mkuu ansema takwimu za watu waliosalia wakimbizi wa ndani kwenye nchi zao duniani kote zinatisha kwani zimefika viwango vya juu, “ watu hawa wamekuwa wakimbizi wa ndani kutokana na vita, majanga na janga la tabianchi.”

Kwa wengine, anasema Katibu Mkuu, “wamefurushwa makwao miaka mingi n ahata miongo, na wakati mwingine wanafurushwa mara kwa mara  huku wengine wakilazimika kukimbia makwao hivi karibuni,” akigusia vita ya Ukraine.

Guterres anasema katika kipindi cha miezi mitatu, vita nchini Ukraine imefurusha watu milioni 13 kutoka majumbani mwao,jamii zao na takribani theluthi mbili wamesalia ndani ya Ukraine.

Sote tuna jukumu la kusaka suluhu ya kuwasaidia

Katibu Mkuu anasema kila mtu ana wajibu wa kusaka majawabu ya kumaliza zahma inayokumba wakimbizi wa ndani.

“Leo nazindua Ajenda ya Hatua dhidi ya Ukimbizi wa Ndani,” anasema Katibu Mkuu akisema kuwa anazingatia mapendekezo ya Jopo la Ngazi ya Juu kuhus uukimbizi wa ndani na kwamba ajenda yake sasa ina malengo makuu matatu.

Watoto wakimbizi wa ndani huko Ituri nchini DRC.
UN/Eskinder Debebe
Watoto wakimbizi wa ndani huko Ituri nchini DRC.

Malengo matatu muhimu ya Ajenda ya Hatua dhidi ya Ukimbizi wa Ndani

Mosi: Kusaidia wakimbizi wa ndani kusaka suluhu za kudumu; Pili, kuwa na uwezo mzuri zaidi wa kuepusha majanga ya kufanya watu wakimbie makwao; tatu, kuhakikisha kuna ulinzi bora zaidi na msaada bora zaidi kwa wale ambao tayari ni wakimbizi.

Guterres amesema, “hebu nieleweke:wajibu wa kumaliza ukimbizi wa ndani kwanza kabisa ni wa serikali. Hata hivyo sote tuna wajibu wa kuchukua hatua.
Ametanabaisha kuwa janga la  ukimbizi wa ndani, ni zaidi ya janga la kibinadamu.

“Inahitajika juhudi na hatua mtambuka – zikijumuisha maendeleo, ujenzi wa amani, haki za binadamu, hatua kwa tabianchi na kupunguza athari za majanga.,” amesema Katibu Mkuu.

Ajenda ya Hatua imeweka bayana ahadi kutoka mfumo wa Umoja wa Mataifa na hivyo Katibu Mkuu amesema ,”natoa wito kwa nchi wanachama, taasisi za kifedha za kimataifa na mashirika ya kiraia nao watekeleze wajibu wao.”

Ametamatisha akisema “kwa pamoja, tunaweza kupunguza  machungu ya binadamu na kuweka mustakabali bora kwa wakimbizi wa ndani na wengine waliohama makwao duniani kote.”