Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Yoga katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York City (20 Juni, 2022).

UN yaadhimisha siku ya yoga ikisisitiza umuhimu wake kwa afya na maendeleo

UN News/Sachin Gaur
Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Yoga katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York City (20 Juni, 2022).

UN yaadhimisha siku ya yoga ikisisitiza umuhimu wake kwa afya na maendeleo

Afya

Wajumbe na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wametandaza mikeka yao ya yoga na kujinyoosha kwa mitindo mbalimbali ya yoga, katika hafla iliyofanyika nje Jumatatu jioni kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York, kwa lengo la kusherehekea maadhimisho ya nane ya Kimataifa ya siku ya Yoga, ambayo kila mwaka huadhimishwa tarehe 21 Juni.

Mwaka huu shughuli nyingoi za Umoja wa Mataifa zikirejea ana kwa ana , uwanja wa North Lawn uliotawala kijani kibichi ulibadilishwa kuwa eneo dogo la mazoezi kwa ajili ya kipindi cha maonyesho ya yoga, ambapo watu wenye uzoefu na watu wapya wanaokuja na mapenzi ya yoga , walikutana kuburudisha miili yao na akili zao.

Ari ya umoja

Yoga ni mazoezi ya tangu enzi na enzi ya kimwili, kiakili na kiroho ambayo yalianzia India na sasa yanafanywa kwa njia mbalimbali duniani kote.

Neno yoga linatokana na Sanskrit na maana yake ni kujiunga au kuungana, kuashiria muungano wa mwili na dhamira.

Akizindua hafla hiyo, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Abdulla Shahid, alibainisha kuwa kama janga la COVID-19 limevuruga maisha na uwezo wa watu kuishi na kusababisha hofu kubwa na msongo wa mawazo, "mazoezi ya yoga hutumika kama njia ya kuponya mwili, afya ya kiakili na kiroho na ustawi wa binadamu.”

Yoga inafanya kazi 

Mwakilishi wa kudumu wa India kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi T.S. Tirumurti amesema katika nyakati ngumu za janga hili la COVID-19, mamilioni ya watu walikumbatia yoga kama mwenza wao, ili kuwa na afya njema, kukabili msongo wa mawazo na afya ya akili na ni kwa kutambua jukumu hili muhimu la yoga ndio maana maudhui ya mwaka huu ni 'Yoga kwa ubinadamu.

Mwakilishi huyo ameongeza kuwa "Yoga pia inaweza kuwa sehemu muhimu ya mkakati wetu wa kujikwamua vyema kutoka kwenye janga hilo la COVID-19".

Maadhimisho ya kwanza ya ana kwa ana baada ya miaka miwili

Maazimisho yam waka huu yameandaliwa na ubalozi wa kudumu wa India kwenye Umoja wa Mataifa , n ani maadhimisho ya kwanza ya ana kwa ana baada ya miaka miwili sababu ya vikwazo vya janga la COVID-19.

Hafla ya maadhimisho hayo yamepewa kichwa “yoga na mtaalam” yakijumuisha mafunzo ya awali ya kufanya Yoga na mifano ya vitendo iliyoendeshwa na wataalam wa yoga, densi ya yoga iliyofanywa na kikundi cha raga cha India, mazoezi ya kupumua ya pranayama yaliyoongozwa na Isha Yoga, aina mbalimbali za mitindo ya yoga zilizooneshwa na kituo cha Bhakti na mafunzo ya kutafakari yaliendeshwa na taasisi ya Integral Yoga.

Akizungunmzia faida za Yoga Sam Chase, mkufunzi wa Isha Yoga amesema, “Yoga inahusu kuwa katika uzoefu ambao wewe na vitu vingine vyote hamtenganishwi. Na sasa kama unafanya yopga , faida hizo zitakuja , utakuwa na utulivu wa kiakili, na afya ya kimwili.”

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Yoga katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York City, 20 Juni 2022.
UN News/Sachin Gaur
Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Yoga katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York City, 20 Juni 2022.

Akiwa anafanya mazoezi ya yoga tangu akiwa na umri wa miaka Kishore Chandra wa kituo cha Bhakti alifurahi sana kurejea kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa 

Akizungumza na UN News, amesema, “Ninajisikia vizuri sana kurudi kwenye nyasi hizi, kwa sababu mwaka wa 2019 mvua ilikuwa inanyesha, na tulifanya hivyo ndani ya Baraza Kuu, na hivyo ni tangu mwaka 2018 ndio tulikuwa hapa, na  hakuna kitu kizuri kama kuwa ana kwa ana nje na kila mtu."

