Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kukomesha ghasia nchini Ukraine ni ufunguo wa kupunguza hatari ya mauaji ya halaiki 

Kikao cha Baraza la usalama kuhusu Ukraine
UN Photo/Manuel Elías
Kikao cha Baraza la usalama kuhusu Ukraine

Kukomesha ghasia nchini Ukraine ni ufunguo wa kupunguza hatari ya mauaji ya halaiki 

Amani na Usalama

Mshauri Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari, Alice Wairimu Nderitu, akizungumza na Baraza la Usalama leo Jumanne; ameangazia hatua kadhaa za kusitisha mapigano; kwake, akiamini kwamba madai ya uwezekano wa uhalifu wa kivita yana nafasi kubwa kuwa yalitekelezwa nchini Ukraine

Baraza la Usalama limekutana leo ili kujadili kuongezeka kwa ghasia nchini Ukraine tangu uvamizi wa Urusi mnamo Februari 24, mwaka huu 2022. 

Bi. Nderitu, akizungumza na Baraza amerejelea kwamba matamshi ya chuki na vitendo vya mauaji ya halaiki ni kinyume cha sheria za kimataifa, na vinatakiwa kuadhibiwa.  

Hatua za kuharakisha usitishaji mapigano 

Kiongozi huyo amekumbusha kwamba kuzuia mauaji ya halaiki pamoja na uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita pia ni wajibu wa nchi wanachama. 

Kuhusu hali ya Ukraine, Alice Nderitu ameangazia kuwa hatua kadhaa zimechukuliwa ili kuharakisha usitishaji mapigano. 

Mbali na maazimio na maombi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, Bi. Nderitu amesema kuwa anatambua uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ICJ, unaotaka kuchukuliwa hatua katika kesi ya tuhuma za mauaji ya kimbari. 

Mshauri huyo pia ameangazia wasiwasi wake kuhusu ripoti za unyanyasaji wa kijinsia na usafirishaji haramu wa binadamu, hasa unaoathiri wanawake na wasichana. 

Mshauri maalum kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari Ngazi: Naibu Katibu Mkuu
Screen capture
Mshauri maalum kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari Ngazi: Naibu Katibu Mkuu

Miongoni mwa hatua nyingine, amesisitiza kwamba Baraza la Haki za Kibinadamu limeunda tume huru ya uchunguzi ya kimataifa ambayo inachunguza madai yote ya ukiukwaji wa haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu. 

Kwa mujibu wake Bi. Nderitu, mwezi Mei, kikao maalum cha 34 cha Baraza la Haki za Kibinadamu kilitoa wito wa kukomeshwa kwa ghasia. Mwendesha mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu alitangaza uamuzi wake wa kuchunguza hali ya Ukraine. 

Kuzuia mauaji ya kimbari 

Akiwa mshauri maalum wa kuzuia mauaji ya kimbari, anasema hayuko katika nafasi ya kufanya uchunguzi zaidi, hata hivyo, ana jukumu la kuzuia mauaji ya halaiki. Katika tathmini yake, “madai tu ya uhalifu wa kimataifa tayari yanaashiria uwezekano kwamba yalifanyika.” 

Kwa njia hii, Nderitu amesisitiza wito wake wa kukomesha vita, kwa ajili ya ulinzi wa raia na kutaka juhudi za kidiplomasia ziharakishwe. 

Aidha amewataka wajumbe wa Baraza la Usalama na wadau kueleza maono shirikishi na kupendekeza ramani ya njia ya kumaliza migogoro ambayo inazingatia kuwa "amani yenyewe ni mchakato ambao haukubaliani na dhuluma". 

Akirejelea ombi la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Alice Nderitu amebainisha kuwa njia ya kidiplomasia ndiyo pekee inayowezekana. Kwake, suluhisho linawezekana kwa kujitolea kwa kila mtu. "Kwa kila ucheleweshaji unaoendelea, kuongezeka kwa mateso ya wanadamu kunaendelea." Amesema.