Watoto milioni 8 wako katika hatari ya kifo kutokana na uzito mdogo kupindukia:UNICEF 

Mtoto mwenye umri wa miezi 7 akichnguzwa utapiamlo unaochochewa na ukame mkali nchiin Somalia.
© UNICEF/Sebastian Rich
Mtoto mwenye umri wa miezi 7 akichnguzwa utapiamlo unaochochewa na ukame mkali nchiin Somalia.

Watoto milioni 8 wako katika hatari ya kifo kutokana na uzito mdogo kupindukia:UNICEF 

Afya

Takriban Watoto milioni 8m walio na umri wa chini ya miaka 5 katika nchi 15 zinazokabiliwa na majanga wako katika hatari ya kifo kutokana na uzito mdogo kupindukia endapo hawatapata haraka matibabu ya lishe na huduma zinazotakiwa limeonya leo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF. 

Onyo hilo limetolewa leo mjini Geneva Uswisi wakati viongozi wa dunia kutoka nchi saba tajiri zaidi duniani au G7 wakijiandaa kwa mkutano wao 

Kwa mujibu wa UNICEF idadi ya watoto walioathirika inaongezeka kila dakika na tangu kuanza kwa mwaka huu, kuongezeka kwa mgogoro wa chakula duniani kumewalazimu watoto 260,000 zaidi au mtoto mmoja kila sekunde 60 kuteseka kutokana na uzito mdogo kupindukia katika nchi 15 zinazobeba mzigo mkubwa wa mgogoro huo, ikiwa ni pamoja na matifa katika Pembe ya Afrika na Sahel ya kati.  

Ongezeko hili la upotevu mkubwa wa uzito kupindukia ni pamoja na viwango vilivyopo vya utapiamlo wa watoto ambavyo UNICEF mwezi uliopita ilionya kuwa umefurutu ada. 

Mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Catherine Russell amesema “Hivi sasa tunashuhudia hali mbaya sana ya viwango vya Watoto kupoteza uzito kupindukia n ani hali inayoonghezeka kwa kasi. Hivyo msaada wa chakula ni muhimu, lakini hatuwezi kuokoa watoto wenye njaa na mifuko ya ngano. Tunahitaji kuwafikia watoto hawa sasa na matibabu muhimu kabla hatujachelewa.” 

Mama akimlisha mtoto wake mwenye utapiamlo mkali katika zahanati nchini Ethiopia
© UNICEF/Esiey Leul
Mama akimlisha mtoto wake mwenye utapiamlo mkali katika zahanati nchini Ethiopia

Ongezeko la bei ya chakula 

Kwa mujibu wa UNICEF kupanda kwa bei ya vyakula kutokana na vita nchini Ukrainia, ukame unaoendelea kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa katika baadhi ya nchi, nyakati fulani pamoja na migogoro, na athari zinazoendelea za kiuchumi za COVID-19 vinaendelea kuwa sababu ya kuongeza uhaba wa chakula na lishe kwa watoto duniani kote, na hivyo kusababisha viwango vya maafa ya utapiamlo mkali au unyafuzi kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 5.  

Katika kukabiliana na hali hiyo, UNICEF inaongeza juhudi zake katika nchi 15 zilizoathiriwa Zaidi zikiwemo Afghanistan, Burkina Faso, Chad, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Ethiopia, Haiti, Kenya, Madagascar, Mali, Niger, Nigeria, Somalia, Sudan Kusini, Sudan na Yemen ambazo zitajumuishwa katika mpango wa kuongeza kasi wa kusaidia kuzuia mlipuko wa vifo vya watoto na kupunguza athari za muda mrefu za uzito mdogo kupindukia kwa Watoto hao. 

Uzito mdogo wa kupindukia ni wakati ambapo watoto wanakuwa wembamba sana ukilinganisha na urefu wao  na ni aina yenye hatari inayoonekana zaidi ya utapiamlo.  

Wanakijiji wanalima mazao ya aina mbalimbali za vyakula ili kusaidia kuzuia utapiamlo kwa watoto katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
© UNICEF/Gwenn Dubourthoumi
Wanakijiji wanalima mazao ya aina mbalimbali za vyakula ili kusaidia kuzuia utapiamlo kwa watoto katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Hatari ya kifo 

UNICEF imesema mifumo dhaifu ya kinga huongeza hatari ya kifo kati ya watoto chini ya miaka 5 hadi mara 11 ikilinganishwa na watoto walio na lishe bora. 

Ndani ya nchi hizo 15, UNICEF inakadiria kuwa angalau watoto milioni 40 wana uhaba mkubwa wa lishe, ikimaanisha kuwa hawapati chakula cha kiwango cha chini cha aina mbalimbali wanachohitaji kukua na kuendelea utotoni.  

Zaidi ya hayo, shirika hilo linasema watoto milioni 21 wana uhaba mkubwa wa chakula, ikimaanisha kukosa chakula cha kutosha kukidhi mahitaji ya chini ya chakula, na kuwaacha katika hatari kubwa ya kuathirika vibaya. 

 Wakati huo huo, bei ya vyakula vilivyo tayari kutumika kutibu upotevu mkubwa wa uzito vimepanda bei kwa asilimia 16 katika wiki za hivi karibuni kutokana na kupanda kwa kasi kwa gharama za malighafi, na kuwaacha hadi watoto 600,000 wa zaidi bila kupata matibabu ya kuokoa maisha na kuwa katika hatari ya kifo. 

Ombi la dola bilioni 1.2 

Wakati viongozi wakijiandaa kukutana katika mkutano wa G7, UNICEF imeytoa ombi la dola za Marekani bilioni 1.2 kwa ajili ya 

• Kutoa huduma muhimu za lishe na matunzo ili kuepusha kile kinachoweza kuwa mamilioni ya vifo vya watoto katika nchi 15 zenye mzigo mkubwa Zaidi wa tatizo la uzito mdogo kupindukia ikiwa ni pamoja na programu za kuzuia utapiamlo na kulinda lishe ya mama na mtoto miongoni mwa wanawake wajawazito na watoto wadogo, programu za utambuzi wa mapema na matibabu kwa watoto walio na ugonjwa mbaya wa upotevu wa kupindukia wa uzito, na ununuzi, na usambazaji wa vyakula tiba vilivyo tayari kutumika. 

• Kutanguliza kinga na matibabu ya upotevu mkubwa wa uzito katika mipango yote ya kukabiliana na mgogoro wa chakula duniani kwa kuhakikisha mgao wa bajeti unajumuisha afua za kuzuia lishe duni pamoja na chakula cha matibabu ili kushughulikia mahitaji ya haraka ya watoto wanaokabiliwa na upotevu mkubwa wa uzito. 

 “Ni vigumu kueleza maana ya mtoto kupoteza uzito kupindukia lakini unapokutana na mtoto ambaye anaugua aina hii hatari zaidi ya utapiamlo, unaelewa na hautasahau kamwe,” amesema Russell.  

Ameongeza kuwa "Viongozi wa dunia wanaokusanyika Ujerumani kwa mkutano wa mawaziri wa G7 wana fursa ndogo ya kuchukua hatua kuokoa maisha ya watoto hawa. Hakuna wakati wa kupoteza. Kusubiri njaa itangazwe ni kusubiri watoto wafe.”