Ameongeza kuwa "Yoga kwa kweli ni njia ya maisha, sio tu mazoezi japo mazoezi ni moja wapo, lakini kwangu inamaanisha njia ya maisha, kwa sababu asanas hukusaidia kupata kitu maalum, ambacho ni amani ya akili."

Kwa kutambua mvuto wa ulimwengu wa yoga, mwaka 2014 Umoja wa Mataifa ulitangaza tarehe 21 Juni kila mwaka kuwa Siku ya kimataifa ya Yoga baada ya kupitishwa kwa azimio la Baraza Kuu nambari 69/131.

Azimio hilo lilisisitiza kuwa afya ya kimataifa ni lengo la maendeleo la muda mrefu ambalo linahitaji ushirikiano wa karibu wa kimataifa kwa kubadilishana mbinu bora zinazolenga kujenga maisha bora ya mtu binafsi yaliyo na utiifu wa kila aina.

Kishore Chandra wa Kituo cha Bhakti akionesha Yoga asana katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York City.
UN News/Sachin Gaur
Kishore Chandra wa Kituo cha Bhakti akionesha Yoga asana katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York City.

Yoga hutoa mbinu za kuboresha afya na ustawi

Kuhusiana na hilo, shirika la afya duniani WHO pia limezitaka nchi wanachama wake kuwasaidia wananchi wao kupunguza uvivu wa kutofanya mazoezi ya kimiwli ambayo ni miongoni mwa sababu kumi zinazoongoza kwa vifo duniani, na sababu kuu ya hatari ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza, kama vile magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, saratani na kisukari.
Rais wa Baraza Kuu amekumbusha kwamba yoga inahusu umoj, kuunganisha akili, mwili na nafsi.

“Kuboresha afya ya kimataifa ni lengo letu la muda mrefu. Kwa hivyo, sherehe ya leo pia ni fursa ya kukuza maisha endelevu zaidi na mtazamo mzuri wa maisha.”

Pia amesema nguvu ya yoga kama nguvu ya umoja kwa afya njema, furaha na mustakabali mzuri kwa wote.

Jukumu la Umoja wa Mataifa

Kali Morse kutoka taasisi ya Integral Yoga aliongoza mafunzo ya kutafakari akisisitoiza umuhimu wa jukumu ambapo Umoja wa mataifa unaweza kulifanya ni kuelimisha kuhusu faida nyingi za kufanya yoga.
“Kwa kuzingatia ukweli kwamba inafanyika kwenye Umoja wa Mataifa ni muhimu sana kwa sababu Umoja wa Mataifa kila wakati umekuwa ni mahali ambapo natumai tunaweza kuwaleta watu pamoja kufanya maamuzi ambayo ni kwa ajili ya ubinadamu.”

 Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa Sayansi ya Jamii na Binadamu, UNESCO, Gabriela Ramos alishiriki katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Yoga 2022, wakati wa ziara yake rasmi nchini India.
UNESCO New Delhi
Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa Sayansi ya Jamii na Binadamu, UNESCO, Gabriela Ramos alishiriki katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Yoga 2022, wakati wa ziara yake rasmi nchini India.

Amesema ni muhimu "kuwa na siku ya kimataifa ya yoga, ambapo unaweza kuunganisha watu, na kisha kuwa na wasemaji wanaozungumza juu ya jinsi tunavyoweza kutumikia ubinadamu, na kuwajibika kama wanadamu, ulimwenguni kote, ili kuepusha vita na machafuko zaidi."

Maisha yenye afya na ustawi pia yametambuliwa kama kipengele muhimu cha ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu.
Njia ya maisha endelevu

Wataalamu wanaamini kwamba kiini cha yoga ni usawa na kwa hivyo inaweza kuwa chombo muhimu cha kukuza maisha endelevu kulingana na sayari ya dunia.

Sam Chase wa Isha Yoga amedokeza jinsi ambavyo tumeendelea kila wakati kujaribu kurekebisha ubinadamu kwa kusema yaliyo sawa, na nini kibaya, lakini yoga haifuati mtazamo huo.

"Ukifika kwenye uzoefu ambapo kila mtu anayekuzunguka na kila kitu kinachokuzunguka ni sehemu yako, basi hakuna mtu anayepaswa kukufundisha nini ni sawa, na nini kibaya. Utawatendea haki watu walio karibu nawe, utaitendea haki dunia inayokuzunguka kwa heshima kubwa, kwa sababu ni sehemu yako.”

Alisisitiza kwamba “sasa kuliko wakati mwingine wowote hasa kutokana na aina mbalimbali za majanga ya kimazingira yanayoendelea duniani, tunapaswa kuja pamoja kama watu, na kuhakikisha kwamba sayari yetu haitoweki mbele yetu”.