Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Akina mama waliokimbia makazi yao wakiwa na watoto wao wakihudhuria zoezi la tathmini ya njaa ya WFP katika Jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Nigeria: Hali itazidi kuwa mbaya kama msaada wa haraka hautapatikana

© WFP/Arete/Siegfried Modola
Akina mama waliokimbia makazi yao wakiwa na watoto wao wakihudhuria zoezi la tathmini ya njaa ya WFP katika Jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Nigeria: Hali itazidi kuwa mbaya kama msaada wa haraka hautapatikana

Msaada wa Kibinadamu

Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Nigeria ambaye pia ni mratibu wa misaada ya kibinadamu nchini humo Matthias Schmale amesema zaidi wa watu milioni 4.1 kaskazini mashariki mwa nchi hiyo wanahitaji msaada wa haraka wa chakula katika msimu wa mwambo utakao anza hivi karibuni.

Akihutubia katika kikao cha nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi Schmale amesema watu hao ambao wameteseka kutokana na vita kwa miaka 12 wanauhitaji mkubwa na waharaka wa misaada ya kibinadamu hususas katika ukanda wa majimbo ya Borno,Adamawa na Yobe ambapo takwimu za mwaka huu 2022 zinaonesha watu wenye uhitaji ni milioni 8.4.

“Uhaba wa chakula umeonekana dhahiri katika majimbo haya hususan wakati huu shughuli za uendeshaji zikiwa zinauhitaji mkubwa wa ufadhili” amesema Schmale na kutolea mfano “katika jimbo la Yobe, familia hazijapokea msaada wa chakula kwa takriban miezi nane, baadhi ya watu wanakosa chakula kwa siku kadhaa “

Akina mama waliokimbia makazi yao na watoto wao wanahudhuria tathmini ya njaa ya WFP katika Jimbo la Borno, Nigeria.
© WFP/Arete/Siegfried Modola
Akina mama waliokimbia makazi yao na watoto wao wanahudhuria tathmini ya njaa ya WFP katika Jimbo la Borno, Nigeria.

Njaa na utapiamlo

Mwakilishi huyo wa Umoja wa Mataifa nchini Nigeria ameziomba nchi wanachama na jumuiya za kimataifa kusaidia kwa haraka ili kuoka maisha ya wahitaji.

Mwezi Machi mwaka huu wa 2022 chombo cha kutambua maeneo yaliyo hatarini kutokana na uhaba wa chakula “Cadre Harmonisé” katika ukanda wa Sahel na Afrika Magharibi likibainisha kuwa kati ya mwezi Juni hadi Septemba watu milioni 4.1 watakuwa na uhaba wa chakula.

Miongoni mwao, karibu watu 600,000 wanatarajiwa kuwa katika viwango vya dharura (Ngazi ya 4), ikimaanisha ni upungufu mkubwa wa chakula, utapiamlo wa hali ya juu na vifo vingi. Ni katika kipindi hiki cha mwambo ukiingiliana na msimu wa mvua, na kuwa ni kipindi ambacho watoto wanakuwa hatarini kupata magonjwa ya milipuko kwakuwa wanakinga dhaifu kutokana na kukosa lishe. Utapiamlo miongoni mwa watoto unazidi kuwa hatari kaskazini-mashariki.

Takriban watoto milioni 1.74 walio chini ya umri wa miaka mitano wanatarajiwa kukumbwa na utapiamlo uliokithiri huko kaskazini-mashariki na kati ya hao, zaidi ya 300,000 wanatarajiwa kukabiliwa na utapiamlo mkali na wako katika hatari kubwa ya kifo ikiwa hawatapokea matibabu ya haraka.

Juhudi za sekta mbalimbali kusaidia kukabiliana na hali hiyo zinaendelea huku zikihusisha ushirikiano baina ya Umoja wa Mataifa na washirika wengine wa masuala ya kibinadamu. Schmale amesema mpango huo wa ushirikiano unahitaji dola milioni 351, ikiwa ni sehemu ya ombi la jumla la dola bilioni 1.1 kwa Mpango wa Mwitikio wa Kibinadamu wa 2022 ambao umefadhiliwa kwa asilimia 19.6 mpaka sasa “Siwezi kusisitiza vya kutosha, tunahitaji rasilimali leo na sio kesho,” alisema Schmale.

Mpango wa Mwitikio wa Kibinadamu wa 2022 unalenga kusaidia watu milioni 5.5 ukijumlisha kuwatoa katika usaidizi wa dharura, kuwatoa katika mazingira hatarishi na kupunguza mahitaji ya kibinadamu kwa kuzingatia zaidi suluhu za kudumu na kujenga ustahimilivu inapowezekana.