Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO kutangaza kesho iwapo ndui ya nyani au monkeypox ni tishio kwa afya duniani au la

Vidonda vya monkeypox kwa kawaida vinapatikana kwenye viganja vya mkono.
© CDC
Vidonda vya monkeypox kwa kawaida vinapatikana kwenye viganja vya mkono.

WHO kutangaza kesho iwapo ndui ya nyani au monkeypox ni tishio kwa afya duniani au la

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO kanda ya Afrika limesema kesho shirika hilo litakuwa na kikao cha dharura kuamua iwapo ugonjwa wa ndui ya nyani au Monkeypox ni janga la afya ya umma au la.

Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika, Dkt. Matshidiso Moeti amesema hayo akizungumza na waandishi wa habari huko Brazaville, Jamhuri ya Congo, wakati huu ambapo kumethibitishwa jumla ya wagonjwa 2103 wa  ndui ya nyani katika nchi 42 na kati ya hizo 8 ni za Afrika. 

Amesema katika nchi hizo za Afrika, ugonjwa huo ulisharipotiwa katika mataifa 6 tu ambazo ni Nigeria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Jamhuri ya Congo,  Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, Benin na Cameroon. 

Ghana na Morocco, Liberia, Uganda, Sierra Leone, Ethiopia, Msumbiji na Sudan ni mara ya kwanza wanapata ugonjwa wa Ndui ya nyani. 

Dkt. Moeti amesema kwa kuzingatia kilichotokea na COVID-19 na Afrika ikawa haijajiandaa akisema,

“WHO inaitisha kikao cha dharura cha kamati ya Ndui ya Nyani Alhamisi tarehe 23 mwezi Juni, kutathmini iwapo mlipuko huu ni tishio la afya kwa umma duniani. Lakini kama WHO Afrika tayari tunasaidia nchi kuongeza uwezo wa kuchunguza Ndui ya Nyani na tuko katika mchakato wa kupata vifaa vya upimaji kwa ajili ya bara hili.” 

Kuhusu chanjo amesema,  chanjo mpya na salama ya ugonjwa wa ndui imeidhinishwa kwa ajili ya kukinga Ndui ya Nyani lakini bado hawashauri kuwa itolewe kwa watu wengi.