Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sanaa ya uchoraji yaepusha vijana na uhalifu huku ikipendezesha Goma

Muonekano wa ukuta uliochorwa na kupakwa rangi ukiwa na ujumbe mbalimbali. Hapa ni kitongoji cha Karisimbi mjini Goma jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC
UN News/Esther Nsapu
Muonekano wa ukuta uliochorwa na kupakwa rangi ukiwa na ujumbe mbalimbali. Hapa ni kitongoji cha Karisimbi mjini Goma jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC

Sanaa ya uchoraji yaepusha vijana na uhalifu huku ikipendezesha Goma

Amani na Usalama

Huko Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, wasanii vijana wanatumia sanaa  ya upakaji kuta rangi kama njia mojawapo ya kuhamasisha jamii kuachana na ghasia sambamba na kueneza kauli za chuki. 

Kuta za baadhi ya maeneo zimechorwa picha zenye ujumbe tofauti tofauti ! Mathalani  Tusitupe mawe na tusichome matairi kwenye barabara ! Tunatakataa Ujeuri ! Tulinde na Tukinge mazingira!

Ujumbe katika kuta hizi ni sehemu ya mradi wa Vijana Pamoja Jenga Nchi, au VIPAJI uliozinduliwa mwezi uliopita na Taasisi ya Sanaa ya Kivu, AKA, taasisi ambayo ni kituo cha tafiti za kitamaduni na ujasiriamali na makao yake ni Goma.

Sanaa inaendelea ya uchoraji ambapo AKA imekaribisha vijana wapendao sanaa hii kutoka mji wa Bukavu, jimboni Kivu Kusini, halikadhalika vijana kutoka mikoa jirani ya Rwanda kama vile Gisenyi.

Mradi lengo lake ni kusongesha amani, kuondokana na ghasia, elimu ya uraia na kulinda mazingira.

Sasa vijana hawana muda tena wa kubeba silaha

Thierry Vahwere Croki, mwenye umri wa miaka 37 ni miongoni mwa waanzilishi wa mradi huu na amekuweko kwenye sanaa hii kwa miaka 17 sasa anafurahi kufanya kazi na vijana kwa sababu vijana wanajipatia kipato na kwamba,“hawana muda wa kwenda kuombaomba au kubeba silaha kwa sababu wana kazi na wana kitu cha kufanya.”

Léon Shika, Christian Mbevarts, Christian Iturab na Nicolas ni miongoni mwa vijana wachoraji na wapaka rangi kupitia mradi wa VIPAJI
UN News/ Esther Nsapu
Léon Shika, Christian Mbevarts, Christian Iturab na Nicolas ni miongoni mwa vijana wachoraji na wapaka rangi kupitia mradi wa VIPAJI

Na zaidi ya yote mradi ni muhimu kwa mji wa Goma wenye wakazi takribani milioni 2 kwa kuwa, “tunauvisha Goma vazi jipya! Michoro hii inapendezesha na siku hizo na teknolojia vijana wengi wana simu janja wakipita wanasoma ujumbe, wanapiga picha na kusambaza pia ujumbe kwa familia, ndugu na jamaa, shuleni na hivyo tunachora picha na kujisogeza karibu na jamii, vijana na wakati huo huo kuvunja fikra potofu.”

Kijana Croki  anasema, « kama tunavyofahamu vita pamoja na mlipuko wa volkano ya mlima Nyiragongo na kwa kukaribia kwa uchaguzi, ni wakati muafaka kuhamasisha vijana umuhimu wa kuimarisha amani, kuwapatia elimu ya uraia na utawala bora. »

Anafafanua kuwa kila mtu anapaswa kubeba tofali la kujenga msingi wa amani. « Amani ni ya kila mtu. Sote tunapaswa kukutana na kusaka amani ambayo kwa muda mrefu imesahaulika kwenye taifa letu na kwenye ukanda huu. »

Mimi si mkorofi

Mradi huu wa VIPAJI, unaohusisha vijana wote, umekuja wakati mvutano kati ya Rwanda na DRC umepamba moto ambapo kijana Croki anasema, « sisi ni vijana. Sisi ni sehemu ya majawabu. Congo ni yetu sote. Kwa pamoja tuna nguvu, hakuna chochote bila sisi. »

Ni baadhi ya ujumbe ambao wasanii hao wa AKA wanataka kuona na mustakabali bora kupitia sanaa.

Thierry Croki, mchoraji akiwa mbele ya moja ya kuta zilizopakwa rangi na michoro kupitia mradi wa VIPAJI
UN News/Esther Nsapu
Thierry Croki, mchoraji akiwa mbele ya moja ya kuta zilizopakwa rangi na michoro kupitia mradi wa VIPAJI

Kuta ndefu zilipakwa rangi ziko katika maeneo matano huko Goma, na maeneo hayo ni Ulpgl, Katoyi, Kituo cha michezo, ofisi ya Cafod na ofisi ya AKA huko Nyiragongo. 

Kwa kijana mmoja mchoraji, ujumbe usemao, “mimi ni kijana na si mkorofi” umechorwa katika kuta wilaya ya Katoyi kwa sababu eneo hili katika manispaa ya Karisimbi linatambuliwa kuwa eneo korofi kwa ghasia.

Mbunifu huyu wa sanaa hii anasema, « wakati wa maandamano, vijana huchoma moto matairi barabarani na hatua hii huibua mzozo kati yao na polisi. Na hii ndio sababu ya kutaka vijana wasiwe wakorofi.”

Amegusia pia uhifadhi wa mazingira akisema ni sehemu ya mradi wao.