Apu ya kukujulisha muda wa kupaka mafuta kuzuia mionzi mikali ya jua

SunSmartApp ya kumjulisha mwenye simu janja wakati wa kupaka mafuta mwilini ili kuzuia mionzi aina ya Ultraviolet au UV inayoharibu ngozi na macho.
UN
SunSmartApp ya kumjulisha mwenye simu janja wakati wa kupaka mafuta mwilini ili kuzuia mionzi aina ya Ultraviolet au UV inayoharibu ngozi na macho.

Apu ya kukujulisha muda wa kupaka mafuta kuzuia mionzi mikali ya jua

Afya

Mashirika manne ya Umoja wa Mataifa hii leo yamezindua apu iitwayo SunSmart Global UV, ya kumjulisha mwenye simu janja wakati wa kupaka mafuta mwilini ili kuzuia mionzi aina ya Ultraviolet au UV inayoharibu ngozi na macho.

Mashirika hayo, lile la afya duniani, WHO, la kazi, ILO, la mazingira, WMO na la mazingira UNEP yamesema mionzi hiyo hutoka kwenye jua na katika mazingira  ya shughuli zinazoendeshwa na binadamu.

SunSmart Global UV itakupata taarifa utakazo

Taarifa iliyotolewa leo na mashirika hayo katika miji ya Geneva, Uswisi na Nairobi Kenya imesema apu hiyo inayopatikana katika Apple Store na Google Play Store itampatia mtumiaji utabiri wa siku 5 na kumweleza ni wakati gani atumie mafuta ya kuzuia mionzo hiyo kama njia ya kupunguza saratani ya Ngozi na uharibifu wa macho kutokana na mionzi hiyo.

“Apu inaelezea ni wakati gani mtu anapaswa kujikinga na jua,” imesema taarifa hiyo kuhusu Apu hiyo ambayo inaweza kupakuliwa kwenye apu za Appple na Google bila gharama yoyote na kwa sa iko katika lugha za Kiingereza, Kichina, Kifaransa, Kirusi, Kidachi na kispanyola.

Dkt. Maria Neira kutoka Idara ya Mazingira, Tabianchi na Afya katika WHO, amesema, “ushahidi unaonesha kuwa kupigwa na kiwango kikubwa cha mionzi ya UV ni sababu kubwa ya saratani ya ngozi. Kwa hiyo ni muhimu kwa mtu kutambua ni wakati gani ajilinde dhidi ya  mionzi hiyo.”

Amesihi kila mtu atumie apu hiyo kujilinda yeye mwenyewe na watoto wake.

Watu wenye ualbino mara nyingi wanakuwa na uoni hafifu na wanahitaji matunzo maalum ili waweze kujikinga na jua.
Corbis Images/Patricia Willocq
Watu wenye ualbino mara nyingi wanakuwa na uoni hafifu na wanahitaji matunzo maalum ili waweze kujikinga na jua.

Takwimu zinasema nini?

Duniani kote, zaidi ya watu milioni 1.5 waliugua saratani ya Ngozi mwaka 2020. Na wakati huo huo, zaidi ya watu 120,000 duniani kote walikufa kutokana na saratani ya ngozi, ugonjwa ambao una kinga.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa moja ya sababu za saratani za ngozi ni kupigwa na kiwango kikubwa cha mionzi ya UV kunakosababishwa na kupungua kwa unene wa bamba la ozone kutokanako na kemikali zinaozalishwa na binadamu.

Itifaki ya Montreal inalinda bamba la Ozoni ambalo kwa upande wake linalinda afya ya binadamu na mazingira kwa kuzuia mionzi mikali ya UV kutoka kwenye jua isifike duniani.

Meg Seki, Mkurugenzi Mtendaji wa Sekretarieti ya Ozoni kwenye UNEP anasema, “Apu ya SunSmart ni nzuri mno katika kufuatilia mionzi ya UV na nasihi kila mtu atumie.”

SunSmart UV index ni Apu ya kupima kiwango cha mionzi ya UV
UN
SunSmart UV index ni Apu ya kupima kiwango cha mionzi ya UV

Tunahitaji jua lakini si kwa kiwango hatarishi

UNEP inasema kila mtu anahitaji jua ambalo ni chanzo cha Vitamini D, vitamin inayozuia magonjwa kama vile kupinda kwa mifupa au matege na kuvunjika kwa mifupa. “Hata hivyo kiwango kikubwa cha mionzi ya jua ni hatari na huweza kuua. Miezi ya kipindi cha majira ya joto kuna hatari.”

Apu hiyo imezinduliwa leo kwenda sambamba na siku ya kwanza ya msimu wa mwaka huu wa majira ya joto ukanda wa Kaskazini mwa dunia.

Njia nyingine za kujikinga na mionzi ya UV ni pamoja na kupima muda wa kuwa juani, kusaka kivuli pindi mionzi inapokuwa mikali, vaa mavazi ya kujikinga na jua, kofia na miwani na pia tumia mafuta ya kuzuia mionzi kupenya kwenye ngozi.